Pages

2014-12-01

Wananchi waitaka Serikali itengue agizo la Pinda

Siha. Wakazi wa Kata ya Gararagua Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wameiomba Serikali itengue uamuzi uliotolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wa kuridhia kuuzwa kwa shamba la Gararagua lenye ukubwa wa ekari zaidi ya elfu tatu, ili kulipa deni la Sh bilioni 3.9 inalodaiwa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU) na benki ya CRDB.

Akizungumza na wakazi hao juzi, diwani wa Kata ya Gararagua, Josephat Lukumaya alisema wakazi hao hawako tayari kuona shamba hilo likiuzwa kwa mtu binafsi wakati wanalitegemea kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.

Lukumay alisema Serikali inatakiwa kuangalia upya mkataba uliosainiwa baina ya benki ya CRDB na KNCU ilipokuwa ikichukua mkopo huo badala ya kukimbilia kuliuza shamba.

Akizungumza kwa niaba ya wenzake, mkazi wa Kijiji cha Wiri, Sharifu Laiza alisema kama shamba hilo litauzwa, huko kutakuwa ni kutaka kuwanyanyasa wakazi wa kata hiyo ambao wengi wao ni wakulima wanaolitegemea shamba hilo kwa kilimo.

Aliishauri Serikali kuangalia namna nyingine itakayowezesha KNCU kulilipa deni hilo. Naye Israeli Moleli alisema tamko lilitolewa na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Godfrey Zambi kusisitiza kuuzwa kwa shamba hilo ambalo ndani yake kuna eneo lililojengwa shule, hawalikubali .

Zambi, wakati wa mkutano mkuu maalumu wa wanachama wa KNCU uliofanyika hivi karibuni mjini Moshi, alisema shamba hilo litauzwa kwa wazi na fedha zake zitawekwa kwenye akaunti maalumu itakayofunguliwa katika benki ya CRDB.

Mwenyekiti wa KNCU, Maynard Swai alimweleza waziri huyo kuwa wanalazimika kulipa riba ya Sh250 milioni kila mwezi na hadi kufikia jana, walitakiwa kulipa Sh250 milioni zingine kama riba jambo ambalo limekuwa ni mzigo kwa chama hicho.

No comments:

Post a Comment