Pages

2015-01-16

Ama Kweli;Umanamba huu ni tangu enzi za mkoloni utaisha lini?

Mkoa wa Kigoma upo magharibi ya Tanzania. Wakazi wake wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara, zaidi ikiwa zao la Kahawa linalostawi kwa wingi katika eneo zima la Manyovu. 



Historia inaonyesha kwamba enzi za utawala wa kikiloni chini ya Mjerumani na hata Mwingereza baadhi ya watu wa Kigoma walichukuliwa na kupelekwa katika mikoa ya Morogoro, Pwani na Tanga kufanya kazi ya kulima mashamba ya Mkonge.


Watu hawa waliokamatwa kwa nguvu na kupelekwa kufanya kazi mashambani, walijulikana zaidi kwa jina la Maanamba.


Pamoja na hayo bado mkoa huu unakabiliwa na wimbi kubwa la vijana wadogo kutumikishwa katika mashamba ya tumbaku katika mikoa ya Tabora na Katavi na baadhi yao hukatisha masomo na kwenda kulima kwa kisingizio cha hali ngumu ya maisha katika familia zao. Ili kuwapata watoto hao, wamiliki wa mashamba katika mikoa hiyo hutafuta madalali katika vijiji mbalimbali ambao wajibu wao mkubwa ni kuwashawishi wakubali kwenda kufanya kazi ya kilimo cha tumbaku kwa ahadi ya kulipwa vizuri wakati msimu wa kilimo unapomalizika.


Kutokana na hali ngumu ya maisha katika familia zao, watoto wanalazimishwa kuacha shule ili wafanye kazi. Hii ni kuendeleza umanamba.


Licha ya wengi kufahamu juu ya watoto hao kuacha masomo, hasa shule za msingi, hakuna juhudi zozote zinazofanywa na jamii, Serikali na hata asasi za kiraia, kupinga vitendo hivyo.


Unaweza kujiuliza ni kwa namna gani wanafanikiwa kupenya katika vizuizi vya polisi barabarani, vilivyotapakaa maeneo mengi? Kwa nini polisi wasishtuke na kuuliza watoto wengi namna hiyo wanapelekwa wapi?


Ni wazi kwamba madalali wanaoshawishi watoto hao ni watu maalumu ambao pengine wanashirikiana na viongozi kwenye ngazi za vijiji na vitongoji. Wanakoenda wanakumbana na visa vingi, vikiwamo vya kukosa fedha, kufundishwa tabia mbaya na hata kuathirika kisaikolojia.


Mtoto mmoja aliyechukuliwa mwaka 2012 kutoka Kata ya Nyumbigwa wilayani Kasulu na kupelekwa kulima tumbaku mkoani Tabora kwa ahadi ya kulipwa fedha nyingi, alijikuta akiishi huko miaka miwili bila kulipwa chochote kwa madai kwamba ‘bosi’ wake alipata hasara.


Mkazi mmoja wa Kijiji cha Msimba katika Wilaya ya Kigoma, Abasi Sago ambaye aliwahi kutimkia Urambo mkoani Tabora kulima Tumbaku katika miaka ya 2000 anasema alipata shida nyingi kiasi kwamba akisikia mtu anaenda huko anamshauri afadhali abakie kijijini kwake na shida zake kwani zina nafuu.


“Hiyo kazi ya kulima tumbaku ni ngumu sana. Nilikaa Urambo bila mshahara. Nililazimishwa kufanya kila kazi ya nyumbani kwa mwajiri wangu tena bila malipo yoyote hadi nilirudi nyumbani bila kitu. Haya ndiyo maisha yanayowakuta Vijana huko,” anasimulia Sago.


Mimi naamini ni rahisi kutokomeza biashara hii haramu ya usafirishaji wa binadamu pamoja na kukomesha kabisa utumikishwaji wa watoto katika mashamba ya Tumbaku sambamba na sekta nyingine kama vile uvuvi, migodini na kilimo cha mazao mengine hususan ya biashara.

No comments:

Post a Comment