Stori: Na Waandishi Wetu Lindi/Ijumaa Wikienda
WAPIGA kura wa Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, wamemwagia sifa mbunge wao ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi) Kassim Majaliwa, wakisema katika kipindi chake cha miaka mitano inayoelekea mwishoni, amejitahidi kutekeleza ahadi zake alizotoa wakati wa Uchaguzi Mkuu 2010.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti kutoka jimboni na jijini Dar es Salaam, wapiga kura hao walisema wanamshukuru mbunge wao kwa jinsi anavyojitoa kuwasaidia.
“Mbunge wangu ananifanya nitembee kifua mbele kwa sababu karibu asilimia tisini ya ahadi zake amezitekeleza vizuri kabisa, kama ataamua kugombea tena, sioni kwa nini nisimpe kura yangu,” alisema Titus Didas, mwenyeji wa jimbo hilo, anayefanya biashara jijini Dar es Salaam.
James Habia wa Lindi, alisema Waziri Majaliwa amefanya kazi kubwa katika kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na kwamba endapo ataamua kugombea tena, itakuwa rahisi kushinda kwani anakubalika.
“Hata hao Ukawa wakiungana na kumleta Dr. Slaa, hawawezi kushinda kama CCM itamsimamisha Kassim Majaliwa,” alisema.
Majaliwa ni mmoja wa viongozi walioonesha uwezo mkubwa katika Baraza la Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete, ambaye mwishoni mwa mwaka huu atamaliza awamu ya nne ya uongozi wa nchi.
No comments:
Post a Comment