Pages

2015-02-27

KOMBE LA SHIRIKISHO: YANGA KAMILI GADO


YANGA iko tayari kwa lolote! Kama haukubali, subiri leo saa 2:30 usiku uone wakiwa kazini dhidi ya BDF XI.

Yanga inahitaji sare ya aina yoyote ili kusonga mbele, au ikiwezekana ushindi, pia poa tu!
Kikosi kizima cha Yanga kimemaliza mandalizi yake kwa ajili ya mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya timu hiyo ya Jeshi la Ulinzi Botswana, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Lobatse, kilomita 70 kutoka jijini hapa.

Wachezaji wa Yanga.

Wachezaji wa Yanga wameonekana kuwa na ari kubwa ya kutaka kufanya vizuri huku Kocha Hans van der Pluijm raia wa Uholanzi akisisitiza: “Yanga inachotaka ni kupita tu.”

Pluijm amesema Yanga itatumia kikosi hiki; Ally Mustapha ‘Barthez’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Kpah Sherman na Mrisho Ngassa.

“Tunachoshukuru baada ya mazoezi ya leo (jana), wachezaji wote wako vizuri, tunasubiri mechi na lengo ni moja, kusonga mbele,” alisema.

Kikosi cha Yanga, jana kilifanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Lobatse ulio katika mji mdogo wa Lobatse ambao utachezewa mchezo huo. Kabla ilifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Jeshi jijini hapa.

Yanga ilishinda kwa mabao 2-0 mjini Dar es Salaam katika mechi ya kwanza, Kocha Letang Kgengwenyane wa BDF XI, amesema hii ni zamu yao.

“Walishinda nyumbani kwao, walistahili. Sisi pia tunapaswa kushinda hapa nyumbani na tutapambana vilivyo kwa kuwa Yanga wana kikosi kizuri,” alisema Kgengwenyane ambaye amechukua nafasi hiyo baada ya aliyekuwa kocha mkuu kutimuliwa mwezi uliopita.

Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Yanga, Jerry Muro ameliambia Championi Ijumaa jijini hapa kuwa kila kitu kipo katika hali nzuri.

“Msafara utaondoka hapa Gaborone saa 8:30 mchana kwenda Lobatse, tutaongozana na msafara wa Watanzania wengine wanaoishi eneo hili ambao wametuunga sana mkono, tunawashukuru,” alisema Muro.

“Hadi sasa, kila kitu kinakwenda vizuri, maandalizi yako safi na mwalimu ana uwezo wa kuchagua nani amtumie kati ya wachezaji 20 walio hapa.”

No comments:

Post a Comment