Pages

2015-03-11

KUBWA KULIKO WAPANDA MAZAO JUU YA KABURI LA MWANAMUZIKI



Baadhi ya wananchi wa eneo la Msamvu mjini hapa wanadaiwa kuvamia makaburi na kupanda mazao juu yake likiwemo la aliyekuwa mwanamuziki maarufu wa dansi Afrika Mashariki, Salum Abdallah Husein Yazidu ‘Say’ aliyekuwa akimiliki Bendi ya Cuban Marimba.

Tukio hilo la aina yake lilijiri wiki iliyopita ambapo watu ambao majina yao hayakupatikana walionekana wakilima na kupanda mazao kama mahindi na mbogamboga, jambo lililosababisha kaburi hilo la mwanamuziki huyo na mengine kuporomoka.

Mwanahabari wetu alifika kwenye makaburi hayo ya Msamvu yaliyopo jirani na Shule ya Msingi Msamvu B na kushuhudia wazee wawili na mjukuu wao wakipanda mahindi juu ya makaburi hayo.
Walipohojiwa na gazeti hili, watu hao waligoma kuzungumza.

“Hebu fikiria, umempumzisha ndugu yako mahali hapa halafu unakuta watu wamebomoa na kulima mazao, ukweli siyo poa,” alisema mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo.

Baada ya kuondoka eneo hilo, mwanahabari wetu alipeleka ‘ubuyu’ kwenye familia ya mwanamuziki huyo maeneo ya Nunge jirani na Hospitali ya mkoa wa Morogoro ambao walikerwa na tukio hilo wakiahidi kuchukua hatua.

Akizungumzia tukio hilo, Afisa Habari wa Manispaa ya Morogoro, Lilian Hennerico alikuwa na haya ya kusema: “Wanadamu wamekuwa na mioyo ya ajabu sana. Hilo ni kosa kisheria kwa sababu maeneo ya makaburi yametengwa maalum kwa ajili ya kuzika wenzetu.

Makaburi ya Msamvu yamejaa hivyo waache mara moja kabla sheria haijachukua mkondo wake.”
Mwanamuziki huyo aliyezaliwa mwaka 1928 alifariki dunia mwaka 1965.

No comments:

Post a Comment