
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Harrison Mwakyembe, amesema kuhamishwa kwake katika Wizara hiyo akitokea Wizara ya Uchukuzi, si kwa sababu ya kuepushwa na kashfa ya ununuzi wa mabehewa feki.
Alisema uamuzi wa kuhamishwa Wizara umefanywa na Rais Jakaya Kikwete kwa sababu tofauti na hizo kama zilivyoandikwa katika gazeti moja linalotoka kila siku .
Dkt. Mwakyembe aliyasema hayo siku moja baada ya gazeti hilo kuandika habari iliyodai uhamisho uliofanywa na Rais Kikwete kwa Waziri huyo ni sehemu ya kumwepusha na kashfa hiyo.
"Kama Rais Kikwete aliona nina dosari, hakuwa na sababu ya kuniteua ili niweze kumsaidia katika Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kipindi hiki ambacho nchi yetu imepata fursa ya kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya.
"Hivi karibuni, Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda alifanya ziara mkoani Mbeya, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kyela, alitoa ufafanuzi mzuri juu ya uamuzi uliochukuliwa na Rais Kikwete kunihamisha Wizara," alisema Dkt. Mwakyembe.
Alisema hana haya ya kurudia ufafanuzi wa Bw. Pinda kwa sababu baadhi ya vyombo vya habari wameyaripoti na kuwataka Watanzania waamke kwani hakuna dosari yoyote ya yeye kuhamishiwa Wizara hiyo.
"Kupelekwa kwangu Afrika Mashariki ambako nilianzia ubunge ni mkakati mzuri wenye tija na nia njema kwa nchi, naomba ifahamike kuwa, sehemu kubwa ya nguvu ya fedha za washiriki wa maendeleo inapitia katika Jumuiya za Kanda.
"Kanda hizo ni pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo hivi sasa Rais Kikwete ndiye Mwenyekiti na mimi ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri," alisema.
Dkt. Mwakyembe aliongeza kuwa, habari iliyoandikwa ikihusisha uhamisho wake na kashfa ya ununuzi wa mabehewa feki ni ya uzushi na porojo za kisiasa hasa kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.
Alisema habari hiyo imemhusisha katika mchakato wa zabuni wakati yeye hana mamlaka nao kikanuni na kisheria ambapo baada ya kupokea malalamiko kuhusu mabehewa yaliyonunuliwa na Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), kutokuwa na viwango vinavyokubalika, alichukua hatua za awali kwa kuunda tume ya uchunguzi.
Aliongeza kuwa, baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi wa tume, alichukua uamuzi wa kuiagiza Bodi ya Wakurugenzi wa TRL kuivunja Bodi ya Zabuni na baada ya kuvunjwa.
"Niliiagiza Bodi ya Wakurugenzi wa TRL iwasimamishe kazi Maofisa Waandamizi wote waliohusika katika mchakato wa manunuzi ya mabehewa hayo ili kupisha uchunguzi uliokuwa ukiendelea kufanywa na tume," alisema.
Dkt. Mwakyembe alisema, pia aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), ifanye uchunguzi wa kina kuhusu mkasa huo kazi ambayo anaamini inaendelea kufanyika hadi sasa.
Alisema kwa msingi huo, habari inayomhusisha na kashfa ya mabehewa hayo imemshtua na kumshangaza.
Dkt. Mwakyembe alisema, pia aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), ifanye uchunguzi wa kina kuhusu mkasa huo kazi ambayo anaamini inaendelea kufanyika hadi sasa.
Alisema kwa msingi huo, habari inayomhusisha na kashfa ya mabehewa hayo imemshtua na kumshangaza.
No comments:
Post a Comment