Dar es Salaam. Siku mbili baada ya kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K Nyerere akiwa na vitu vinavyodhaniwa ni dawa za kulevya, Mwanahiphop Rashid Makwiro maarufu Chid Benz, anatarajiwa kufikishwa mahakamani.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania, Godfrey Nzowa aliliambia Mwananchi jana kuwa, mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika.
“Dawa tulizomkuta nazo tumezichunguza na kugundua kwamba ni Heroin kete 14, tumemhoji na anachokisema yeye ni kwamba zilikuwa kwa ajili ya matumizi yake. Upelelezi unaendelea kufanyika kabla hajapandishwa mahakamani,” alisema Kamanda Nzowa.
Akizungumza na gazeti hili jana Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege ACP Hamis Selemani, alisema hatma ya msanii huyo itajulikana kesho Jumatatu.
Hata hivyo Kamishna huyo alisema mabadiliko yanaweza kutokea muda wowote baada ya Jumatatu, lakini mtuhumiwa huyu amekiri kwamba dawa hizo zilikuwa kwa ajili ya kutumia yeye mwenyewe.
“Tumemhoji mtuhumiwa kwa muda mrefu na hatimaye amekiri kuwa dawa hizo hazikuwa kwa ajili ya kuuza, bali alikuwa azitumie akiwa jijini Mbeya ambako alikuwa anaelekea kwa ajili ya tamasha lililofanyika Jumamosi,” alisema ACP Selemani.
Chid Benz alikamatwa Ijumaa alasiri akijaribu kuvuka na dawa hizo akielekea Mbeya. Msanii huyo alikuwa katika hatua za ukaguzi kwa ajili ya kupanda ndege ya Fastjet kuelekea Mbeya akiwa na msanii mwenzake Nirdin Bilal maarufu ‘Sheta’.
Msanii huyo alikamatwa akiwa na kete 14 za dawa za kulevya aina ya Heroin pamoja na misokoto miwili ya bangi, ambayo alikuwa ameiweka katika mfuko wa shati alilokuwa amevaa. Pia alikutwa na kigae kidogo cha chungu pamoja na kijiko, vitu vya maandalizi ya kutumia dawa hizo na hivi vyote vilikutwa katika begi lake.
Julai mwaka jana wasanii wawili Melisa Edward na mwenzake Agnes Gerald ‘Masogange’ walikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Oriver Tambo nchini Afrika Kusini, wakiwa na dawa za kulevya aina ya Crystal Methamphetamine takribani kilo 150, zilizokuwa na thamani ya Sh. 6.8 bilioni.
Source: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment