2015-01-16

Ni daima:Hatuna kiongozi wa mfano’


  Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Alisema baadhi ya viongozi hao mara kadhaa wamekuwa wakipinga rushwa lakini kwa nyakati tofauti, hufanya vitendo wanavyokemea na kwamba njia pekee itakayowabadilisha na kurejesha maadili yaliyopotea ni kuwa wazi kwa kila jambo wanalofanya.

Dar es Salaam. Profesa Humphrey Moshi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema hivi sasa hakuna kiongozi anayefaa kutazamwa kama wa mfano hapa nchini kutokana na kushindwa kutekeleza mambo wanayoyasema.

Alisema baadhi ya viongozi hao mara kadhaa wamekuwa wakipinga rushwa lakini kwa nyakati tofauti, hufanya vitendo wanavyokemea na kwamba njia pekee itakayowabadilisha na kurejesha maadili yaliyopotea ni kuwa wazi kwa kila jambo wanalofanya.

Alitoa kauli hiyo chuoni hapo jana wakati akichangia matokeo ya utafiti kuhusu ‘upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ushindani wa kisiasa’ uliowasilishwa na Profesa Mohabe Nyirabu wa chuo hicho. 


Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo, Profesa Nyirabu alisema kumekuwapo na ongezeko kubwa la matumizi ya fedha kwenye vyama vya siasa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.

Alisema kuwa baadhi ya vyama vya siasa vinaonekana kutumia fedha nyingi kuliko mapato vinayopata na kwamba kuna haja ya vyanzo vya mapato hayo kuwekwa bayana.

Alisema kama matumizi ya fedha nyingi na utoaji wa rushwa umekithiri katika jamii, sera zinazosimamia masuala hayo hazina budi kuboreshwa.

Mhadhiri Mwandamizi kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Uongozi wa Umma UDSM, Dk Lupa Ramadhani akiwasilisha matokeo ya utafiti kuhusu “hali ya ustahimilivu wa kidini”, alisema viashiria vya kushuka kwa ustahimilivu huo katika jamii vimeongezeka katika miaka ya karibuni.

Alisema sakata la kuchinja ng’ombe lililotokea Geita mwaka 2005 lilipaswa kuchukuliwa na Serikali kama somo la kudhibiti uchochezi wa migogoro ya kidini, lakini akasema kwa bahati mbaya uongozi haukuchukua hatua za kutosha kumaliza jambo hilo lililosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila.

“Hivi sasa hatuoni machafuko yakiendelea lakini baadhi ya watu hawanunui tena nyama katika baadhi ya mabucha,” alisema. Alisema matukio ya kumwagiwa tindikali viongozi wa dini Arusha na Zanzibar yameacha ‘kovu’ linaloendelea kuisumbua jamii.

Hata hivyo, Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Rwekaza Mukandala alisema Serikali imefanya kazi kubwa katika kukabiliana na changamoto zinazohusu masuala ya kidini, ingawa baadhi ya watu hawazioni. 


“Njia ya kutatua masuala haya kwanza ni kueleza uelewa na kusema nini kinachofanyika kuna masuala yanaonekana ni ya kidini lakini ndani yake ni ya kiuchumi. Jamaa wana mambo yao wanataka kuyaendeleza kwa kutumia mwamvuli wa dini,” alisema Profesa Mukandala.

Profesa wa UDSM, Palamagamba Kabudi alisema hakuna dini hata moja inayozungumza kuhusu chuki dhidi ya nyingine, ila wapo baadhi ya viongozi waliojificha ndani ya taasisi hizo kutekeleza mambo yao. 

Mwananchi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...