Vitendo vya kikatili na unyanyasaji wa Wanawake na watoto vinaendelea kushika kasi licha ya Serikali na mashirika mbalimbali ya haki za Binadamu kupiga vita vitendo hivyo kwa nguvu .
Hali hiyo imejitokeza katika kijiji cha Kasaka, Kata ya Nyaruyoba Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma baada ya Baba mzazi aliyefahamika kwa jina la Sindotuma Nyamubi, kumchoma moto na kumuunguza vibaya sehemu za mdomoni wake, mtoto wake wa miaka saba akimtuhumu kudokoa maharage yaliyotakiwa kutumika kama mboga kwa ajili ya kulia chakula.
Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Bwa Felix Cosmas amesema kuwa mtoto huyo alibainika kuwa amefanyiwa kitendo hicho baada ya majirani kutomuoana akicheza na wenzake kwa muda wa siku tatu kama ilivyokuwa imezoeleka, ndipo walipogundua alikuwa amefichwa ndani ya nyumba na kugundua tatizo hilo na kutoa taarifa hatua iliyofanikisha mzazi huyo kukamatwa na kufikishwa Polisi.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Kibondo,Bi Sofia Gwamagobe amesema kuwa ni vizuri wazazi na walezi kutambua na kujali hali za watoto na sambamba na jamii pia kuendelea kufichua na kutoa taarifa katika vyombo husika ili kuweza kuokoa maisha ya watu wanaofanyiwa mambo kama hayo kama wamejeruhika kuwapatia matibabu kabla hawajapata madhara makubwa
Mkuu wa Jeshi la Polisi wilayani Kibondo, amekiri kuwepo kwa tukio hilo, na kumtaja aliyejeruhiwa vibaya kuwa ni Shukuru Sindotuma na amesema baada ya mtuhumiwa huyo kufikishwa kituoni hapo, amekubali kuwa alimchoma moto mtoto wake kwa kosa la kula maharage bila ruhusa yake
Mtoto huyo Shukuru Sindotuma alikuwa anaishi na baba yake ,mdogo wake mmoja huku Wazazi wao wakiwa wametengana.
0 comments:
Post a Comment