
Tunaendelea na sehemu ya pili ya makala haya ambayo ndiyo hitimisho la mada hii:
Kwa kuwa wazazi ndiyo wa kwanza kuliona jua, wameona vitu vingi, wamejifunza mengi, wanapaswa kukupa ushauri sahihi katika kila hatua ambayo unataka kuipiga.
Wakikufundisha juu ya tofauti za kiimani, utakuwa makini katika kuchagua mchumba ambaye utaanzisha naye uhusiano. Ni bora kutatua tatizo likiwa dogo kuliko kulilea hadi pale linapokuwa kubwa.
WASHIRIKISHE MAPEMA
Wanandoa watarajiwa wanapaswa kuwashirikisha wazazi wao mapema kuhusu uchumba wao, mtoto wa kike anaweza kumshirikisha mama yake vilevile wa kiume anaweza kumshirikisha baba yake mapema.
Si vibaya mtoto wa kiume akimwambia baba yake kwamba amepata mchumba, si dhambi mzazi kumshauri mwanaye juu ya mtu sahihi ambaye anastahili kuolewa na mwanaye.
Hapo ndipo utakapopata suluhu mapema kabla hata hujaamua kuanzisha safari na huyo umpendaye.
Dunia ya sasa imebadilika. Jifunze kutoka kwa wazazi ili kuwa na uelewa mpana wa kung’amua mambo. Wapo watu ambao malezi yao yalikosa mafunzo na badala yake wanakuwa wahuni wenye tabia mbalimbali ambazo kimsingi haziwezi kufanana na mtu ambaye amekulia katika malezi bora.
Ni muhimu kumjua mwenzako tabia kabla hujaingia kwenye uhusiano. Ni bora kumpima mapema pale mnapoanzisha safari kabla mambo hayajafikia katika hatua ya mbele zaidi. Fanya uamuzi sahihi kabla penzi halijaweka mizizi, likishakuwa na mizizi, ni vigumu sana kufanya maamuzi.
Kabla ya kufikia kwenye migogoro ya aina hiyo, wazazi wanatakiwa kukushauri vyema kulingana na miiko ya mila na desturi ambazo wao wameishi. Wanapaswa wakulee katika maadili ambayo wao wanayaishi.
Wazazi wasipokupa maadili mazuri mapema kulingana na wao wanavyoishi, ni rahisi kuja kupata matatizo mbele ya safari. Msingi mzuri watakaoujenga kwako ndiyo matokeo mazuri ya nyumba ambayo unaijenga.
Wakupe ushauri mzuri juu ya mke au mume mwema. Umtambue kabla hujakutana naye, wakufundishe ili uwe na uwezo wa kupembua mambo kwa busara ili ikiwezekana utatue tatizo kabla ya kufikia kwenye migogoro.
YAKISHATOKEA
Endapo mpo katika hatua za kuelekea kwenye ndoa, kukatokea mvutano wa hali yoyote ile, busara za wazazi zinapaswa kutumika lakini busara za wanandoa wenyewe ndizo zinahitajika.
NAFASI YA WAHUSIKA
Wanandoa watarajiwa nao wana nafasi kubwa katika kufanya uamuzi juu ya mvutano wowote ambao umetokea na kulifanya penzi lao likose muelekeo.
Wanapaswa wenyewe kuzungumza na kukubaliana jambo la kufanya kwa kutumia busara kisha kulifikisha kwa wazazi na kuomba baraka zao. Washirikisheni wazazi kwamba misingi ya uhusiano wenu ulikuwa ni nini, mipango yenu hivyo wawape ridhaa ya kufanikisha jambo hilo katika namna ambayo vile ambavyo mnaona inafaa.
Mkitumia busara kuliwasilisha kwa kuwapa mikakati na muda ambao nyinyi mmekaa na kupanga maisha yenu, hakika hawawezi kukataa. Kama binadamu ni rahisi kubadilisha misimamo na mitazamo na kuwaruhusu muingie kwenye ndoa ambayo itakuwa ya furaha na amani!
GPL
0 comments:
Post a Comment