2015-02-06

ZA CHEMBE LAZIMA UKAE: ASHA BARAKA, CHOKI HIVI MNAJUA MNA DENI KUBWA ........waambiwa lazima walipe

Asha na Choki wakishow love ndani ya studio za Global TV Online baada ya upatanisho.

NINAWAFAHAMU vizuri sana hawa watu wawili, dada Asha Baraka ‘Iron Lady’ na mdogo wake, Ally Choki mwenye majina mengi ya kisanii, lakini mimi nikilipenda zaidi la Mzee wa Kizigo, kwa vile kwangu lina kumbukumbu ya mambo mengi. 




Hakuna utata kuwa Asha Baraka ni mmoja wa wanawake wapambanaji katika zama za sasa ambao taifa linaweza kujivunia, kwani mikononi mwake wamepitia watu wengi sana kisanaa.

Kama nitajaribu kukamata kalamu na kuandika mambo nisiyoyapenda au ambayo nimewahi kukwazwa na huyu dada, basi ninaweza kujaza kurasa nyingi za gazeti hili, lakini kwa kuwa hilo halijawahi kuwa lengo langu, itoshe tu kumtaja Asha Baraka kama mwanamke aliyejitoa muhanga kuwa mmoja wa watu ambao historia ya muziki wa dansi haiwezi kuwasahau, vyovyote iwavyo.

Kuanzia Msondo Ngoma, Sikinde, Vijana Jazz na bendi nyingine za wakati ule, hadi FM Academia, Mashujaa Band, Malaika, Extra Bongo na nyingine za zama hizi, zote zina damu yake.

Muulize leo mzee Said Mabela wa Msondo kuhusu mchango wa Asha Baraka katika muziki, majibu yake hayatatofautiana sana na atakachokuambia Dogo Rama (ambaye kiumri anaweza kuwa mwanaye) anayepiga mzigo African Stars ‘Twanga Pepeta’. Kifupi, huyu dada hana roho mbaya.

Lakini hata wasanii wa muziki wa kizazi kipya na filamu, wanajua huyu ni nani katika sanaa, kwani amewahi kuwapa shavu vijana walioibuliwa na taasisi nyingine kama Bongo Stars Search au THT na ikumbukwe pia wakati mmoja enzi za uhai wake, alimsafirisha marehemu Steven Kanumba hadi Uingereza ambako alicheza filamu iliyojipatia mashabiki wengi, iliyoitwa Lovely Gamble.

Kwa Choki, naye mchango wake katika sanaa siyo haba na huenda ndiye mwanamuziki pekee wa dansi la kisasa mwenye mafanikio zaidi. Wenzake, aliokuwa akigombea nao ufalme, Ramadhan

Masanja ‘Banza Stone’ na Muumin Mwinjuma ‘Kocha wa Dunia’ ni kama wamekubali yaishe.
Choki anaupenda muziki, anauchukulia kama kazi. Anauheshimu na anajua thamani yake. Watu wanaomuunga mkono wanafahamu msimamo wake unaoshikiliwa zaidi na uwezo wake.

Anajua tabu alizopata katika muziki, ndiyo maana, kijana huyu wa Kibaha, hana roho mbaya kwa wenzake.

Nimewahi kuwa karibu na Choki, najua jinsi gani kina Banza na Msafiri Diouf wanavyomsema, lakini najua jinsi anavyowasaidia bila kukumbuka yaliyotokea nyuma.

Pamoja na uzuri wote wa hawa watu, kama binadamu, wana upungufu ambao mimi na wewe tunao. Wanasamehe, lakini hawasahau. Nalisema hili kwa sababu wote nimewahi kufanya nao kazi.

Wiki iliyopita, Global Publishers iliwakutanisha na kuwaomba kumaliza tofauti zao. Katika hali ya kiungwana wa hali ya juu kabisa, wawili hawa waliamua kuweka pembeni tofauti zao na kuanza maisha mapya. Nawapongeza sana.

Katika maisha yao ya kazi, wawili hawa wamewahi kugombana mara kadhaa kiasi cha kunipa wakati mgumu mimi kutekeleza majukumu yangu. Ukienda kwa Asha anakuambia wewe mtu wa Choki na ukija huku vilevile. Na katika kipindi hicho, wamegombana, kununiana na kurejesha uswahiba si chini ya mara moja. 


Ingawa ningependa hii iwe mara ya mwisho kwao kugombana na kurudisha uhusiano, lakini uzoefu wangu unaniambia hili litakuwa gumu kidogo. Ndiyo maana ninawaambia kuwa wana deni kubwa kwa wadau wao.


Asha Baraka mtu wa kinyongo, Choki mtu wa potelea mbali.
Kama kila mmoja wao atabaki na msimamo wake, muziki wa dansi hauwezi kufika mbali kwa sababu wawili hawa ni vichwa vinavyotegemewa sana ili kuufanya uendelee! 
GPL

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...