

Ukitaka kujua hali yangu, mimi niko poa na ninaendelea na majukumu yangu ya kujenga taifa kama kawaida na barua hii ni sehemu ya majukumu yangu ya kazi hivyo lazima nikuandikie tu, sina jinsi.
Dhumuni la barua hii kwanza kabisa ni kutaka kukukumbusha kidogo umuhimu wako katika jamii. Sitaki kuamini kwamba hujui umuhimu wako lakini kukumbushana ni muhimu, binadamu tumeumbwa kusahau.
Chid wewe ni mwakilishi mzuri sana wa Muziki wa Hip Hop. Tangu kipindi kile ulichosumbua na wimbo wako wa Dar es Salam Stand Up na nyingine kibao.Ulikuwa hukosei, ulikuwa unaachia jiwe baada ya jiwe na kila mtu alikuwa anakubali uwezo wako.
Kudhihirisha wewe ni mkali, nakumbuka ulikuwa ni lulu katika suala zima la kolabo. Wasanii walikuwa wakipanga msururu kukusaka, waliamini ukiingiza sauti yako katika nyimbo zao basi nazo zitakuwa tamu kama mcharo.
Hilo halikuwa na kificho, ulifanya kolabo nyingi sana. Nyimbo kama Neila ya Tunda Man, Hao na nyingine kibao zilinoga sana pale ulipoingiza sauti yako yenye mamlaka ambayo ulijua kuipangilia na kuendana na biti, wewe ni mkali aisee!
Pamoja na uzuri huo, juzikati hapa liliingia suala la wewe kunaswa na madawa ya kulevya. Binafsi sikushtuka sababu dalili za wewe kutumia nilishaziona kabla.Niliona dalili kutokana na matendo yako, yalikuwa hayafanani na uwezo wako mkubwa wa kutunga mashairi yenye uzito. Matukio kama yale ya kumdunda msanii mwenzako, Rehema Chalamila ‘Ray C’, nilijua kabisa si wewe.
Lilipokuja kutokea lile la kukamatwa na madawa pale Air Port, nilisikitika sana kama shabiki wako. Suala la wewe kuanza kuingizwa kwenye mikono ya sheria ni kuzidi kudidimiza kipaji chako na muziki wako kwa jumla.
Nilifuatilia kwa makini kesi yako hadi pale ulipotakiwa kulipa faini nikasema ni jambo la heri lakini unapaswa sasa kubadilika kweli na kutokubali kurudi nyuma. Uliwahi kukiri kuwa unatumia madawa, ukaahidi kuacha lakini ukarudia.
Nikushauri, mimi pamoja na mashabiki wengi Bongo na nje tunakupenda na tunahitaji kuendelea kusikia ‘madini’ yako.Ngoma yako ya Kimbiza ambayo haina muda mrefu sana tangu uiachie inatosha kuonesha kwamba uwezo unao, tupe raha kama ile ambayo ulikuwa unatupa.
Achana kabisa na madawa ya kulevya, sitegemei kukuona tena unakamatwa au unahusishwa katika suala hilo kwa namna yoyote.Ni matumaini yangu utabadilika kweli, kwa leo ni hayo, kila la kheri!
0 comments:
Post a Comment