2015-03-23

MMESHINDWA KUPATA WATOTO? SOMA HAPA



Ni matumaini yangu kwamba mpenzi msomaji wa safu hii uko poa na unaendelea na majukumu yako ya kila siku. Wiki iliyopita tulihitimisha mada ya namna ya kuishi na mwenzi wako akiwa mjamzito.
Hata hivyo, baadhi ya wasomaji wangu waliniomba pia tujadiliane kuhusu namna ya kuishi katika uhusiano wa kimapenzi ambao umeshindwa kuleta watoto. Kwa kuwa nakujali msomaji wangu, leo nimeamua kuiweka mezani mada hii.

Nakukaribisha kwa moyo mkunjufu tujadiliane kuhusu mada hii kama inavyojieleza hapo juu.

MATARAJIO YA WENGI

Watu wengi, wanaume kwa wanawake, wanapoanzisha uhusiano wa kimapenzi na watu wanaowapenda, huwa na matarajio makubwa ya kuanzisha nao maisha mapya, kujenga familia na kuzaa watoto.

Inapotokea matarajio hayo yakaenda kinyume, hata kama watu walikuwa wakipendana kiasi gani na kutimiziana mahitaji yote muhimu, ufa huanza kujitokeza kwenye uhusiano wao wa kimapenzi na kama hakuna anayejua namna ya kuishi na mwenzi wake katika mazingira magumu kama haya, uwezekano mkubwa ni kwamba uhusiano utavunjika, hata kama tayari wawili hao walishaoana kihalali.

Hata kama hali hii haijakutokea wewe, bila shaka tayari umeshawahi kusikia au kuwashuhudia wanandoa au watu wanaopendana sana lakini wanashindwa kupata mtoto. Hebu jaribu kuvuta picha, kama ndiyo ungekuwa wewe ungefanya nini?

WANAWAKE NDIYO HUBEBESHWA LAWAMA

Mila na desturi za watu weusi, hasa Watanzania, huwa zinawakandamiza sana wanawake linapotokea tatizo la wawili waliopo kwenye uhusiano wa kimapenzi kushindwa kupata mtoto.

Mazoea huwafanya watu wengi kuamini kwamba mwanamke ndiye pekee anayeweza kuwa na tatizo la kushindwa kubeba ujauzito. Matokeo yake, wanawake wengi hunyanyasika sana, wakishutumiwa kwamba wao ndiyo wenye matatizo. Ndugu wa upande wa mume au wakati mwingine mume mwenyewe ndiyo huwa mstari wa mbele kutoa tuhuma hizi ambazo mwisho husababisha uhusiano wa wawili wanaopendana kuvunjika.



HATA WANAUME WANAWEZA KUWA NA TATIZO

Jambo ambalo watu wengi hawalijui ni kwamba inapotokea wanandoa au watu wawili wanaopendana wakashindwa kupata mtoto, uwezekano wa kuwa tatizo lipo kwa mwanamke au kwa mwanaume huwa ni asilimia hamsini kwa hamsini.

Tafsiri yake ni kwamba yawezekana kabisa mwanamke akawa hana tatizo isipokuwa mwanaume ndiyo akawa na tatizo, jambo ambalo watu wengi huwa hawaliamini.

MFANO HALISI

Msomaji wangu, mama Habiba wa Kariakoo, alinitumia ujumbe ufuatao:

“Mimi na mume wangu tulioana miaka sita iliyopita kwa ndoa halali ya Kiislamu.

Siku za mwanzo za uhusiano wetu, tulipendana sana kwa kweli lakini tatizo likaanza miaka miwili tangu tufunge ndoa. Hatukubahatika kupata mtoto na licha ya kujitahidi kuhangaika huku na kule kutafuta tiba za asili lakini ilikuwa sawa na kazi bure.

“Baadaye ndugu wa mume wangu walianza kunishutumu kwamba mimi najaza tu choo na kumfuja ndugu yao wakati sikuwa na uwezo wa kuzaa. Walimjaza maneno mume wangu naye akaanza kuwaamini. Miaka miwili baadaye, ndoa yetu ikiwa imeshafikisha miaka minne, tulitengana.

“Miezi kadhaa baadaye nilikutana na mwanaume mwingine ambaye alitokea kunipenda. Nilisita sana kuanzisha naye uhusiano nikiwa naamini yatanitokea kama yaliyotokea kwa mume wangu lakini alinitoa wasiwasi.

Cha ajabu, nilipoanzisha uhusiano naye, miezi kadhaa baadaye nilibainika kuwa ni mjamzito, ndiyo nikamzaa mwanangu Habiba. Yeye mpaka leo hana mtoto hata wa kusingiziwa.

NINI CHA KUFANYA?

Kama wewe ni mmoja wa watu wanaokabiliwa na tatizo hilo, fuatilia mada hii hadi mwisho naamini utapata elimu ya nini unatakiwa kufanya.Ukiwa na maoni tumia namba hizo hapo juu.

Tukutane wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...