
Usemi wa Kiswahili kwamba bega haliwezi kushinda kichwa umetimia jana kwa kocha wa JKT Ruvu, Fred Felix Minziro aliposhindwa vishindo vya Yanga na timu yake kufungwa mabao 3-1.
Kwenye mchezo huo wa kiporo wa Ligi Kuu, mshambuliaji Simon Msuva alifunga mabao mawili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam yaliyomfanyam kumpiku Didier kavumbagu wa Azam mwenye mabao kumi.
Kavumbagu alikuwa akiongoza katika orodha ya ufungaji kwa muda mrefu.
Naye Danny Mrwanda alifunga bao lake la kwanza tangu alipojiunga na Yanga akitokea Polisi Morogoro kwenye dirisha dogo la usajili wakati Samwel Kamuntu aliifunga JKT bao la kufutia machozi.
Ushindi huo umeifanya Yanga ijikite kileleni mwa ligi kwa pointi 40, ikifuatiwa na Azam (36) na Simba ni ya tatu ikiwa nazo 32.
Yanga ilianza mchezo kwa kasi na dakika ya kwanza Msuva alikosa bao baada ya shuti lake kutoka nje baada ya kuwatoka mabeki wa JKT Ruvu.
Naye Mrisho Ngassa alikosa bao, dakika ya 20, akiwa na kipa Benjamin Haule, baada ya kupiga shuti lilitoka nje.
Yanga ilitawala kiungo, kutegeneza nafasi nyingi kwa washambuliaji ambao waliiweka safu ya ulinzi wa JKT Ruvu kwenye wakati ngumu.
Kasi hiyo ilizaa matunda dakika ya 34, wakati kiungo wa JKT Ruvu, Jabir Aziz aliposhika mpira kwenye eneo la penalti na mwamuzi Isihaka Shirikisho kutoa adhabu ya penalti iliyofungwa na Msuva.
Mrwanda alifunga bao lake la kwanza akiwa Yanga dakika ya 42, baada ya kugongeana pasi na Ngassa na kupiga shuti lililomshinda kipa Haule na kujaa wavuni.
Baada ya bao hilo wachezaji wa Yanga walionekana kuridhika na matokeo hayo na kuwaacha JKT Ruvu kujipanga na kufanikiwa kupata bao dakika ya 45, lililofungwa na Kamuntu, akimalizia pasi ya Idd Mbaga na kufanya matokeo kuwa 2-1 hadi mapumziko.
Wakati timu zinakwenda mapumziko mabeki wa Yanga, Juma Abdul na nahodha Nadir Haroub walishikana mashati wakitaka kupigana wakilaumiana kwa uzembe uliosababisha bao la JKT Ruvu.
0 comments:
Post a Comment