2014-12-24

Wataweza;kwa matokeo haya wataendeleza harakati za kugombea Urais??


Matokeo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 yanaonyesha kuwa CCM imefanikiwa kupata ushindi wa jumla mitaa na vijiji 9,406, huku vyama vingine vya upinzani, vimegawana nafasi 3,211. 



Hata hivyo, kwa ushindi huo upinzani umeongeza viti 1,981 ikilinganishwa na uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopita, ambao kwa ujumla, ulipata nafasi 1,230 za wenyeviti wa mitaa na vijiji.


Kwa upande wake, CCM imepoteza nafasi 2,636 za uenyekiti wa vijiji na mitaa ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2009 ilipopata jumla ya viti 12,042. 



Uchaguzi wa mwaka huu, umefanyika kukiwa na nyongeza ya amikoa, wilaya, mitaa na vijiji katika baadhi ya maeneo nchini.


CCM imepata vijiji 7,290 kikifuatiwa na Chadema yenye vijiji 1,248. CUF imeshika nafasi ya tatu kwa kuwa na vijiji 946, ikifuatiwa na UDP yenye vinne na TLP na NLD vyenye viwili kila kimoja.


Katika nafasi za wenyeviti wa mtaa, CCM kimechukua jumla ya mitaa 2,116. Vyama vingine na nafasi zao kwenye mabano ni Chadema (753), CUF (235), ACT (9), NCCR - Mageuzi (8) wakati vyama vya TLP, UMD, UDP na NRA vimepata mtaa mmoja kila kimoja.


Ushindi huo unaotajwa kuwa ni mdogo ikilinganishwa na ule wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2009 unaonekana kuwa na maana kubwa kwa chama tawala CCM, hasa katika maeneo ambayo wanatokea wabunge wake ambao wanatajwa kutaka kuwania urais mwaka 2015.


Moja ya hoja za wagombea urais watakazotumia kujipigia debe au kuponda wapinzani waoni kwanza kukubalika kwenye majimbo yao ya ubunge, jambo ambalo pia ni ishara wamekipigania vipi chama kwenye maeneo yao kabla ya kuomba kupewa dhamana kubwa zaidi ya kuongoza nchi mwaka 2015


Wanaotajwa kuutaka urais ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye anatokea jimbo la Katavi, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (Monduli), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira (Bunda), Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (Mtama).


Wapo pia aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja (Sengerema), Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba (Bumbuli).


Wengine ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka (Muleba Kusini), Dk Emmaniel Nchimbi (Songea Mjini), Dk Hamisi Kigwangalla (Nzega), Mwigulu Nchemba (Iramba Magharibi), Profesa Mark Mwandosya (Rungwe Mashariki) na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe (Kyela).

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...