
Waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa akionyesha kifimbo alichopewa na Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, kama ishara ya kutambua mchango wake katika sekta ya elimu kwa watoto wa kike wa jamii ya Kimasai mkoani Arusha jana. Kulia ni Mama Siti Mwinyi. Picha na Mussa Juma
Ni katika kusaidia watoto wa kike kwenda shule badala ya kuolewa
Monduli. Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi ameitaka jamii ya wafugaji wa Kimasai kuunga mkono jitihada za waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa na Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi kuikomboa kielimu jamii hiyo kwa kuhakikisha watoto wa kike wanakwenda shule badala ya kuolewa mapema.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 20 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Masai iliyopo wilayani Monduli jana, Mwinyi alisema inasikitisha wakati kuna watu wamejitolewa kuisaidia jamii hiyo, lakini bado kuna wazazi hawataki watoto wao wa kike wasome.
“Tusiwaachie Lowassa na Mengi jukumu la kusaidia watoto hawa peke yao, juhudi zao zinapaswa kuungwa mkono,” alisema Mwinyi.
Rais Mwinyi, ambaye ndiye aliyeweka jiwe la msingi la kuzindua shule hiyo Mei 27, mwaka 1995, aliipongeza Taasisi ya Operation Bootstrap Africa (OBA) kwa kusaidia shule hiyo hadi sasa imekuwa na mafanikio makubwa.
“Leo nimefurahi sana, nilikuja hapa shule ikiwa na darasa moja, leo kuna madarasa 12,” alisema na kuongeza: “Hakukuwa na maabara, leo nashuhudia maabara nne...mabweni hayakuwapo, sasa yako 12 na nyumba za walimu 15.
Pia, nimeelezwa kuwa, hadi sasa shule hii imetoa walimu 250, wanasheria tisa, daktari mmoja, mhandisi na mchungaji mmoja, hili ni jambo jema sana.”
Hata hivyo, aliushauri uongozi wa shule hiyo kuanzisha kozi za ufundi stadi ili wahitimu watakaokosa nafasi za elimu ya juu, wajiendeleze na ufundi wa aina mbalimbali.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Lowassa alimpongeza Mwinyi kwa kuwa mwanzilishi wa kwanza kusaidia ardhi ya ujenzi wa shule hiyo, pia kuchangia Sh46 milioni kwa chama cha kwanza cha walimu cha kuweka na kukopa wilayani Monduli.
Mwenyekiti wa IPP, Mengi alisema amekuwa akisaidia watoto wa jamii ya Kimasai katika shule hiyo, siyo kwa sababu na yeye alitoka katika jamii maskini ila kwa sababu anatambua mahitaji ya msingi ya elimu.
Askofu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Salomon Masangwa alimshukuru Mwinyi kwa kuwa mfano wa mafanikio katika shule hiyo.
Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment