
Arusha. Wajumbe wa Baraza la Biashara wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa vitendo ili kuchochea ukuaji wa shughuli za biashara na uwekezaji mkoani hapa.
Ushauri huo ulitolewa na mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa, Daudi Ntibenda katika kikao cha kawaida cha baraza kilichofanyika hivi karibuni.
“Tunahitaji yale yote tuliyoyajadili hapa yatekelezwe kwa vitendo ili kuvutia zaidi biashara na uwekezaji katika mkoa wetu,” alisema Ntibenda. Mabaraza ya biashara ya mikoa yanafanya kazi chini ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na kuundwa na wajumbe kutoka sekta za umma na binafsi.
Ntibenda alisema mkoa una fursa nyingi za biashara zinazopaswa kutumiwa vyema na wajumbe wa baraza kwa kuzitangaza kwa wawekezaji.
Aliwataka maofisa wa biashara wa wilaya kuwasaidia wenyeviti wa mabaraza ya biashara ya wilaya zao kuhakikisha shughuli hizo zinashamiri kwenye maeneo yao.
Alisema ili mabaraza hayo yafanye kazi vizuri, halmashauri zinatakiwa kutenga bajeti za uendeshaji wake kwa kuwa yanatambulika kisheria.
“Sekretarieti ya mkoa imejipanga kuhakikisha Baraza la Mkoa linafanya kazi kwa ufanisi na kuleta maendeleo,” alisema mkuu huyo wa mkoa.
Naye mkurugenzi wa Mazingira ya Biashara wa TNBC, Arthur Mtafya alisema baraza la mkoa linatakiwa kufanya vikao kwa mujibu wa uendeshaji wa baraza kwa nia ya kuchochea shughuli za biashara na uwekezaji.
“Vikao hivi vya baraza ni muhimu kwa sababu wajumbe wote hupata fursa ya kujadili kwa pamoja masuala ya biashara na uwekezaji,” alisema.
Alibainisha kuwa mikutano hiyo ya majadiliano na wawekezaji iwe inaandaliwa kwa kufuata utaratibu wa mabaraza, licha ya kuwapo kwa makongamano ya biashara ya kikanda na mapendekezo yake, mkoa pia unaweza kuibua fursa zake za kibiashara na kuziwekea mikakati.
0 comments:
Post a Comment