2015-02-20

Duuuuuuuuuu Aliyetemwa ukuu wa wilaya ageukia ubunge



Aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu.






Dar es Salaam. Siku moja baada ya uteuzi wake kutenguliwa na Rais Jakaya Kikwete, aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu amesema sasa anageukia ubunge katika Jimbo la Singida Magharibi.


Kingu alisema siku nyingi alikuwa na shauku ya kugombea ubunge katika jimbo hilo, kwamba kuondolewa katika wadhifa huo kutampa nafasi ya kujipanga na kuhakikisha anashinda jimbo hilo linaloongozwa na Mohamed Hamisi Missanga (CCM).


“Unajua kwa muda sasa akili yangu ilijikita zaidi katika ubunge ili niweze kuwasaidia wananchi kwa ukaribu zaidi. Wananchi wa Jimbo la Singida Magharibi wamekaa muda mrefu bila kupata mtu wa kutatua matatizo yanayowakabili,” alisema.


Alifafanua kuwa Februari 28, mwaka huu atafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika jimbo hilo, ataitumia siku hiyo kutangaza rasmi nia yake ya kugombea ubunge.


“Nitakachokifanya sasa ni kuwa karibu zaidi na wananchi na kuhakikisha matatizo yanayowakabili ninayajua kiundani ili niweze kuyatatua kwa urahisi,” alisema.


Aliongeza, “Namshukuru Rais Kikwete kwani aliniamini na kazi aliyonipa niliifanya kwa uaminifu na uzalendo wa hali ya juu, kufanikiwa kuleta mabadiliko katika sekta ya kilimo, afya, mifugo, uvuvi na maendeleo kwa vijana,” alisema Kingu (pichani).


“Rais ameamua nipumzike na ninamshukuru kwa uzalendo wake mkubwa naamini bado ana imani kubwa na mimi.”


Akitoa ushauri wa wakuu wapya wa wilaya alisema, “Wanatakiwa kuhakikisha wanamsaidia kazi Rais Kikwete na kutekeleza ilani.”


Wakati Kingu akieleza hayo, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Zelothe Stephen ambaye ameteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya ya Musoma.


Alisema: “Sina maneno mengi kwa sasa nitasema kauli tatu; Asante kwa pongezi yako, namshukuru Mwenyezi Mungu, namshukuru sana Rais Kikwete kwa kuniteuwa kushika wadhifa huu.”


Kwa upande wake Martha Umbulla aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, alipotafutwa na gazeti hili siku nzima ya jana alisema kuwa yupo katika kikao na kuahidi kuzungumzia uteuzi huo baada ya kumalizika kwa kikao, jambo ambalo hakulitekeleza.


Wilaya ya Kiteto ni moja kati ya wilaya zilizokithiri migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, iliyosababisha watu zaidi ya 10 kuuawa na wengine kujeruhiwa.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...