Yohana alitekwa nyumbani kwao saa mbili usiku, akiwa amebebwa na mama yake. Tukio la kutekwa mtoto huyo lilifanywa na watu wawili, ambao pia walimjeruhi mama huyo kwa kumkata mapanga kichwani.
Kamanda wa Polisi mkoani Geita, Joseph Konyo alisema juzi kuwa mwili wa mtoto huyo ulikutwa kwenye shamba la mahindi katika Kijiji cha Kimasa.
Alisema mwili huo uliokotwa juzi Februari 17, saa 12 jioni kwenye makazi yasiyo rasmi.
Ndugu wa marehemu, waliiambia gazeti hili kuwa Kamanda Konyo ameahidi kutoa ulinzi mkali wakati wa mazishi hayo kutokana na mazingira ya tukio lenyewe.
Katika hatua nyingine, hali ya mama wa mtoto mwenye ulemavu wa ngozi, ambaye alitekwa na kufariki dunia baada ya kukatwa viungo, imeelezwa kuanza kuimarika na kwamba kwa sasa ameanza kuzungumza polepole pamoja na kula.
Mama huyo, Esther Jonas (30), ambaye alifanyiwa upasuaji wa kichwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, hali yake imeanza kuimarika baada ya kuanza kupumua vizuri tofauti na alivyokuwa jana na kwamba bado madaktari wanaendelea kumpa matibabu.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Mkuu wa Kitengo cha Dharura BMC, Dk Derick David alisema hali ya mama huyo kwa sasa imeanza kuwa nzuri tofauti na jana.
“Ninachoweza kusema kwa leo (jana), hali ya mfiwa imeanza kuimarika na ameanza kupumua vizuri na kuzungumza polepole,” alisema Dk David.
0 comments:
Post a Comment