2015-02-11

Mbowe avunja uongozi Chadema Ukonga, Ilala je, wajua ni kwa nini? fuatlia chanzo hapa



“Tulichambua kwa kina na kuona huo upungufu, hatukuwafukuza viongozi wale, lakini viongozi walitakiwa kuwajibika kisiasa na walijiuzulu,” Freeman Mbowe.

Mwenyekiti huyo aliamua kuvunja uongozi wa majimbo hayo na sasa uchaguzi wa kuweka viongozi wapya utafanyika Februari 14

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ameuvunja uongozi wa chama hicho kwenye majimbo ya Ukonga na Ilala kutokana na kutoelewana kwa muda mrefu baina ya viongozi na kutofanya vizuri kwa chama hicho kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 mwaka jana. 


Habari ambazo Mwananchi imezipata na kuthibitishwa na Mbowe zinaeleza kuwa mwenyekiti huyo aliuvunja uongozi huo wiki mbili zilizopita baada ya kikao cha siri na viongozi wa majimbo hayo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Klabu ya Billicanas iliyopo katikati ya jiji.

Pamoja na CCM kuibuka na ushindi mkubwa kwenye uchaguzi huo wa ngazi ya mwanzo ya uongozi, Chadema iliongoza kwa upande wa upinzani ingawa haikuwa na matokeo mazuri kwenye majimbo hayo mawili.

Katika uchaguzi huo, CCM ilishinda kwa asilimia 79.4 katika nafasi ya uenyekiti wa mitaa, Chadema asilimia 15.1 na CUF asilimia 4.6. Vyama vingine kwa ujumla vilipata asilimia 0.9.

Matokeo ya uchaguzi wa wenyeviti wa vitongoji yanaonyesha kuwa CCM ilishinda kwa asilimia 79.3, Chadema asilimia 15.6, CUF asilimia 4.3 na vyama vingine vilipata asilimia 0.8. Katika uchaguzi wa nafasi za uenyeviti wa mitaa, CCM ilishinda kwa asilimia 66.5, Chadema asilimia 25.4, CUF asilimia 6.8 na vyama vingine vilipata kwa asilimia 1.3.

Matokeo ya Wajumbe wa Serikali za vijiji/mitaa yanaonyesha CCM ilipata asilimia 79.3, Chadema asilimia 15.7, CUF asilimia 4.3 na vyama vingine asilimia 0.7, wakati katika wajumbe wa viti maalum CCM ilipata asilimia 82.1, Chadema asilimia 13.7, CUF asilimia 3.5 na vyama vilivyobaki navyo vilipata asilimia 0.7.

Mbowe akerwa

Chanzo cha habari kinapasha kuwa ushindi wa CCM katika maeneo mengi na zaidi Jimbo la Ukonga ndiyo uliomkera zaidi Mbowe pamoja na misigano ndani ya chama.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, Mbowe alikiri kufanya kikao cha uongozi ambapo pamoja na mambo mengine waliangalia uwajibikaji, mafanikio na kushindwa kwa chama hicho katika uchaguzi huo wa serikali za mitaa. 

Alieleza kuwa, katika kikao hicho waligundua kasoro mbalimbali katika majimbo hayo ya Ukonga na Ilala na kuafikiana kuwa viongozi wao wawajibike kutokana na upungufu huo.

“Tulichambua kwa kina na kuona huo upungufu, hatukuwafukuza viongozi wale, lakini viongozi walitakiwa kuwajibika kisiasa na walijiuzulu,” alisema Mbowe.

Kwa maelezo ya Mbowe, sasa majimbo hayo yapo chini ya Ofisi ya Kanda Maalumu ya Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam, ambayo inasimamiwa na Mabere Marando hadi hapo uongozi wa kikatiba utakaporejeshwa.


Mwananchi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...