2015-02-10

Mtuhumiwa sakata la Escrow kizimbani leo


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo inatarajia kumsomea maelezo ya awali Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma anayekabiliwa na kesi ya kupokea Sh milioni 323.4 ambazo ni sehemu ya fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Mujunangoma anatarajiwa kupanda kizimbani na kusomewa maelezo ya awali mbele ya Hakimu Mkazi Emilius Mchauru kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Anakabiliwa na mashitaka ya kupokea Sh 323,400,000 kama tuzo baada ya kushughulikia masuala ya kampuni ya IPTL kama mfilisi, jambo ambalo linahusiana na kazi yake.

Katika mashitaka yake anadaiwa, Februari 5, 2014 katika jengo la Benki ya Mkombozi alipokea rushwa ya fedha hizo kupitia akaunti namba 00120102602001 kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya Kufua Umeme ya VIP Engineering and Marketing ambaye pia alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya IPTL, James Rugemalira.

Inadaiwa fedha hizo ni sehemu ya zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow. Mujunangoma yupo nje kwa dhamana baada ya kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani ya nusu ya fedha anazodaiwa kupokea, pamoja na wadhamini wawili watumishi wa umma waliosaini hati ya Sh milioni 10 kila mmoja.





0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...