2015-03-06

Albino waandamana wakienda kwa Rais Kikwete


 
Mwenyekiti wa Chama cha Albino Tanzania, Ernest Kimaya (kushoto) akizuiwa asiendelee kugombana na wanachama wake karibu na uzio wa Ikulu waliokuwa wakitaka wote waambatane kwenda kuonana na Rais Jakaya Kikwete kueleza matatizo yao jijini Dar es Salaam jana. Rais Kikwete alitoa mwaliko wa kukutana na viongozi wa chama hicho.

Pembeni ya barabara inayopakana na Ikulu, karibu na jengo la Wizara ya Elimu wakati wakielekea kumuona Rais Kikwete, wanachama hao walianza kumshambulia Kimaya wakidai kuwa si kiongozi halali, lakini aliokolewa na maofisa usalama waliokuwapo katika tukio hilo.

Dar es Salaam. Hali ya sintofahamu ilitokea jana baada ya wanachama wa Chama cha Albino Tanzania (Tas) kumshambulia kiongozi wao, Ernest Kimaya wakati wakiwa njiani kuelekea Ikulu ambako Rais Jakaya Kikwete aliwaita kwa mazungumzo.

Pembeni ya barabara inayopakana na Ikulu, karibu na jengo la Wizara ya Elimu wakati wakielekea kumuona Rais Kikwete, wanachama hao walianza kumshambulia Kimaya wakidai kuwa si kiongozi halali, lakini aliokolewa na maofisa usalama waliokuwapo katika tukio hilo. 

Wanachama hao walitaka kushinikiza na wao kumwona Rais Jakaya Kikwete badala ya viongozi 15 ambao ndiyo waliotakiwa wamwone Rais na kuzungumza naye. Saa moja baadaye, viongozi hao wa Tas waliingia Ikulu kuonana na Rais Kikwete.

Wanachama hao walikuwa wakimtaka Kimaya aachie wadhifa wake kwa kuwa si kiongozi.

Kimaya alizomewa muda wote na kumvuta nguo na baadhi ya wanachama hao ambao walimtuhumu kuwa anajinufaisha na vifo vya albino vinavyozidi kutokea nchini.

Hata hivyo, Kimaya alishindwa kujizuia na kutaka kupigana na baadhi watu waliokuwa wakimzonga na kumtukana. Maofisa usalama walimchukua na kumwondoa eneo la tukio ili vurugu zisiendelee.

Baadhi ya wanachama wa Tas walisema viongozi wao wamejikusanya wenyewe kwenda Ikulu bila kuwashirikisha na kuwa hawafanyi mikutano ya mara kwa mara zaidi ya kuwaita kwenye maandamano.

Mmoja wa albino hao, Nuru Iddi alisema hawana imani na viongozi wao kwa sababu muda wao wa kuwepo madarakani uliisha tangu mwaka jana.

Alisisitiza kuwa tangu wakati huo hawajafanya uchaguzi wowote na viongozi wametulia ili waendelee kujinufaisha. 


“Albino akiuawa kule Mwanza mimi ndiyo napata uchungu, siyo hawa viongozi... wao wanapokea michango mingi kutokana na vifo vya wenzetu lakini hawafanyi jambo lolote la maana kulinda maisha yetu,” alisema mwanachama huyo.

Iddi aliongeza kuwa wao ndiyo walitakiwa kuonana na Rais Kikwete ili wamueleze hali halisi na nini cha kufanya ili kulinda maisha yao.

Aliulaumu uongozi wa Tas kwa kutowashirikisha wao kama wanachama kutoa maoni ambayo yangewasilishwa kwa Rais.
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...