2015-03-06

Kambi ya Simba ni balaa!


                                 Kambi ya Simba .


SIMBA ipo kisiwani Unguja, Zanzibar, ikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga, ambayo itapigwa keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, lakini katika kambi hiyo kuna mambo mengi ambayo yanaonyesha kweli timu hiyo ya Msimbazi imepania kufanya kweli.

Championi Ijumaa ambalo limeweka kambi kisiwani hapa kwa siku kadhaa tangu Simba iwasili kisiwani hapa, limeshuhudia mambo mengi na linakupa ripoti kamili.

Nyumbani kwa tajiri
Kikosi cha Simba, chote kimeweka kambi kwenye nyumba ya tajiri mmoja ambaye anatajwa kufahamika kwa jina la Abdul Zacharia na siyo hotelini kama ambavyo imekuwa ikitokea siku za nyuma.


Simba ipo kwenye nyumba hiyo ya ghorofa ambayo ina hadhi ya kuitwa ya kifahari kutokana na jinsi ilivyo na mazingira yake yalivyo eneo la Chukwani, kisiwani hapa.

Ulinzi mkali
Katika kambi hiyo kuna ulinzi mkali ambapo siyo kila mtu anaruhusiwa kuingia au kusogelea karibu ya nyumba hiyo, gazeti hili lilishuhudia kukiwa na walinzi wanne ambao walikuwa na kazi ya kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri na hata wachezaji wenyewe hawaruhusiwi kutoka bila ruhusa maalum.

Gazeti hili lilifika katika kambi hiyo na kupata baadhi ya picha na kujionea matukio kadhaa ikiwemo wakati wachezaji wanaingia na walivyokuwa wakitoka.

Kocha Msaidizi wa Simba, Selemani Matola alishuhudiwa akiwasili kambini hapo akiwa katika gari binafsi lenye namba za usajili za Zanzibar ambapo alikuwa akiendesha mwenyewe na hata alivyofuatwa aligoma kuzungumza chochote kwa madai kuwa ndivyo utaratibu ulivyo kambini hapo.

Akizungumza na gazeti juu ya kambi hiyo, mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Abdul Mshagama alisema kuwa tajiri huyo amekuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo tangu iwasili kisiwani hapa na kudai kuwa hata mazingira ya maandalizi nayo yamekuwa mazuri na kuamini kuwa itawajenga wachezaji kisaikolojia kuelekea mchezo huo wa Yanga.

“Mbali na hapo tumekuwa tukiendelea vizuri na mazoezi lakini tumekuwa tukibadili viwanja vya mazoezi kutokana na mazingira ya kukwepa hujuma zozote zinazoweza kutokea,” alisema kiongozi huyo ambaye ni mwenyeji wa Zanzibar.


GPL

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...