2015-03-31

Tuwaandae kuwa wakakamavu wa mwili au akili?



Lugha inayotawala sasa kwa vijana wengi ni kukosa ajira, kukosa kazi. Na kubwa zaidi Serikali inalaumiwa kwa kuwanyima ajira vijana.


Vijana waliotoka JKT juzi juzi walidiriki kuandamana kuishinikiza Serikali iwaajiri. Maana wana haki ya ziada kuajiriwa na Serikali baada ya kupata mafunzo ya ukakamavu wa mwili jeshini. Pengine inawezekana ni kweli!


Wakati mtazamo wa vijana kulalamikia kukosa ajira ukizidi kukua na kushamiri kwa wengi. orodha ya ajira na nafasi za kazi zinazotangazwa kwenye mitandao ya kijamii, kwenye tovuti za ajira na magazetini ni nyingi.


Wageni na wakakamavu wa akili wanazichangamkia fursa hizo na wanaajiriwa na kuwaacha vijana wanaendelea kulalamika hawana kazi.


Nimewahi kusema huko nyuma kuwa pamoja na kwamba Tanzania yetu Mungu alitujalia rasilimali kama misitu, vipaji mbalimbali kwa watu, wanyama pori na ardhi kubwa na yenye rutuba, bado kuna Watanzania wanasimama kwa ujasiri na kutamka kuwa “hawana kazi”


Tunalalamika hatuna kazi na lazima Serikali ituajiri. Kwa mtazamo wangu ni kosa kubwa. Tunajichelewesha wenyewe kimaendeleo.


Madhara ya mtazamo huu ambao umejengeka kwa kasi nchini kwetu ni kwamba, vijana wengi hawajishughulishi kufikiri, kuthubutu wala kujituma, wanashinda vijiweni wakisubiri ajira za serikalini. Na wachache wanaoajiriwa hawawezi kazi na hawapendi kazi, wengi wanafukuzwa kazi kwa sababu ya uvivu na uzembe.


Vijana sasa wanatamani mafanikio kwa njia ya mkato, ndiyo maana wanajiunga na vikundi vibaya ili kupata utajiri wa muda mfupi.


Hawajitumi kufanyakazi wala kubuni fursa za kujiendeleza, wanatumiwa na wanasiasa kuivuruga nchi na kuwaingiza wenye pesa madarakani.


Nguvu kazi ya Taifa maana yake ni vijana walioandaliwa kuijenga nchi. Vijana wakakamavu wa kufikiri, kuchangamkia fursa, kubuni fursa na kufanya kazi kwa bidiii.


Vijana wenye uzalendo wa kujenga nchi yao. Vijana wanaojitambua wao ni kina nani wana wajibu gani kwa familia na Taifa lao. Vijana wanaofanya bidii kuzalisha na kuijenga nchi.


Wasiotumiwa na wanasiasa au watu fedhuli kubomoa umoja wa kitaifa na kuingiza wezi madarakani. Hawa ndio vijana wakakamavu.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...