2015-03-31

Watengeneza printa ya aina yake Afrika Mashariki



  Meneja wa Maabara ya Buni Hub Jacquline Dismas akieleza namna printa ya 3D inavyofanya kazi hivi karibuni.Picha na Nuzulack Dausen.
Na Nuzulack Dausen

Huenda isiwe inafahamika na Watanzania wengi, lakini mashine ya kwanza ya kuchapa vifaa vya maumbo mbalimbali, imeanza kutengenezwa nchini.

Kwa mara ya kwanza Afrika Mashariki na Kati, Printa inayochapa kitu katika pande tatu maarufu kwa kiingereza kama ‘3D Printer’, imetengenezwa jijini Dar es Salaam katika kituo cha kukuza ubunifu na ujasiriamali cha Buni Hub.


Printa hiyo, yenye uwezo wa kutengeneza vifaa mbalimbali vya plastiki kutokana na usanifu wake, ilitengenezwa na timu ya wataalamu wa elektroniki na teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) baada ya kupatiwa ujuzi na mtaalamu kutoka Uingereza, Mathew Rogge.


Kwa wengi waliozoea printa za kuchapa karatasi watashangazwa na uwezo mkubwa wa printa hiyo inavyoweza kuuchapa mchoro uliopo kwenye kompyuta hadi kuwa kifaa pasina kukosea.


Baada ya wiki tatu za kuitengeneza, printa hiyo imeshatengeneza vifaa kadhaa vya plastiki vinavyoweza kutumika kama vipuri kutengenezea mashine nyingine ya namna hiyo.


“Mashine hii tulioitengeneza kwa kutumia mabaki ya vifaa vya elektroniki, inaweza kutengeneza vitu unavyoweza kuvishika na kuvitumia katika kazi mbalimbali kama vikombe, midori, sampuli za nyumba, viatu na vinginevyo,” anasema Meneja wa maabara ya Buni Hub, Jacqueline Dismas.


“Tunajaribu kwa hali na mali kuhakikisha mazingira yetu ni safi kwa kupunguza taka ambazo zinaweza ama kutumika tena au kutengenezwa upya.”


Ili kupata vifaa vya kuundia mashine hiyo, anasema iliwahitaji kuzunguka kwenye vituo vya kukusanya taka za kielektroniki kama printa, kompyuta na televisheni vilivyopo jijini hapa.


Matumizi ya taka hizo, zinazosaidia kupatikana kwa mota, chanzo cha nishati ya umeme (power supply) na reli za kujengea printa, yanasaidia kupunguza tatizo la taka ngumu na kujenga tabia ya kutunza mazingira.


Tofauti na printa zinazochapa karatasi ambazo hutumia wino kuchapa, printa za 3D zinatumia malighafi za plastiki, chuma, udongo, na nyinginezo ziitwazo ‘filament’ kuzalisha bidhaa tofauti kutokana na mahitaji.


Kuingia kwa teknolojia ya uundaji printa za 3D hasa kwa kutumia taka za kielektroniki, kutapunguza gharama za ununuzi wa mashine hizo zilizoanza kupata umaarufu ulimwenguni kwa kurahisisha kazi lukuki ambazo awali zilifanyika kiwandani.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...