Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameitaka Serikali kuacha siasa kwenye masuala ya kiuchumi, ukiwamo mgogoro kati ya Tanzania na Kenya kuhusu sekta ta utalii.
Akifungua kikao cha Baraza la Uongozi wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Arusha jana, Mbowe aliwataka viongozi Serikali kutumia busara kushughulikia mgogoro huo ulioibuka baada ya Kenya kuzuia magari yenye usajili wa Tanzania kufika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.
“Asilimia 40 ya watalii zaidi ya milioni moja wanaokuja Tanzania kila mwaka, hupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Hatustahili kugombana nao, bali tunapaswa kutafuta namna bora ya kushirikiana. Tuna uwezo wa kuchagua marafiki, lakini kamwe hatuwezi kuchagua majirani. Hawa (Kenya) ni wenzetu, tutaendelea kuwa nao pamoja maisha yote.
“Tutunge sera nzuri ya usafiri wa anga na kuvutia kampuni kubwa za ndege kuja kuwekeza nchini kwa kutumia viwanja vyetu, Kilimanjaro, Zanzibar, Dar es Salaam na Mbeya,” alisema.
Kuhusu sera na mfumo mpya wa elimu uliozinduliwa juzi na Rais Jakaya Kikwete, Mbowe alisema tatizo la sekta ya elimu siyo sera, bali bajeti finyu na usimamizi mbovu.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment