2015-02-02

Ni balaaaaaaaa!!!!!!!!!!! Fagio la Mwakyembe kule Uchukuzi, Sitta umeliona au…



Binafsi, ninaamini hivyo, hasa baada ya uamuzi wake wa wiki moja iliyopita wa kubadili Baraza la Mawaziri ili kujaza nafasi za mawaziri wake wawili waliokumbwa na kashfa.

Ni dhahiri kusema kuwa kufanya kazi na Rais Jakaya Kikwete na hasa ukiwa mmoja wa wasaidizi wake wa karibu kwa hakika ni mzigo mzito.

Binafsi, ninaamini hivyo, hasa baada ya uamuzi wake wa wiki moja iliyopita wa kubadili Baraza la Mawaziri ili kujaza nafasi za mawaziri wake wawili waliokumbwa na kashfa.

Kama kawaida, uamuzi ule ukapokewa kwa hisia nyingi tofauti na Watanzania mijini na vijijini. 


Wapo wale wachache au wengi waliohoji sababu za msingi, kwa mfano za kumbadilishia kituo cha kazi aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe na kumpeleka Ushirikiano wa Afrika Mashariki, akibadilishana na mkongwe, Samuel Sitta.

Sina shaka kuhusu uwezo wa Sitta kwani yeye ni kiongozi mzoefu katika medani ya siasa nchini ambaye ameitumikia nchi kwenye nafasi mbalimbali, ingawa ile inayomtambulisha zaidi hadi sasa ni ile ya kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa uongozi wa Awamu ya Tatu, chini ya Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

Akiwa spika, Sitta aliyekuwa akisaidiwa na Spika wa sasa, Anne Makinda alikuwa na kaulimbiu ya kasi na viwango, ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo iliyomjenga na hata kumpa heshima wakati akiongoza mhimili huo mmoja wa dola. Ni heshima ambayo nusura iingie doa wakati akiongoza Bunge Maalumu la Katiba mwaka jana, ambako matukio kwenye kikao hicho na uamuzi wa mwanasiasa huyo viliacha nyuma maswali mengi. 
 Hata hivyo, kama nilivyosema wiki chache zilizopita kuwa, tatizo letu sisi (Watanzania) ni kupenda kufanya mambo kwa maneno, wala si vitendo, ndiyo maana kaulimbiu kama ile ya Sitta inaweza kuonekana kwenye makaratasi.

Ni tofauti na kina Dk Mwakyembe na wengineo ambao wameyaishi maneno yao. Akiwa Uchukuzi, Dk Mwakyembe aliwanyima usingizi wengi, wakiwamo watendaji wa idara, taasisi zote zilizokuwa chini ya wizara yake.

Ndiyo maana siku ya Jumamosi Rais Kikwete alipotangaza uamuzi wa kumwondoa Dk Mwakyembe kutoka Uchukuzi, nimeambiwa kuwa, wapo baadhi ya watumishi wa taasisi zile zile au idara waliokesha wakila na kunywa, eti wakisherehekea kuondolewa kwa mbaya wao.

Ninajua ni kweli wapo, hivyo basi hao watakuwa walisahau kuwa Dk Mwakyembe alikuwa kiongozi wa taasisi, wala ile haikuwa kama nyumba yake mwenyewe na ndiyo maana amekuja Sitta, naamini kwa spidi na viwango vile vile amevaa viatu vya mtangulizi wake, hawezi kutumia miezi michache iliyobaki ya uongozi wa sasa kuacha uchafu urejee bandari, viwanja vya ndege au kwingineko ambako Dk Mwakyembe alikuwa amesafisha. 



Ni imani yangu kuwa fagio lile lile ambalo alilitumia Dk Mwakyembe kufanyia usafi kwenye taasisi na idara zilizoko kwenye wizara ile bado lipo, tena ni bichi, kiasi kwamba Sitta ameliona, atalitumia ili kuondoa uchafu na maovu yaliyozifanya bandari zetu ikiwamo ya Dar es Salaam zikimbiwe au kupungukiwa na wateja kutoka nchi jirani ambao awali walizitumia kuingiza au kutoa mizigo yao, lakini wizi, urasimu na umangimeza vikawaondoa.

Nilisema awali kuwa, kufanya kazi na Rais Kikwete ni kazi ngumu kwani ninajiuliza wateule wake, kiasi cha 60 waliofanya kazi naye wakiwa mawaziri au naibu wao, wanamwonaje leo? Huenda wapo waliotupwa lakini bila kukosea, kushindwa kazi na wakati mwingine bila kufanya kosa lolote.
 Inawezekana kwa wengine waliponzwa na usemi ule wa kuvuja kwa pakacha, nafuu kwa mchukuzi, kwamba walipoondolewa, wengine waliingia na kupata ulaji, maisha yakasonga mbele.

Kama nilivyoeleza awali, si nia yangu kupingana na mtazamo wa Rais Kikwete kumteua fulani kuwa msaidizi wake, kushika nafasi ya uongozi, ila, ninachokiangalia ni kuona jinsi ambavyo wasaidizi wake, hasa mawaziri, walivyogeuka zaidi wasemaji, wala si watendaji.



Mwananchi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...