2015-02-02

Ni hatariiiiiiiiii!!!! Moto kumwakia Nyalandu bungeni leo


              Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu

Ni katika ripoti ya Kamati ya Maliasili na Mazingira inayotarajiwa kuwasilishwa leo

Moshi. Wabunge wamejipanga kumweka kitimoto Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu kwa kutotekeleza hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu tozo za hoteli za kitalii mbugani na hivyo kusababisha Serikali ipoteze mapato ya Sh21 bilioni kwa mwaka.

Nyalandu anatarajiwa kuwekwa kitimoto bungeni mjini Dodoma leo wakati Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira inayoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli itakapowasilisha taarifa yake ya kazi.

Mwaka 2007 Bunge lilipitisha sheria inayotaka wamiliki wa hoteli hizo kulipa kati ya Dola za Marekani 35 hadi 50 kwa siku kwa kila mgeni anayelala katika hoteli hizo ikiwa ni tozo kwa ajili ya uhifadhi.

Awali, hoteli hizo zilikuwa zikitozwa kati ya Dola 6 hadi 8 na wakati huo gharama ya mgeni kulala katika hoteli hizo ilikuwa kati ya Dola 100 hadi 200 kwa siku. 


Kiwango hicho cha tozo kiliongezwa kutokana na utafiti kuonyesha kuwa hoteli hizo zilikuwa zimepandisha bei ya kulala kwa siku na kuwa kati ya Dola 800 hadi 1,000 kwa siku.

Baada ya kupandishwa kwa tozo hiyo, baadhi ya wamiliki wa hoteli hizo waliigomea na kukimbilia mahakamani, lakini Septemba 12, 2014 Mahakama ikatupilia mbali malalamiko yao.

“Katika hukumu, Jaji aliagiza waziri mwenye dhamana kutangaza mara moja tozo hizo kwenye Gazeti la Serikali lakini leo ni mwezi wa sita waziri hajatangaza,” alidai mbunge mmoja ambaye aliomba jina lake lisitajwe na kusema waziri angeeleweka kama kungekuwa na rufaa kupinga hukumu hiyo, lakini hadi sasa hakuna rufaa yoyote.

“Wakati Serikali ikilia haina fedha, inapoteza mapato ya Sh21 bilioni kwa mwaka. Kwa kweli hapatatosha kama hawezi atupishe waje wengine.”

Hukumu hiyo ya kesi namba 25/2011 iliyofunguliwa na kampuni 17 za hoteli, ilitolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha, Stella Mugasha.

Jaji Mugasha alimwagiza Waziri wa Utalii kutangaza mara moja tozo hizo kwenye Gazeti la Serikali ili kuiwezesha Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa) kuikusanya ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. 


“Msimamo unaoendelea wa kutotangaza tozo hizo unakwenda kinyume na sera na masilahi ya umma jambo ambalo ni wajibu wa kiongozi aliyeaminiwa na kukabidhiwa ofisi ya umma na katika shauri hili ni waziri wa utalii,” ilisema hukumu hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Grace Kiwelu ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo alipoulizwa jana, alisema: “Tangu 2011 mpaka sasa tumeshapoteza Sh80 bilioni halafu Serikali inalia haina fedha. Nimeomba kuchangia na kwa kweli nitahitaji majibu.
 Tunataka kujua kigugumizi hiki cha Nyalandu kinasababishwa na nini. Mahakama imesema atangaze mara moja kwenye Gazeti la Serikali yeye mpaka leo kimya. Kuna nini?” 

Mwananchi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...