Mtu
mmoja aliyefahamika kwa jina la Reus Amosi (50), Mkazi wa Uhamila, Kata
ya Ubaruku, Tarafa ya Rujewa katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya
amekutwa ameuawa kwa kunyongwa shingo kisha mwili wake kutupwa kwenye
mfereji wa umwagiliaji wa Highland Estate mjini hapa.
Tukio hilo la kikatili lilitokea hivi karibuni ambapo mwili wa marehemu ulikutwa kwenye mfereji huo saa 12:45 mchana eneo hilo la Uhamila, ukiwa umeharibika.
Chanzo chetu ambacho kilikuwa eneo la tukio kilidai kuwa marehemu Reus alitoweka nyumbani kwake tangu Februari 24, mwaka huu huku ikidaiwa kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mmoja (jina linahifadhiwa) mkazi wa Isisi.
Chanzo kiliendelea kueleza kuwa mwanamke huyo ambaye mume wake alishafariki dunia siku nyingi zilizopita, bado alikuwa anaishi pamoja na watoto wake kwenye nyumba ya marehemu mume wake.
“Kuna madai kuwa kuna watu walikuwa wanachukizwa au kumuonea wivu Reus kutokana na kitendo chake cha kuingia katika nyumba ya marehemu ambayo hakuijenga yeye na kulala humo,” kilisema chanzo hicho.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, SACP Ahmed Msangi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kufafanua kuwa watu wanne wamekamatwa kwa mahojiano kuhusiana na kifo hicho.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Ruth Msosi (30), Thomas Minzi (46), Stefano Kibwana (50) na Belina Kipamana(50), wote wakazi wa Isisi
0 comments:
Post a Comment