2015-03-30

Mahakama ya Kadhi yawavuruga wabunge


Na Debora Sanja na Fredy Azzah, Dodoma
WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jana nusura wazichape kavukavu baada ya kutofautiana juu ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi.

Hali hiyo ilijitokeza wakati wabunge hao wakiwa katika semina iliyohusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali, ambapo miongoni mwa sheria zilizomo ndani yake ni pamoja na ile ya Mahakama ya Kadhi.
Sakati hilo lilitokea katika semina kuhusu muswada huo unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni keshokutwa iliyofanyika katika Ukumbi wa Msekwa, mjini hapa.

Licha ya badhi ya wabunge kutaka kunyanyuka kwenye viti vyao na kwenda kupigana, wapo waliokuwa wakirushiana maneno makali.

Semina hiyo ilianza katika hali ya utulivu, lakini baada ya muda hali ya hewa ilichafuka baada ya baadhi ya wabunge kusimama na kupinga sheria hiyo.

Hali ilibadilika baada ya Mbunge wa Kisarawe, Seleman Jafo (CCM), aliposimama na kuchangia ambapo aliunga mkono muswada huo.

Katika mchango wake, Jafo aliwashangaa Wakristo kujifanya wazungumzaji wakubwa kuhusu suala hilo la Mahakama ya Kadhi wakati jambo hilo haliwahusu.

“Nataka niwaambie Serikali msije mkafanya masihara Muswada huu usiingie bungeni, muswada uje tutafanya ‘Amendment’ (marekebisho) huko na naitahadharisha Serikali iwe makini katika hili,” alisema Jafo.

Alipokuwa akichangia, baadhi ya wabunge walikuwa wakimzomea na kusababisha mbunge huyo kususa kuendelea kuchangia ambapo alilazimika kwa kuwataka wabunge waislamu wakutane nje baada ya kumalizika kwa semina hiyo.

Kauli ya Jafo ya kuwataka wabunge Waislamu kukutana baada ya semina ilionekana kuwachefua baadhi ya wabunge ambapo walisimama na kupinga kauli hiyo, huku wengine wakitoka nje ya ukumbi huo.

Wabunge waliosimama na kuanza kumpinga Jafo ni pamoja na Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul (Chadema), Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM) na Mbunge wa Nyamagana, Hezekiah Wenje (Chadema).

Wakati hali hiyo ikiendelea, Mbunge wa Chwaka, Yahaya Kassim Issa (CCM) na Mbunge wa Konde, Khatibu Saidi Haji, (CUF) walisimama na kutaka kwenda kumshambulia Machali, kabla ya kuzuiwa na wenzao waliokuwa wamekaa nao jirani.

Hali hiyo ya vurugu na makelele iliendelea kwa takribani dakika 10, huku baadhi ya wabunge wakitaka semina ivunjike.

Wakati vurugu hizo zikimshinda aliyekuwa Mwenyekiti wa semina hiyo, William Ngeleja, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alikuwa mgeni rasmi katika semina hiyo, walikua wameketi kwenye viti vyao huku Spika Anne Makinda akilazimika kusimama na kuanza kuwatuliza wabunge hao.

Mbunge wa Sumve, Richard Ndasa (CCM), alisema katika katiba Ibara ya 19 ilishaweka wazi kuhusu suala la uhuru wa kuabudu kwamba jumuiya zote za kidini zitakuwa nje ya mamlaka za nchi.

Mwenyekiti wa kikao hicho (Ngeleja) alimtaka Ndasa avute subira kusikia maudhui ya semina hiyo huku akisisitiza kwamba hakuna kipengele chochote cha Katiba kilichovunjwa.

Mbunge wa Ngara, Deogratius Ntukamazina (CCM), alisema yeye kama mjumbe wa Kamati ya Bunge Katiba na Sheria walikutana na makundi 11 ya masheikh lakini yaliukataa muswada huo.

“Waislamu hawa walisema wao hawaitambui Bakwata (Baraza Kuu la Waislamu Tanzania), naiomba Serikali kwa jambo hili kubwa la Mahakama ya Kadhi hamuwezi kulileta kwa marekebisho madogo kama haya.

Mbunge wa Viti Maalumu, Rukia Kasim Ahmed (CUF), alipinga kitendo cha mahakama hiyo kuanzishwa chini ya uratibu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), kwa madai kwamba ni taasisi ya mtu binafsi iliyosajiliwa na Rita kama zilizovyo taasisi nyingine.

“Suala hili halikubaliki, kwa nini Mahakama ya Kadhi iundwe chini ya Mufti, au Waziri Mkuu anataka tu kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi kwa kuwa alishaahidi, msitake kuipasua hii nchi.

“Kama waziri mkuu yeye aliahidi kwa ajili ya kuutafuta urais shauri yake ila ni marufuku kuwalazimisha watu kuwa chini ya Bakwata, kufanya hivyo ni kukiuka Katiba.

“Huyu Mufti anapatikana kwa mujibu wa Katiba ya Bakwata, na Bakwata ni taasisi tu, Waziri Mkuu anajua suluhisho la jambo hili.

“Tume ya watu 25 iliundwa kulishughulikia, baadae ikawaundwa ya watu watano kupanga muundo wa Mahakama ya Kadhi, lakini leo hii anawapa Bakwata, Waziri Mkuu ndio chanzo cha yote haya, suala hili halikubaliki na tutalipinga,” alisema.

Mbunge wa Kasulu Mjini,Moses Machali (NCCR-Mageuzi) alisema wabunge hao wanakosea kulijadili suala hilo na kwamba tayari limeleta mgawanyiko baina ya waislamu wenyewe.

“Inawezekana waziri mkuu aliahidi jambo hili kwa malengo ya urais, na kama muswada utaingizwa ndani ya Bunge, na sisi wakatoliki tutaleta mabadiko yetu ya Canon Laws, huko Mbeya na wenyewe madhehebu yao yote wataleta mabadiliko yao,” alisema.

Mbunge wa Tarime, Nyambari Nywangwine (CCM) pamoja na kusema kwamba jambo hilo ni zito alisema taasisi za dini ziliukataa katika Kamati ya Bunge na kwamba Bakwata walitoa masharti kwamba Serikali igharamie.

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) alisema Serikali isipokuwa makini Bunge linaweza kuingia katika historia ya kuivuruga nchi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa (CCM) alisema Nyerere na Karume hawakuwa wajinga waliposema nchi haina dini na kutahadharisha kuwa Serikali isopokuwa makini inaweza kuliingiza taifa kwenye machafuko ambayo hayajawahi kutokea na kwamba yeye hata kubali hilo litokee.

Kwa upande wake Mbunge wa Mwanakwerekwe, Haji Juma Sereweji (CCM), alitaka muswada huo uwasilishwe bungeni na kwamba wabunge watapewa nafasi ya kupendekeza marekebisho yao.
“Sioni sababu ya kwanini muswada usipelekwe bungeni, yule ambaye anaona haufai siku hiyo wasije bungeni au watotke nje.

“Karume alikubali Mahakama ya Kadhi ndio maana Zanzibar ipo, Nyerere alishauri kuanzishwa kwa Bakwata ili waislamu wawe na sehemu yao ya kusemea, sheria hii iletwe ili waislamu wasimamie mambo yao,” alisema.

Mbunge wa Nkasi Kasikazini, Ali Keissy, alisema hakubaliani na suala la Mahakama ya Kadhi kwani siyo kati ya nguzo kuu za Waislamu.

Akifunga semina hiyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema baada ya kusikiliza wabunge hao alitambua kuwa ndani ya Waislamu wenyewe hakuna maelewano juu ya uanzishwaji wa mahakama hiyo.
Alisema kuwa, baada ya kuona hali hiyo serikali itaona kama jukumu lake kurekebisha hiyo hali au laa.

“Kwamba baadhi ya Waislamu hatujawafikisha pale wanapotaka, lakini hiki ni matokeo ya mjadala ulioibuka ndani ya Bunge la Katiba,” alisema Pinda.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...