2015-03-04

Ngeleja awatumia Zitto, Mengi, Manji kujitetea


Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja akiapa kabla ya kuanza kuhojiwa na Baraza la Sekretarieti ya Viongozi wa Umma, Dar es Salaam jana.

Ngeleja ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini alikuwa anajitetea mbele ya baraza hilo kuhusiana mgawo wa Sh40.4 milioni, aliopata kutoka kwa mfanyabiashara na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engeneering & Marketing Limited, James Rugemalira.

Dar es Salaam. Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja jana alimtaja Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe na baadhi ya matajiri wanaowafadhili wabunge nchini, kama sehemu ya utetezi wake mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.

Ngeleja ambaye amewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini alikuwa anajitetea mbele ya baraza hilo kuhusiana mgawo wa Sh40.4 milioni, aliopata kutoka kwa mfanyabiashara na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engeneering & Marketing Limited, James Rugemalira. 

Pamoja na kudai kuwa mgawo huo haukuwa na mgongano wa masilahi, Ngeleja aliibua tuhuma mpya akihoji ni kwa nini Zitto hakuhojiwa na baraza kwa kutuhumiwa kupokea fedha kutoka katika Kampuni ya Pan African Power Solution (PAP), ambayo pia inahusishwa katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa ndani ya Benki Kuu ( BoT) wala tuhuma za kufadhiliwa na Mfuko la Hifadhi ya Jamii (NSSF).

Mashtaka dhidi ya Ngeleja

Akimsomea mashtaka, Mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mwanaarabu Talle alidai kuwa Ngeleja akiwa kiongozi wa umma alipokea fedha hizo kwenye akaunti yake namba 0011010265260 katika Benki ya Mkombozi na hivyo kusababisha mgongano wa kimaslahi.

Wakili Talle alidai kuwa kwa kupokea fedha hizo kutoka kwa kampuni hiyo, Ngeleja alikiuka kifungu cha 6(e) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kinachozuia kiongozi wa umma kujiingiza katika mgongano wa masilahi.

Pia wakili Talle alidai kuwa Ngeleja alijipatia manufaa ya kifedha kinyume cha kifungu cha 12 (1) (e) cha sheria hiyo.

Ushahidi wa sekretarieti

Baada ya kumsomea mashtaka hayo, Ngeleja alikana na shahidi wa Sekretarieti, Waziri Yahya akiongozwa na Wakili Talle alidai kuwa baada ya kuchunguza walibaini kuwa Ngeleja alipewa Sh40,425,000 kutoka VIP Engeneering & Marketing Februari 12, 2014. 

Alidai kitendo cha Ngeleja cha kupokea pesa hizo kumekiuka sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo hairuhusu kuomba, kupata au kupokea fedha.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, walibaini kuwa mwaka 2007 Ngeleja alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na kwamba kuanzia 2008 hadi 2012 alikuwa Waziri wa Nishati na Madini ambapo aliendelea na majukumu ya kusimamia utekelezaji wa mkataba kati ya Tanesco na IPTL ambayo VIP ilikuwa na hisa.

Alidai kitendo cha Ngeleja baadaye kupokea fedha kutoka kwa kampuni hiyo ni kujiingiza katika mgongano wa masilahi na kwamba ni muhimu viongozi wa Serikali wakasimamia misingi ya maadili ya viongozi, vinginevyo itasababisha wananchi wasiwe na imani na Serikali.
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...