Atamba ana fedha kuliko mamilioni aliyogawiwa, Adai hajui ni za nini ingawa alizifungulia akauntiMnikulu, Shaban Gurumo.
Mnikulu, Shaban Gurumo, amekiri kupokea mgawo wa zaidi ya Sh. milioni 80.8 kutoka kwa mmiliki wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing, James Rugemalira, unaodaiwa kuwa ni sehemu ya zaidi ya Sh. bilioni 200 zilizochotwa kifisadi katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lakini akasema hata kama asingepata, angeweza kutatua shida zake kwa kuwa anamiliki fedha zaidi ya hizo.
Pia ametaka watu wote, wakiwamo wabunge na baadhi ya vyombo vya habari waliohusika kutangaza kwamba, alipokea Sh. milioni 800 kutoka kwa Rugemalira wakati siyo kweli, wachukuliwe hatua kama zilizochukuliwa dhidi yake, ikiwamo kuhojiwa na kufikishwa mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, kujieleza kuhusiana na hilo.
Alisema hayo wakati akiongozwa na wakili wake, Lucas Kamanija, kujieleza kuhusiana na malalamiko dhidi yake, yaliyowasilishwa na wanasheria wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma mbele ya baraza hilo, jijini Dar es Salaam jana.
Gurumo alidai Rugemalira ni rafiki yake takriban miaka 10 sasa, ndiye aliyemshauri kufungua akaunti kwenye Benki ya Biashara ya Mkombozi, tawi la St. Joseph, jijini Dar es Salaam, kabla ya kumuingizia Sh. 80, 850,000 katika akaunti hiyo.
Alidai aliyemuunganisha na Rugemalira, ni Dk. Fred Limbanga wa hospitali binafsi ya Sanitas, iliyoko Mikocheni, Dar es Salaam, ambaye jana alifika katika baraza hilo kutoa ushahidi upande wa utetezi.
AMSHANGAA RUGEMALIRA
Hata hivyo, Gurumo aliliambia baraza hilo linaloongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Hamisi Msumi, kuwa hakutambua kusudio la Rugemalira kumuwekea fedha hizo kwenye akaunti hiyo.
Alidai anahisi pengine Rugemalira alifanya hivyo kwa kuwa kipindi hicho alikuwa ana mgonjwa anayesumbuliwa na maradhi ya saratani.
Hata hivyo, alidai hakujishughulisha kabisa kuuliza ili kujua sababu za Rugemalira kumuwekea fedha hizo kwenye akaunti yake.
Alidai aliitwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kuhojiwa na kutakiwa kwenda na nakala ya taarifa ya benki hiyo, ambayo aliitambua jana mbele ya baraza hilo.
Hata hivyo, alidai yeye na Rugemalira hawajawahi kuzungumzia lolote kama fedha hizo ziliwekwa kwenye akaunti hiyo na kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited, kama hati ya malalamiko ilivyoeleza.
Alidai anafahamu kuwa kila mwaka mtumishi wa umma anatakiwa kutamka kwenye fomu maalumu ya ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu mali na madeni anayomiliki.
Kutokana na hali hiyo, alidai kila mwaka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imekuwa ikimwandikia barua kumtaka afanye hivyo na kwamba, mara ya mwisho aliyoandikiwa ilikuwa Oktoba 2, mwaka jana.
Alidai aliwahi kuwasilisha fomu kama hiyo kwenye Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Septemba 29, ambayo ilipokelewa siku hiyo hiyo na kwamba, tarehe ya mwisho kuwasilisha tamko kwenye sekretarieti hiyo ilikuwa Desemba 31, mwaka jana.
Gurumo alidai hajawahi kutumia cheo chake kupata manufaa kutoka kwa mtu yeyote na pia haijawahi kuingia akilini mwake kuifikiria kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited.
Pia alidai hajawahi kuwa na uhusiano na Rugemalira wa kiuchumi wala wa kibiashara.
BUNGE, VYOMBO VYA HABARI
Alidai tuhuma kwamba, alipokea Sh. milioni 800 kutoka kwa Rugemalira, kwa mara ya kwanza alizisikia redioni zikizungumzwa na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, bungeni, akiwa ndani ya gari akitokea nchini Afrika Kusini.
Alidai baadaye tuhuma hizo zilichapishwa kwenye baadhi ya magazeti na katika mitandao ya kijamii.
“Awali, lilipokuja kwenye Sekretarieti (ya Maadili ya Viongozi wa Umma), cha kwanza lilikuwa ni Bunge na vyombo vya habari. Kwa sababu hiyo, kama inaruhusiwa, wahusika wachunguzwe nao wapitie kwenye mikondo hii hii, ambayo mimi napitia,” alisema Gurumo.
Alidai hata siku moja hajawahi kuwa na maslahi ya kiuchumi na Rugemalira, mbali na ya kifedha na pia hana uhusiano wowote na kampuni ya VIP Engineering and Marketing.
Hata hivyo, akihojiwa na Wakili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Getrude Cyriacus, Gurumo alikiri kuwa Rugemalira ni mmiliki wa VIP Engineering and Marketing Limited.
ADAI KUWA ANA FEDHA NYINGI
Pia alikiri kuwa taarifa ya benki iliyotolewa ikionyesha aliingiziwa fedha hizo na VIP Engineering and Marketing iliyowasilishwa katika baraza hilo na shahidi wa upande wa malalamiko, Basilio Mwanakatwe jana kama kielelezo, ndiyo aliyoipeleka kwenye kamati ya uchunguzi ya sekretarieti hiyo ilipomhoji.
Vilevile, akihojiwa na wakili huyo, Gurumo alikiri kutumia fedha alizopewa na Rugemalira kwa matumizi yake binafsi.
“Ningeweza kufanya hivyo bila kutumia fedha hizo (alizopewa na Rugemalira). Nina fedha zaidi ya hizo za Rugemalira,” alitamba Gurumo mbele ya baraza hilo jana.
Alidai kila mfuko wa suruali aliyovaa umesheheni fedha, hivyo daima maishani mwake hapatwi na ukata kiasi cha kutegemea fedha za Rugemalira.
“Hapa nina fedha na huku nina fedha,” alisema Gurumo mbele ya baraza hilo, huku akijipigapiga kwenye mifuko ya suruali aliyovaa jana.
Hata hivyo, alikana fedha alizopewa na Rugemalira kuwa zilikuwa ni zawadi na pia alipotakiwa na Wakili Getrude kueleza kama zilikuwa ni mshahara au posho aliyolipwa na VIP Engineering and Marketing Limited na siyo zawadi, Gurumo alisisitiza kuwa hajui.
ADAI HAKUJUA FEDHA ZA NINI
Pia alipotakiwa na Wakili Getrude kueleza kama aliwahi japo tu kujiuliza sababu ya kupewa fedha hizo, Gurumo alisema hakuwa nayo na kwamba, tafsiri ya zawadi katika fedha alizopewa na Rugemalira haipo.
Akijibu swali la wakili mwingine wa upande wa malalamiko, Hassan Mayunga, Gurumo alidai pia kuwa hakujua kama fedha hizo ni zawadi au manufaa.
Pia akiongozwa na Wakili Kamanija, Gurumo alidai siyo sekretarieti hiyo tu, bali hata afisa ma-suul wake, ambaye ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais hana uwezo wa kumpangia matumizi ya fedha na kwamba, Rugemalira hajampa utaratibu wowote wa kutumia fedha alizompa.
Awali, shahidi wa upande wa malalamiko, Mwanakatwe, ambaye ni Afisa Uchunguzi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, akiongozwa na Wakili Mayunga, alidai alikutana na Gurumo Desemba 19, mwaka jana wakati wa uchunguzi walioufanya dhidi yake kutokana na taarifa walizozipata kutoka vyanzo mbalimbali, ikiwamo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Alidai katika uchunguzi huo, walibaini kuwa Februari 5, mwaka jana, Gurumo alipokea kiasi hicho cha fedha kupitia tawi la benki hiyo na kwamba, katika mahojiano, alikiri kupokea fedha hizo.
Kutokana na hali hiyo, alidai kuwa Gurumo alikiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma inayokataza kiongozi wa serikali kupokea zawadi zaidi ya awadi ndogondogo na ukarimu wa kawaida, pia inakataza kiongozi wa umma kudai, kuomba au kupokea maslahi ya kiuchumi zaidi ya ukarimu wa kawaida au zawadi ndogondogo.
Alidai kamati ya uchunguzi pia ilibaini kuwa Gurumo hakutamka zawadi aliyopokea wala thamani yake na hakuikabidhi kwa afisa mas-uul wake ili amwambie matumizi yake na namna ya kushughulika nayo.
Shahidi huyo alidai pia kuwa kamati ilibaini kuwapo na mgongano wa maslahi na kwamba, Gurumo kwa nafasi aliyonayo serikalini, anafahamu siri nyingi, hivyo kitendo chake cha kupokea kwa mfanyabishara, ni dhahiri kuwa hakupanga mambo yake namna ambayo ingemzuia kujiingiza kwenye mgongano wa kimaslahi.
“Viongozi wa umma ndiyo injini ya uendeshaji, wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa viwango, wanapaswa kuonyesha mfano.
Ukiukwaji wa maadili unaweza kuwakosha wananchi imani na serikali yao,” alidai shahidi huyo.
Hata hivyo, akihojiwa na Wakili Kama shahidi huyo alidai kuwa taarifa kwamba, Gurumo alipokea Sh. milioni 800 kutoka kwa Rugemalira, hazina ukweli na ndiyo alihojiwa na kamati ya uchunguzi ya sekretarieti kwa kuwa hawana utaratibu wa kupokea na ‘kumeza’ porojo.
Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Msumi alizipa pande mbili za shauri hilo muda hadi Machi 13, mwaka huu, wa kuwasilisha kwa maandishi maelezo yake ya mwisho kabla ya kuandaa maamuzi na kuyapeleka kwa mamlaka husika za nidhamu dhidi ya mlalamikiwa.
Leo baraza hilo linatarajia kusikiliza malalamiko dhidi ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Philip Saliboko, anayetuhumiwa kupokea Sh. milioni 40.4 katika mgawo wa fedha zilizochotwa katika akaunti ya Tegeta Escrow.
0 comments:
Post a Comment