Showing posts with label SIASA. Show all posts
Showing posts with label SIASA. Show all posts

2015-04-10

Zitto Kabwe Asema Kitendo Cha kuitwa MSALITI Ni Mbinu Zinazotumika Kumuua Mwanasiasa wa Upinzani

Kiongozi wa chama cha ACT-Tanzania,Zitto Kabwe amesema kuitwa msaliti ni mbinu zinazotumika 'kumuua' mwanasiasa wa upinzani nchini.

Amesema mwanasiasa wa upinzani akitakiwa kuuawa kisiasa si jambo geni kusikia anatuhumiwa kutumika na Usalama wa Taifa au Pandikizi la Chama cha Mapinduzi, CCM.

Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dae es Salaam juzi,Zitto alisema kauli kama hiyo ilitumika kumshusha kisiasa mjumbe wa kamati kuu ya CHADEMA, Mabere Marando na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.

"Si jambo jipya, mmesahau kwamba Mbatia aliitwa pandikizi,leo Mbatia yuko wapi,si yuko meza moja na UKAWA?

"Mmesahau baada ya serikali ya Umoja wa kitaifa juzi tu hapa kwamba CUF waliitwa CCM-B, mmesahau kwamba CUF waliitwa mashoga, leo kiko wapi?

"Mmesahau Marando aliitwa pandikizi, tena dhidi ya Mrema(Mwenyekiti wa TLP),leo Marando ni shujaa na Mrema tunamtukana.Hizi ni siasa tu na zitaendelea tu," alisema

Aidha alisema kuna watu wengine wataibuka baadaye nao wataanza kulaumiwa, kama Mwalimu Nyerere alivyosema.....Ukishakula Nyama ya Mtu Huachi.

Kutokana na hali hiyo alisema, walioitwa wasaliti wametoka huko walikokuwa na watasikika wasaliti wengine wanaibuka kwa sababu siasa iko hivyo..

"Juzi nimemsikia Halima Mdee anasema mimi siyo ACT,ninyi mliwahi kuandika kama Halima ni ACT,hiyo maana yake nini,inamaanisha kuna presha anapigwa huko.

"Angalau Shibuda ni mtu ambaye haeleweki misimamo yake ni nini, lakini hivi ni vitu vya kawaida,"alisema.


Akizungumzia kutumiwa na vyombo vya usalama,Zitto alisema yeye kama kiongozi hawezi kuacha kuwasiliana na watu wa usalama wa Taifa.

"Huwezi kuwa kiongozi wa chama kikubwa kinachojiandaa kushika dola usiwe na uhusiano na Mkuu wa Jeshi la Polisi,Mkuu wa jeshi la wananchi au Mkuu wa Usalama wa Taifa,utakuwa ni kiongozi wa ajabu sana." Alisema

2015-04-09

Zitto Kabwe Aanza Na Ngome Kuu ya CCM


Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe anaanza ziara yake ya kwanza ya ujenzi wa chama hicho kipya mwishoni mwa wiki hii kwa kutembelea mikoa ambayo inachukuliwa kama ngome za Chama Cha Mapinduzi ( CCM ).

Zitto ambaye aliacha uanachama na ubunge wake wa CHADEMA mwishoni mwa mwezi uliopita, atafanya mkutano wake wa kwanza wa kisiasa mkoani Ruvuma.

Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa iliyobaki hapa nchini ambayo haijawahi kuwa na walau mbunge mmoja kutoka chama cha upinzani tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa zaidi ya miaka 20 iliyopita.

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinaeleza kwamba katika ziara hiyo, ACT-Wazalendo kinatarajiwa kufanya mikutano ya kisiasa kwenye mikoa 10 tofauti katika kipindi cha takribani wiki mbili. 
Kwa mujibu wa ofisa habari wa chama hicho,Abdallah Hamis, mikoa ambayo ACT kitaanza kujitangaza kwa mara ya kwanza ni Ruvuma,Njombe,Iringa,Morogoro,Dodoma,Singida,Tabora,
Shinyanga,Mara na Mwanza.

"Tutaanza mkoa wa Ruvuma mwishoni mwa wiki hii na kuelekea kwenye mikoa hiyo mingine kwa mujibu wa ratiba.Viongozi wa juu wa chama wamefanya uamuzi wa kuanza kazi na mikoa ambayo CCM imekuwa ikishinda.

"Ile kazi ya kufyeka pori ndo sasa inaanza rasmi.Chama kimeona itakuwa busara kuanza na maeneo mapya ambako kuna fursa nzuri zaidi ya kuleta mabadiliko.

"Baadaye tutakwenda kwenye mikoa mingine, lakini la msingi ni kuanza kazi katika maeneo magumu na kumalizia katika yale ambayo mbegu zimeshapandwa tayari,"alisema Hamis

Mikoa ya Ruvuma,Njombe,Morogoro,Dodoma na Tabora haina mbunge hata mmoja kutoka miongoni mwa vyama 22 vya upinzani vilivyopo hapa nchini,wakati mikoa ya Singida,Mara,Mwanza,Shinyanga na Iringa ina walau mbunge mmoja wa upinzani.

Akiwa Naibu katibu mkuu wa CHADEMA,Zitto alikuwa mmoja wa wahusika wakuu katika kile kilichoitwa "Oparesheni Sangara" iliyokuwa kampeni maalumu ya kukitangaza chama hicho katika mikoa ya kanda ya ziwa ambayo ndiyo inatajwa kuwa chachu ya kukua kwa ushawishi wa vyama vya upinzani kwenye mikoa hiyo.

Kwa mujibu wa Hamis,katika ziara hiyo,Zitto atafuatana na takribani viongozi wote wa juu wa chama hicho,akiwemo mwenyekiti Anna Mghwira, na katibu mkuu,Samson Mwigamba. 

Zitto na Mwigamba wanauzoefu wa kufanya mikutano ya hadhara katika sehemu mbalimbali hapa nchini tangu wakiwa CHADEMA,lakini kwa Mghwira hiyo itakuwa ni mara yake ya kwanza, akitarajiwa kuwa kivutio katika mikutano hiyo.

Mgwira ameingia katika historia ya Tanzania kama mwanamke wa kwanza kupewa wadhifa wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Siasa, baada ya kumshinda Estomil Mala katika uchaguzi wa ndani wa ACT uliofanyika jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa mwezi ulipita.

Chadema kumng’oa Mwenyekiti wa CCM................ni balaaaaaaaaaaaaaaa


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tawi la Mbigiri wilayani kilosa, kimesema kitamng’oa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Hemed Ibrahim Salim, kama ataendelea kutoitisha vikao kwa kisingizio cha kuogopa kukataliwa kwa kukosa taarifa ya makabidhiano.

Akizungumza na Tanzania Daima, Mwenyekiti wa Chadema Tawi hilo, Maftaha Hamis, alimtuhuhu, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho kwamba, alichapisha Vitabu vya Risiti za Michango kwa ajili ya ufuatiliaji wa Mgogoro wa Wakulima na Wafugaji, ikidaiwa fedha hizo zilizokusanywa; Zimetafunwa.

Awali ilifahamika kwamba, Mwenyekiti Salum anabanwa kuhusu taarifa ya makabidhiano ya Serikali ya Kijiji hicho kwa sababu, kabla ya kuchaguliwa Desemba 14, mwaka jana kwenye uchaguzi wa Serikali mitaa, kwa kuwa alikuwa mwenyekiti wa Mpito, baada ya aliyekuwa mwenyekiti kujiuzulu.

Hamisi alisema, “Kuna risiti feki alizochapisha na kugonga Mhuri wa Halmashauri kisiri, ambapo Wakulima waliopo kijijini mbigiri, walichangishwa Sh. 2,000/-, na Wakulima wa Mbigiri wanaoishi Morogoro Mjini walichangia Sh.5,000/-, lakini kwa masikitiko, fedha hizo zilitafunwa”.

Mbali ya fedha zenye risiti feki kutafunwa, Mwenyekiti Hamis wa Chadema, alidai sababu nyingine za kumng’oa Mwenyekiti wa CCM, Salim, ni pamoja na sintofahamu ya ziliko fedha za Ruzuku ya Kijiji Sh. Milioni 15/-, na Mifuko Saruji 50 za Mfuko wa Maendeleo wa Rais (TASAF), ambazo hazijulikani ziliko.


Aidha Hamis aliongeza kutoa madai kwamba, bado kuna sintofahamu kuhusu Shule ya Sekondari ya Mazoezi ya Mbigiri, ambayo imekuwa haifahamiki kama imesajiriwa au laa, kwa sababu tayari imetumia fedha nyingi kuikarabati, na wananchi wamechangia nguvu zao kwa kiwango kikubwa.

Awali, Mwenyekiti Salim alipohojiwa dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwake, alikanusha vikali, na kudai, kuhusu mifuko 50 ya Saruji, anatakiwa ahojiwe aliyekuwa mwenyekiti kabla yake, ili kujua waliitumiaje na aliyekuwa Mkandarasi wa Sekondari ya Magore, na kuhusu Sh. Mil. 15/-, alisema zilipopelekwa kijijini hapo, zilipokelewa zikiwa na Maagizo ya Wilaya ya Kilosa, ya nini zifanye.

Chadema Moro kumuunga mkono Abood


Lengo ni kutaka taarifa za fedha zinazohusu ujenzi wa kituo cha mabasi cha Msamvu

Morogoro. Mvutano wa uendelezaji ujenzi wa kituo cha mabasi cha Msamvu mjini hapa, umeingia hatua mpya baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutangaza maandamano kuunga mkono hatua za Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Abood kuhoji matumizi ya fedha za mradi huo. 

Mradi huo wa ujenzi wa stendi ya mabasi unaofanywa kwa ubia na Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF) Sh720 milioni zimeshatolewa kumlipa fidia aliyejenga ghorofa ndani ya eneo hilo.

Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Morogoro, James Joel alisema wanakusudia kufanya maandamano Aprili 14 .

Alisema uamuzi wa kufanya maandamano unatokana na Abood kufanya ziara ya kawaida kukagua mradi huo unaofanywa kwa ushirika na Manispaa ya Morogoro ambayo imeshindwa kutoa taarifa za matumizi hayo. 

Mwenyekiti huyo wa Chadema, alisema kuwa katika mradi huo inaonekana kuna harafu ya ufisadi miongoni mwa viongozi wa manispaa ndiyo maana wanakataa kuweka wazi taarifa za mradi huo. “Tunaomba polisi ituache, haya maandamano ni ya amani...tunataka maelezo ya hizi fedha kwa kuwa fedha ni za wananchi, wanakosa huduma muhimu kutokana na mradi huo,”

Alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, Abood alisema kinachotakiwa ni kuwekwa wazi suala la fedha za mradi huo.

Naibu Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwenendo wa Bunge na Halmashauri wa Chadema, Dk Albanie Marcossy alisema maandamano hayo ni mwendelezo wa operesheni iliyoanzishwa na Chadema ya kuelimisha jamii kuhusu matumizi mbalimbali ya fedha za Serikali.

Katibu wa Chadema, Wilaya ya Morogoro, Esther Taweta alisema chama hicho kipo kwa ajili ya kutetea masilahi ya wananchi.

Alisema fedha zilizotolewa kujenga mradi wa maendeleo hazijulikani zilipo.



Mwananchi

Wabunge 50 kutua ACT...........ni hatariiiiiiiiiiiiiiiiii

 
Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza na wahariri wa gazeti la Mwananchi alipotembelea makao makuu ya Mwananchi Communications Limited, yaliyopo Tabata Relini, Dar es Salaam jana.

Zitto ambaye alijivua ubunge wa Kigoma Kaskazini baada ya kufukuzwa uanachama wa Chadema, amebainisha kuwa wabunge hao, wakiwamo wa CCM na Chadema, ni miongoni mwa watu wanaokichangia fedha chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei, mwaka jana na kuzinduliwa mwezi uliopita.

Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe amesema zaidi ya wabunge 50 wa vyama mbalimbali vya siasa nchini watajiunga na chama hicho kipya na kugombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Zitto ambaye alijivua ubunge wa Kigoma Kaskazini baada ya kufukuzwa uanachama wa Chadema, amebainisha kuwa wabunge hao, wakiwamo wa CCM na Chadema, ni miongoni mwa watu wanaokichangia fedha chama hicho kilichopata usajili wa kudumu Mei, mwaka jana na kuzinduliwa mwezi uliopita.

Pia, amewatangazia vita wabunge wa majimbo manane ya Mkoa wa Kigoma, akijigamba kuwa ili waweze kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo ni lazima wakubali kujiunga na ACT kwa kuwa chama hicho kimejipanga kuyabeba majimbo yote. 

Akizungumza na waandishi wa Mwananchi katika ofisi za gazeti hili, Dar es Salaam jana, Zitto alisema ACT ni chama kilichojipanga na ndiyo maana haikuwa ajabu katika mkutano wake mkuu wa hivi karibuni kuhudhuriwa na wanachama zaidi ya 400 na kufanya uzinduzi wa aina yake, huku akisisitiza kuwa chama hicho kinaungwa mkono na watu wengi.

“Tuna wagombea ubunge wengi wakiwamo wabunge wa sasa ambao katika Uchaguzi Mkuu Oktoba hawatagombea kupitia vyama vyao vya sasa. Wapo ambao hawatakwenda hata katika kura za maoni za vyama vyao na wameshafanya uamuzi,” alisema.

Huku akizungumza kwa kujiamini, Zitto alisema wabunge hao ndiyo sababu ya chama hicho kuwa na uwezo wa kujiendesha na kufafanua kuwa ACT kinawakaribisha wabunge na makada wote kutoka vyama vya Chadema na CCM.

“Wale ambao wanabanwa CCM na kukosa uhuru wa kuhoji jambo lolote hiki (ACT) ndicho chama chao. Wale ambao wanaamini kuwa aina za siasa tulizotaka kuzifanya ndani ya Chadema tukashindwa kuzifanya na wanadhani ni siasa muhimu zinazotakiwa, wapo na sisi,” alisema.

Kuhusu Kigoma

“Nahitaji majimbo yote ya Kigoma kuchukuliwa na ACT bila kukosa hata moja na hili hata Serukamba (Mbunge wa Kigoma Mjini-CCM) analijua. Mwanasiasa anayetaka kuwa mbunge Kigoma lazima aje ACT,” alisema Zitto ambaye pia alirejea kauli yake kuwa atagombea ubunge katika jimbo jingine lakini siyo Kigoma Kaskazini. 

Kauli hiyo ya Zitto inawagusa wabunge wa sasa wa majimbo ya Kigoma ambao ni; Felix Mkosamali (Muhambwe), Moses Machali (Kasulu Mjini), Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) na David Kafulila (Kigoma Kusini), wote wa NCCR-Mageuzi na Peter Serukamba (Kigoma Mjini, Christopher Chiza (Buyungu) na Albert Obama (Manyovu) wa CCM.

Alipoulizwa iwapo wabunge hao wa majimbo ya mkoa huo ni miongoni mwa watu watakaohamia chama hicho alisema, “Sasa huo ni mtizamo wenu. Ukiwa mwanasiasa lazima uwe na msingi, nataka msingi uwe Kigoma.

Tutakutana tena kwenye chumba hiki (cha mikutano) baadaye mwezi Novemba ili mnisute kwa kauli yangu na hapo itakuwa baada ya matokeo kutoka. Nahitaji kushinda kila kitu.
Mwananchi

Lowassa: Natazamwa na CCM kila kona


Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara. 

Alisema hayo jana alipoulizwa kuhusu kauli ya Rais Jakaya Kikwete wiki iliyopita akiwa Marekani ambako alielezea mafanikio na changamoto alizokumbana nazo wakati wa uongozi wake wa miaka 10.

Dar es Salaam. Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa amesema anashindwa kujitokeza kuzungumzia au kufanya mambo yanayohusiana na urais kwa kuwa Kamati ya Maadili ya CCM inamfuatilia kwa karibu.

Alisema hayo jana alipoulizwa kuhusu kauli ya Rais Jakaya Kikwete wiki iliyopita akiwa Marekani ambako alielezea mafanikio na changamoto alizokumbana nazo wakati wa uongozi wake wa miaka 10. 

Kikwete alisema: “Wakati unaingia Ikulu unakuwa na shauku kubwa pamoja na furaha ya ushindi, lakini hakika urais ni kadhia kubwa. Ukipata fursa ya kuwa rais kwa awamu mbili kama mimi nadhani zinatosha kabisa. Nimefanya mengi kwa nchi yangu atakayekuja ataendeleza nilipoishia.”

Kauli ya Lowassa inakuja ikiwa ni siku chache baada ya makada wengine wanaotajwa kuwania urais kupitia CCM kueleza maoni yao juu ya kauli hiyo ya Rais.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba ameshalieleza gazeti hili kuwa kauli hiyo inampa hamasa kwa nia yake ya kutaka kuwania urais na kwamba alitangaza nia hiyo huku akifahamu kwa asilimia 100 uzito wa jambo hilo akisema kufahamu changamoto hizo ndiyo moja ya vitu vilivyomsukuma kuchukua uamuzi huo.

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye alisema: “Kama mtu ameamua kuwania nafasi hiyo ina maana anafahamu anachokitaka. Tunajua ziko changamoto na namna ya kukabiliana nazo, kwa hiyo hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi.”

Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla alisema: “Kauli kama hiyo haiwezi kumvunja mtu moyo, ari itabaki palepale tu kwa aliyetangaza nia. Aliyetangaza nia anataka kutoa utumishi wake kwa nchi yake kama mimi.”

Lowassa hajatangaza wazi nia hiyo zaidi ya kusema ameshawishika kuwania urais baada ya hivi karibuni, makundi mbalimbali kufika nyumbani kwake mjini Dodoma kumshawishi achukue fomu kuwania nafasi hiyo.

Miongoni mwa makundi yaliyojitokeza na kumshawishi pamoja na kumchangia fedha za kuchukua fomu ya kugombea urais ndani ya CCM ni pamoja na masheikh kutoka wilayani Bagamoyo, wachungaji wa makanisa ya Kipentekoste, wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na madereva bodaboda. 

Msimamo wake hadi jana

Akizungumza jana wakati wa kuaga mwili wa Mkurugenzi wa zamani wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Mohamed Mhita nyumbani kwa marehemu Oysterbay jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema: “Muda mwafaka ukifika nitatangaza nia na kuweka mikakati yangu wazi ili wananchi waijue. Kwa sasa siwezi kusema chochote kwa sababu ninatazamwa sana na chama. Ninachoweza kusema, siku nitakayotangaza nia, nitaeleza ni nini nitafanya kukabiliana na changamoto zote zilizopo Ikulu.

“Ninafahamu kuna changamoto nyingi, lakini siwezi kusema, subirini siku nitakapotangaza nia, nitaelezea ni kwa namna gani nitakabiliana na changamoto zilizopo katika ofisi hiyo nyeti nchini.”




Mwananchi

Bakora sita za Ukawa kwa CCM..........soma hapa


Wafusia wa Chama cha Mapinduzi wakiwa katika moja ya mikutano ya hadhara ya chama hicho jijini Dar es Salaam.

Vikwazo hivyo ni kuwapo kwa makundi ndani ya CCM yanayotokana na mitandao ya urais, hasira za wananchi juu ya mchakato wa Katiba Mpya, tuhuma za ufisadi ama kwa makada au Serikali yake, suala la Mahakama ya Kadhi, ahadi za Rais 2010 ambazo hazijatekelezeka na kuimarika kwa upinzani na muungano wake wa Ukawa. 

Dar es Salaam. Uhakika wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kutamba katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utategemea umahiri wake katika kukabiliana na vikwazo sita vinaonekana kuwa mwiba kwake ambavyo upinzani kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), unatarajiwa kuvitumia kama mtaji wake katika kampeni.

Vikwazo hivyo ni kuwapo kwa makundi ndani ya CCM yanayotokana na mitandao ya urais, hasira za wananchi juu ya mchakato wa Katiba Mpya, tuhuma za ufisadi ama kwa makada au Serikali yake, suala la Mahakama ya Kadhi, ahadi za Rais 2010 ambazo hazijatekelezeka na kuimarika kwa upinzani na muungano wake wa Ukawa.

Hata hivyo, baadhi ya makada wa chama hicho bado wanaona kuwa pamoja na vikwazo hivyo, chama hicho kitapenya katika uchaguzi huo na kuongoza tena Dola kwa kuwa kinao mtaji mkubwa wa wanachama na mtandao wake ni mpana kuliko chama chochote nchini.

Mgawanyiko na makundi

Kwa nyakati tofauti, viongozi wa CCM kupitia vikao vya ndani na mikutano ya hadhara, wamekuwa wakizungumzia jinsi ya kudhibiti mivutano ya makundi ya urais miongoni mwa wanachama wake, tatizo kubwa likiwa ni jinsi gani ya kuwaleta pamoja na kuponya makovu baada ya uteuzi.

Mathalani, tangu uchaguzi mkuu uliopita, viongozi wa CCM wamekuwa wakieleza mgawanyiko baada ya uteuzi kama sababu ya kuyakosa baadhi ya majimbo muhimu nchini na tatizo hilo linaweza kukikumba hata ngazi ya urais, kisipokuwa makini.

Makundi ya watia nia ya urais kwa sasa yamesambaa mikoani kimyakimya kutafuta uungwaji mkono na baadhi yake yamejijengea ushindani wa kihasama kati ya kundi moja na jingine hadi kutupiana maneno makali na tuhuma mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo linaweza kuhatarisha uimara wa chama na kukiathiri katika uchaguzi wa Oktoba.

Mchakato wa Katiba

Tangu ulipoanza mchakato huo hadi sintofahamu inayoendelea ya Kura ya Maoni, yametokea mambo mengi na kuzua hasira kwa baadhi ya Watanzania, hivyo kuwa miongoni mwa mambo yanayohofiwa kutumika kama bakora ya kuiadhibu CCM katika Uchaguzi Mkuu.

Hasira hiyo inatokana na jinsi wananchi walivyoipokea na kuiamini Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba na kuyakubali matokeo ya kazi yake lakini baadaye yakapinduliwa na Bunge la Katiba, kwa wingi wa kura za wajumbe wa CCM, ambazo hadi leo bado zinatia shaka.

Hata kitendo cha kushindikana kwa karata ya Serikali kuitisha Kura ya Maoni Aprili 30, ni kikwazo kingine kwa chama hicho, kwa kuwa hakuna namna nyingine ya kuonyesha kuungwa mkono na umma, ikiwa ni siku chache baada ya nguvu yake kuonekana kupungua katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
 
Ufisadi 
Mwananchi

Vigogo Rubada wasimamishwa


 
Waziri wa kilimo, chakula na ushirika  Steven Wassira

SERIKALI imewasimamisha kazi vigogo watatu wa Mamlaka ya Ustawishaji Bonde la Mto Rufiji (Rubada) kwa muda usiofahamika.

Vigogo hao wamesimamishwa kazi baada ya kutuhumiwa kwa ubadhilifu wa zaidi ya Sh bilioni 2.3.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira, aliwataja vigogo hao ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Aloyce Masanja, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji, Tabu Ndatulu na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala, Filozi Mayayi.

Alisema ubadhilifu huo umebainika baada ya tume iliyoundwa na wizara kwa kushirikiana na Hazina kufanya uchunguzi wa kina.

Wasira alisema viongozi hao wamekuwa wakijihusisha na masuala mbalimbali ya kiuongozi, jambo ambalo kamwe Serikali haiwezi kulivumilia.

Alisema amechukua uamuzi huo wa kinidhamu kwa kutumia mamlaka yake ya waziri mwenye dhamana.

Wasira alisema makosa mengine ya kijinai ameiachia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi.

Alisema vigogo hao walikuwa wakiwatoza fedha watu ambao walikuwa wanataka kuwekeza kwenye kilimo.

“Kibaya, hawa viongozi walikuwa wakiwatapeli wawekezaji kwenye sekta ya kilimo kwa kuwatoza fedha bila kuwaonyesha maeneo ya kulima jambo ambalo lilizua malalamiko makubwa,” alisema Wasira.

Alisema zaidi ya Sh bilioni 2.7 zilipokewa na maofisa hao kutoka kwa wawekezaji, lakini fedha zilizoonekana kwenye akaunti ni Sh milioni 714.6 wakati Sh bilioni 2.3 hazijulikani zilipo.

Wasira alisema tayari ameiandikia Bodi ya Wakurugenzi ya Rubada ianzishe mchakato wa kujaza nafasi hizo haraka iwezekanavyo ili kazi ziweze kuendelea kama kawaida.

“Maofisa hawa wakuu walikuwa wakijilipa masurufu na baadhi ya fedha zimegundulika kuwekwa kwenye akaunti zao binafsi badala ya ile ya Rubada.

“Fedha za wafanyakazi zaidi ya Sh milioni 58 walizokuwa wakikatwa kwa ajili ya kupelekwa katika Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ziliishia mifukoni mwao, taratibu za utoaji tenda zilikiukwa, wamefanya watakavyo,” alisema Wasira.

Alisema mfumo mzima wa utendaji wa mamlaka hiyo ulikuwa dhaifu na hakukuwapo na mgawanyo wa kazi, huku maofisa hao wakiidhinisha malipo na kutembea na fedha mifukoni.

Wasira alisema kazi hiyo ilipaswa kufanywa na mhasibu kama utaratibu wa Serikali unavyotaka.

2015-04-08

Mambo Sita Yaliyomshinda Rais Kikwete Katika Muda Wake ni Katiba Mpya, Mahakama ya Kadhi, Sheria ya Habari, kupambana na Ufisadi....

Rais Jakaya Kikwete alitoa ahadi lukuki kwa makundi mbalimbali ya jamii katika kipindi cha miaka 10 ya utawala wake kupitia kaulimbiu yake ya Maisha Bora kwa Kila Mtanzania, lakini anaondoka madarakani mwaka huu akiwa ameshindwa kutekeleza ahadi nyingi na zaidi ameacha manung’uniko na mgawanyiko.

Mwaka 2005, alipoingia madarakani aliahidi kuondoa uhasama wa kisiasa kati ya visiwa vya Unguja na Pemba, kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, kuwapatia wanahabari Sheria ya Habari, kupambana na ufisadi; na mwaka 2010 aliahidi kuwapa Waislamu Mahakama ya Kadhi na wananchi Katiba Mpya.

Mambo hayo sita yamekuwa mfupa mgumu kwa Rais Kikwete na anaondoka akiacha uhasama mkubwa wa kisiasa visiwani Zanzibar, wakulima na wafugaji wakihasimiana, ufisadi ukiotesha mizizi, vyombo vya habari kufungiwa, nchi ikipasuka kuhusu Katiba Mpya na Mahakama ya Kadhi.

Sheria ya Habari

Rais Kikwete alijigamba kuruhusu uhuru wa vyombo vya habari na Serikali yake ilianza kuandaa muswada mwaka 2007 lakini haukufikishwa bungeni. Machi 30, 2012 Kikwete alipokuwa mgeni rasmi katika utoaji Tuzo za Umahiri katika Uandishi (EJAT), aliahidi mambo mengi mazuri likiwamo la kuwasilishwa Muswada wa Sheria ya Kusimamia Vyombo vya Habari katika Bunge la Oktoba.

Kuthibitisha kwamba Rais Kikwete hamaanishi anachokisema, Julai 30, 2012 yaani miezi minne tangu awape matumaini wanahabari, Serikali yake kupitia Idara ya Habari (Maelezo), ililifungia gazeti la MwanaHalisi, kwa muda usiojulikana. Halafu Septemba 27, 2013 gazeti la Mtanzania lilifungiwa kwa muda wa siku 90 na Mwananchi kwa siku 14. Magazeti mengine yaliyowahi kufungiwa siku 90 ni Kulikoni (Januari 8, 2010) na MwanaHalisi (Oktoba 13, 2008).

Desemba 8, 2011 mwanasafu wa gazeti la Tanzania Daima, Samson Mwigamba; mhariri mtendaji wa gazeti hilo, Absalom Kibanda na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Mwananchi Communications Ltd iliyochapisha gazeti hilo walifikishwa kortini wakikabiliwa na mashtaka ya uchochezi.

Septemba 2, 2012 aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi alipigwa na kufariki dunia akiwa mikononi mwa polisi alipokuwa akiripoti mkutano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa. Januari 23, 2015 Serikali yake imeamua kupiga marufuku usambazwaji wa gazeti la The EastAfrican nchini.

Katiba Mpya

Ilani ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 haikuwa na ahadi ya Katiba Mpya, lakini Novemba 8, 2010 siku alipozindua Bunge la 10, Kikwete alizungumzia umuhimu wa kuipa uhai Katiba iliyopo na Februari 2011 katika sherehe za CCM alisema atawapa Watanzania Katiba Mpya.

Kwa kuwa wazo hilo halikutokana na CCM, Kikwete alipata shida kulinadi ndani ya vyombo vya chama na Serikali na hata walipokubali, wasaidizi wake walidai ni marekebisho yeye akisema kuhuisha. Serikali ikatengeneza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, akaunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji mstaafu, Joseph Warioba ambayo ilifanya kazi ya kukusanya maoni na kutengeneza Rasimu ya Katiba. Mwaka 2014 akaunda Bunge Maalumu la Katiba (BMK) ambalo liliandika Katiba Inayopendekezwa.
Ukosoaji mkubwa aliofanya Rais Kikwete alipozindua BMK, uliwagawa wabunge katika makundi mawili ya kudumu; wanachama wa CCM upande mmoja na wapinzani upande wa pili. Pia, Tume ya Warioba ilipingana na BMK lililoongozwa na Samuel Sitta.

Aprili 16, wapinzani chini ya umoja wao Ukawa walisusia BMK, likawa pigo la kwanza. Pigo la pili na la mwisho ni Januari 23, 2015 Ukawa walipotangaza kususia Kura ya Maoni iliyopangwa Aprili 30. Kutokana na misuguano hiyo, na kwa kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi haikuwa imepewa fedha za kutosha zikiwamo za kununulia mashine za BVR kwa ajili ya kuandikisha wapigakura, Aprili 2, 2015 Kura ya Maoni ikafutwa hadi itakapotangazwa tena.

Mahakama ya Kadhi

Mwaka 2010, katika mazingira tata CCM iliingiza ahadi ya Mahakama ya Kadhi kwenye Ilani ya Uchaguzi. Lakini Serikali haikufanya juhudi kubwa kutengeneza mazingira ya kukubalika kwa mahakama hiyo; kwanza, kwa Waislamu wenyewe; pili, kwa Wakristo.

Kosa namba moja. Agosti 30, 2011 alipokuwa mgeni rasmi katika Baraza la Idi katika msikiti wa Gadaffi, Dodoma, Rais Kikwete aliwaambia Waislamu kwamba amezungumza na maaskofu na wamemwambia kuwa hawana shida na Mahakama ya Kadhi isipokuwa wanataka iundwe na kuhudumiwa na Waislamu wenyewe. Waislamu walilalamika mambo yao kujadiliwa kwanza na Wakristo ndipo waelezwe wao.

Kosa namba mbili. Serikali imekuwa ikikutana na uwakilishi mpana wa maaskofu kutoka madhehebu yote kupata maoni yao lakini imekuwa ikikutana na uongozi wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) ambalo halikubaliwi na Waislamu wote.

Kosa namba tatu. Dalili zote zikionyesha hakuna uwezekano wa kukubalika kwa Mahakama ya Kadhi, Serikali ilitoa ahadi nzito ndani ya BMK na Waislamu waliporidhia, hazikuwepo juhudi za kuandaa semina za kuelimisha wadau kuhusu muundo na uendeshwaji wake hali iliyosababisha hata baadhi ya Waislamu kuikataa kwamba siyo kati ya nguzo tano za Uislamu. Vilevile, lilikuwepo shinikizo kutoka kwa maaskofu na hasa ulivyoligawa Taifa mapande mawili.

Mgogoro Zanzibar

Moja ya ahadi nzito iliyofurahiwa na Watanzania ni ile ya kumaliza uhasama wa kisiasa Zanzibar kati ya wanachama wa CCM wengi wao wakiwa Unguja na wenzao wa Chama cha Wananchi (CUF) ngome yao ikiwa Pemba. Ahadi hiyo iliianza kutekelezwa baada ya kuanzishwa mazungumzo baina ya viongozi wa CCM na CUF na hatimaye kufikia maridhiano na Katiba ikafanyiwa marekebisho kuruhusu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuongozwa kwa mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK). 

Pamoja na mafanikio hayo, uhasama wa kisiasa umerejea; CCM wakionekana kuwa vinara wa siasa za uhasama; wanawavizia na kuwapiga wafuasi wa CUF. Katika mikutano yao huhubiri ubaguzi kwa kuzingatia asili ya watu kwamba Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu wanatajwa kuwa ni vibaraka wenye lengo la kurudisha utawala Kisultani. Wanadai kwamba vibaraka hao wanataka kurudisha utawala wa Sultani aliyepinduliwa mwaka 1964, Jamshid bin Abdullah Al Said, kizazi cha masultani kutoka Oman kilichotawala Zanzibar kuanzia mwaka 1832 hadi mwaka 1964.

Huu ni unafiki, ukweli ni kwamba Jamshid aliyetawala Zanzibar kuanzia Julai Mosi, 1963, baada ya kupinduliwa Januri 12, 1964 alikimbilia Uingereza. Salmin Amour, Rais wa awamu ya tano wa SMZ alitangaza kumpa uhuru Sultani huyo anayeishi Portsmouth, kurejea Zanzibar kama raia mwingine. Hajarudi.


Wakulima, wafugaji
Jambo jingine kubwa aliloahidi kushughulikia katika hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la Tisa Desemba 31, 2005 ni kulinda mazingira kwa kuhakikisha wakulima wanaachana na kilimo cha kuhamahama na wafugaji aliodai wanatembea umbali mrefu kusaka malisho wakiwa wamekonda na mifugo imekonda, kuwapa mbinu za ufugaji ili sekta ya ufugaji iwe ya kisasa.

Baada ya kuunda Serikali alitembelea Wizara ya Maendeleo ya Mifugo, aliwaagiza watendaji: kuongeza mchango wa sekta ya mifugo katika pato la Taifa; kudhibiti uhamishaji holela wa mifugo; kuimarisha huduma za ugani; kufufua ranchi zilizopo na kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa; na kutoka katika uchungaji wa kuhamahama na kwenda katika ufugaji wa kisasa na wa kibiashara.

Vilevile, aliwaagiza kutafuta masoko ya nje ya kuuza mifugo na mazao yake; na kufikisha madawa na huduma za mifugo kwa wafugaji. Lakini miongoni mwa picha zilizojaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii kuanzia mwaka 2006 ni za maiti ya wakulima na wafugaji katika maeneo tofauti nchini.

Baadhi zikionyesha watu waliokatwa koo, waliopasuliwa vichwa na waliopigwa mishale na mikuki; nyingine zikionyesha nyumba au maboma yalivyochomwa moto, mifugo kuuawa. Hasira na uhasama vimetanda kila mahali.

Katika kipindi cha uongozi wake, imeshuhudiwa migogoro mingi ya ardhi kati ya masikini na matajiri, wakulima wazawa na wawekezaji na mbaya zaidi kati ya wakulima na wafugaji ambao wamechinjana Mbarali, Kilosa, Kiteto na kwingineko. Rais Kikwete anaondoka huku hali ikiwa mbaya kuliko alivyoikuta.

Vita ya ufisadi

Ahadi nyingine ya Rais Kikwete kwa Watanzania aliyoitoa katika hotuba yake ya Desemba 31, 2005 ni kuanzishwa kwa mapambano dhidi ya rushwa kubwa kubwa kwa vitendo na siyo lazima ushahidi uwepo kwa asilimia 100.

Alisema: “hata ukihisiwa umekula rushwa tutahakikisha tunachunguza na kushughulikia…” Lakini licha ya Taasisi ya Makosa Makubwa ya Jinai ya Uingereza (SFO) kutaja waliokula rushwa kupitia ununuzi wa rada ya kuongozea ndege, Serikali ilikataa kuwashughulikia.

Mafisadi wengine ambao hawakushughulikiwa na Serikali yake ni walionufaika kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa), walitoengeneza dili kupitia kampuni ya kufua umeme wa dharura ya Richmond/Dowans, walioiuzia vifaa hospitali ya Muhimbili kwa bei mbaya, waliochangisha fedha za kula tu baada ya kupitisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini (2012) na sasa waliotengeneza mazingira ya kuchotwa Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, Serikali imewanasa walimu na mahakimu na kuwafungulia mashtaka kwa madai ya kuchukua rushwa ndogondogo.

2015-04-07

Muhamasishaji wa CHADEMA na mtunzi wa nyimbo ya Slaa anaweza ahamia chama cha ACT Wazalendo


Muhamasishaji wa CHADEMA mtunzi wa nyimbo maarufu ya SLAA ANAWEZA na nyingine ndugu MASHAKA PEPE almaarufu PEPE ameachana rasmi na CHADEMA na kujiunga na Chama cha wazalendo ACT WAZALENDO Leo.

amekabidhiwa kadi na mwenyekiti wa Taifa ndugu Anna Mghwira sambamba na viongozi Wengine. 



 

Chama Cha ACT Wazalendo Kimejipanga kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwezi Agosti~2015

Baada ya chama hicho kuzinduliwa rasmi, nguvu yake imeelekezwa katika kujijenga na kujiimarisha zaidi,” Mwenyekiti wa ACT-Tanzania, Anna Mghwira

Dar es Salaam. Chama cha ACT- Tanzania, kimesema hakina muda wa kufanya siasa za chuki na malumbamo dhidi ya vyama vingine vya siasa, badala yake kinajipanga vizuri na kuandaa mazingira ya kushiriki katika uchaguzi mkuu ujao.

Mwenyekiti wa chama hicho Anna Mghwira, aliliambia gazeti hili mwishoni mwa juma kuwa, baada ya chama hicho kuzinduliwa rasmi Machi 29 mwaka huu, nguvu yake sasa imeelekezwa katika kujijenga na kujiimarisha.

Alisema katika kujiimarisha, chama hicho kinatafuta wanachama, kwa kuwa kinatambua kuwa ni mtaji wa kujihakikishia ushindi katika uchaguzi mkuu, pamoja na kuandaa wagombea kwa kuangalia uwezo wao kadri watakavyojitokeza.

“Mimi mwenyewe ni miongoni mwa wagombea ubunge, nitagombea Jimbo la Singida mjini na naamini kwamba nitaweza kupata nafasi hiyo kwa sababu ninafahamika kule ni nyumbani nilikozaliwa .

Nimesoma huko, nimekulia huko na najua changamoto zinazotukabili wakazi wa kwetu na jinsi nitakavyoshiriki kukabiliana nazo nikiwa mbunge,”

Mghwira alieleza kuwa chama hicho kinajiimarisha, huku kikitambua kuwa kina wajibu wa kuendeleza ushirikiano na vyama vingine vya siasa, badala ya kujitenga na kuendesha shughuli zake kama kisiwa.

Mwenyekiti huyo, alitolea mfano siku ya uzunduzi wa chama hicho akisema kuwa kulikuwa na watu wengi kutoka vyama mbalimbali ambao walitaka kurudisha kadi za vyama hivyo hadharani na kuchukua kadi za ACT, lakini walisitisha shughuli hiyo kuepuka uhasama.

“Kuwa vyama tofauti haina maana kwamba tuwe maadui, kulikuwa na wanachama wapya siku ya uzinduzi (wa ACT) walitaka kuonyesha hadharani wanavyorudisha kadi za vyama vyao vya awali hatukuwapa nafasi hiyo, kwa sababu hatuoni kuwa hilo ni jambo la kuvutia kwetu,” alisema.

Kwa mujibu wa Mghwira siku hiyo walipokea wanachma wapya 2,000 na bado wanaendelea kupokea wanachama wengine kutoka vyama mbalimbali vya siasa lakini kwa siri.

Ingawa Mghwira hakutaja watu, asilimia kubwa ya viongozi wa kitaifa wa chama hicho, akiwamo Zitto Kabwe ambaye sasa ni Kiongozi Mkuu wa chama hicho na Katibu Mkuu Samson Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo, wamejiunga na chama hicho baada ya kufukuzwa na vyama vyao.

“Pia katika kuonyesha nia yetu ya kuhitaji ushirikiano mwema wa kisiasa tuliwaalika viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani, ikiwemo Chadema na CUF,” alisema.

Alisisitiza kuwa Profesa Ibrahimu Lipumba ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) ni miongoni mwa wasomi na viongozi wa vyama vingine vya siasa walioalikwa kutoa mada katika uzinduzi wa chama hicho, lakini alipata udhuru hivyo hakufika.

“Hata hivyo tulifarijika kuona shughuli yetu ya uzinduzi wa chama ikifanyika vizuri na kwa amani,” alisema.

Chama Kipya Cha Zitto Kabwe, ACT-Tanzania Chapania Kuchukua Majimbo Manne Ya Uchaguzi Mwaka Huu


Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT), kimesema kinatarajia kunyakuwa majimbo manne ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.

Kimetaja majimbo hayo kuwa ni Ubungo, ambalo linaongozwa na John Mnyika (Chadema), Kawe linaloshikiliwa na Halima Mdee (Chadema), Segerea ambalo Mbunge wake ni Makongoro Mahanga (CCM) na Kahama la James Lembeli (CCM).

Kiongozi Mkuu wa Chama hicho, Zitto Kabwe, alisema hayo katika kipindi cha Hot Mix kinachorushwa na kituo cha EATV.

Zitto aliendeleza msimamo wake wa kutogombea ubunge kwenye jimbo lake la awali la Kigoma Kaskazini.

“Nina maombi jimbo la Kahama, Kawe, Ubungo na Segerea lakini kwa kuwa ACT kinaongozwa kizalendo, tutaweka utaratibu mzuri wa kuweka wagombea kila eneo, binafsi kwa sasa siwezi kusema wapi nitagombea,” alisema.

Alipoulizwa ni eneo gani kati ya hayo aliyoyataja huduma yake inahitajika, alijibu kwa kifupi kuwa, nchi nzima ina muhitaji.

“Kabla ya kampeni kuanza wagombea wakirudisha fomu ndipo mtajua Zitto anagombea jimbo gani, lakini lazima niongozwe na chama nikagombee wapi , wanaweza kusema Zitto kagombee jimbo A,” alisema.

Aliongeza kuwa, ACT kinahitaji kujipanga kuingia kwenye mapambano ya kufyeka msitu wa siasa kwa kuwa ndani yake kuna vyama zaidi 22 na vingine vikiwa na uzoefu mkubwa kutokana na kudumu zaidi ya miaka 23.

Alisema kazi kubwa walionayo ni kukijenga chama ili kiweze kulirudisha taifa kwenye misingi ya waasisi waliyoiacha.

Aliongeza kuwa, baadhi ya watu wanamuona kama anaanza upya kwa sababu wapo wachache waliwahi kujaribu na kuishia njiani.

Alipoulizwa kuhusu wachambuzi wa siasa wanavyomchukulia hivi sasa, Zitto alisema wapo wenye mtazamo hasi na wengine chanya.

Alisema kwa wale wanaomchukulia kwa mtazamo hasi anaendelea kuwafundisha na kuwaonyesha kwamba muono wao ni tofauti wakati wale wa chanya anaendelea kuwasikiliza ili kupata muongozo zaidi kutoka kwao.

“Tukumbuke hii nchi watu wamezoea kuchukia mabadiliko angalia kwenye sanaa wakimuona Diamond amefanikiwa waanza kutoa maneno ambayo siyo, watu wanachukia mabadiliko,” alisema.

Kuhusu kuitwa msaliti ndani ya Chadema kwa madai kuwa baada ya kuikosesha Chadema jimbo kule Katavi, alisema jambo hilo siyo la kweli na kwamba amekitumikia chama hicho nusu ya maisha yake na alichokifanya kinafahamika kwa wanachama na viongozi. 


“Ambacho sikufanya mimi ni binadamu sipo sawa kwa kila kitu hakuna binadamu ambaye hana makosa lakini yapo mema ambayo nimefanya lakini sasa nimeyakunja na kuyaweka pembeni na tumechora mstari na kuanzisha chama cha siasa cha wazalendo,” alisema.

Kuhusu kurasa zake kwenye mitandao ya kijaamii kuwa na maoni hasi, Zitto alisema kila mtu ana mawazo yake na hawezi kuyabadisha.

“Wito wangu ni kwa watu ambao ni waoga wa kuchukua maamuzi, waweke akiba ya maneno kwa sababu ACT ni sawa na moto wa pumba ambao ukiwaka juu unadhani hakuna moto lakini ukiweka mguu kuna moto mkali sana,” alisema.

Wanachokitaka UKAWA Kabla Ya Uchaguzi Mkuu Wa Octoba Mwaka Huu.......soma hapa


Uamuzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa umewafungulia viongozi wa Ukawa kuishinikiza Serikali kuiboresha Katiba ya sasa katika maeneo manne ili kuondoa mvutano katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.

Mambo manne yanayodaiwa na Ukawa ni:

  1. Ushindi wa urais kuamuliwa kwa asilimia zaidi ya 50.  
  2. Mgombea binafsi katika nafasi za udiwani, ubunge na urais.
  3. Tume huru ya uchaguzi.
  4. Trais kupingwa mahakamani.
Mwenyekiti mwenza wa umoja huo, James Mbatia amesema maboresho yaliyofanyika chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ni ya lazima ili kufanikisha uchaguzi huo kabla ya kupitishwa kwa Katiba Mpya na kuondoa uwezekano wa vurugu.

Katika kikao hicho, Mbatia alisema walitiliana saini kuwa iwapo uchaguzi wa mwaka huu utafanyika kwa kutumia Katiba ya 1977, Bunge lingekutana Novemba mwaka jana kufanya marekebisho hayo ya 15 ya Katiba na endapo hilo lingeshindikana, basi lingekutana Februari, jambo ambalo pia halikufanyika.

Utekelezaji wa masuala hayo utawezekana iwapo Serikali itawasilisha marekebisho hayo bungeni ili yajadiliwe kwa dharura katika mkutano ujao wa Bajeti wa mwisho wa Bunge la Kumi, kwa kuwa uwezekano wa kupata Katiba Mpya kabla ya uchaguzi ni kama haupo.

Alipoulizwa iwapo jambo hilo linawezekana katika Mkutano wa Bajeti, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Ndiyo inawezekana. Serikali inaweza kuwasilisha jambo hili kwa dharura na litajadiliwa na Kamati ya Uongozi, kama ikiona linafaa litapelekwa bungeni kujadiliwa.”

Katika hilo Mbatia alisema: “Bado kuna nafasi ya Bunge kufanya marekebisho. Hili linatakiwa kufanyika kama ambavyo tulikubaliana na Rais kupitia TCD.”

Alisema ushauri wa TCD kwamba mchakato wa Kura ya Maoni uahirishwe hadi mwakani umepuuzwa na matokeo yake yameonekana wazi na kwa msingi huo, suala la kurekebisha maeneo hayo manne, si la kupuuza hata kidogo.


“Hili lisipofanyika utaibuka mgogoro mkubwa. Tatizo la Serikali yetu ni kutotaka kutekeleza mambo yanayoonekana wazi kuwa na mkanganyiko, ndiyo sababu ya kukithiri kwa migogoro ya wakulima, wafugaji, wafanyakazi na mingine mingi,” alisema Mbatia.

Dk Slaa akata tamaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema endapo Serikali itashindwa kutekeleza makubaliano hayo, vyama vya upinzani havina budi kuingia katika mapambano kwa katiba hiyohiyo.

“Kama hatumwelewi Rais Kikwete katika suala hili, basi hatuwezi kumwelewa tena. Sioni juhudi zozote za Serikali kubadili maeneo haya. Tulikubaliana naye mambo mengi lakini yote ameshindwa kuyatekeleza, hata hili pia hawezi kulitekeleza,” alisema Dk Slaa.

Katibu mkuu huyo wa Chadema alisema umefika wakati wa vyama vya upinzani kupambana hivyohivyo licha ya kuwapo tume ya uchaguzi isiyo huru.

“Nimeshinda ubunge Karatu vipindi vitatu na tume ikiwa ni hiihii. Wapinzani tuna wabunge zaidi ya 100, nadhani tupambane tu,” alisema.

Alisema umefikia wakati wa kuing’oa CCM kwa kutumia Katiba mbovu (iliyopo sasa) na kinachotakiwa kufanywa na vyama vya upinzani ni kujipanga kuanzia vijijini hadi mijini ili kuzoa kura zote.

“Tumeshinda Kawe, Ubungo, Mbeya Mjini na hata Nyamagana. Tuache kulialia sasa, twende katika mapambano. Kwanza Bunge lijalo ni la Bajeti na kwa vyovyote vile mabadiliko tunayoyataka hayawezi kufanyika,” alisema.

Kiongozi Mkuu wa chama cha ACT-Tanzania, Zitto Kabwe alisema kinachotakiwa kufanywa sasa ni Baraza la Vyama vya Siasa kuitisha mkutano wa vyama vyote ili kukubaliana mambo ya kuboresha katika Katiba ya sasa.


“Jambo la pili ni Rais kuitisha Bunge kabla ya kuanza kwa Bunge la Bajeti kujadili mabadiliko hayo na kuyapitisha ili kuufanya uchaguzi mkuu uwe wa haki na huru,” alisema Zitto

Ukawa wataka Maalim Seif awe makamu

  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimependekeza kwamba Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Shariff Hamad, anapaswa kuwa mgombea mwenza wa Rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, Raia Mwema linafahamu.

Hata hivyo, pendekezo hilo limekataliwa na chama anachotoka Maalim Seif, yaani Chama cha Wananchi (CUF), kwa maelezo kwamba muda wa kujadili mambo hayo haujafika bado.

Gazeti hili linafahamu pia kwamba pendekezo hilo la Chadema liliwasilishwa kwanza na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kwenye kikao maalumu cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kilichofanyika Zanzibar mwishoni mwa wiki iliyopita.

Viongozi wakuu wa Ukawa kutoka vyama vya CUF, Chadema, NCCR Mageuzi na National League for Democracy (NLD), walikutana mjini hapa kwa ajili ya kuangalia namna ya umoja huo utakavyosimamisha wagombea katika uchaguzi huu.

“Mtu wa kwanza kutoa pendekezo hilo la Maalim Seif kuwania Umakamu wa Rais wa Muungano alikuwa ni Mbowe na baadaye Makamu Mwenyekiti, Profesa Abdallah Safari, naye aligusia suala hilo.

“ Hata hivyo, majadiliano hayo hayakwenda mbali sana kwa sababu CUF walisema muda wa kujadili suala hilo haujafika kwa vile Ukawa bado hawajakubaliana kila kitu kuhusu majimbo ya ubunge na hivyo suala la Urais linaweza kusubiri,” kilisema chanzo cha gazeti hili kilichozungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kwa maelezo kwamba si msemaji rasmi wa umoja huo.

Mmoja wa viongozi wa Ukawa aliyekuwa Zanzibar wakati wa mkutano huo, alisema suala hilo linaweza kuwa gumu kukubalika na CUF kwa sababu mbalimbali za kisiasa na kiuchumi.

“Kisiasa, kama CUF itakubali Chadema ndiyo itoe mgombea Urais na yenyewe itoe mgombea mwenza maana yake itakuwa inajiua. Labda nikwambie kwanini. Kwanza, kama mtu mwenyewe ni Maalim Seif, itabidi atoke CUF na kuhamia Chadema.

“Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa sheria za nchi, mgombea urais na yule mwenza ni lazima watoke katika chama kimoja. Sasa kweli Maalim Seif ahame CUF? Hiyo inaingia akilini kweli? Hapo kuna ugumu. Kwa kifupi naweza kusema hilo haliwezekani ng’o.
 

“Lakini pia usisahau, chama kitakachokuwa na mgombea urais ndicho kitakachozunguka nchi nzima kuomba kura na ndicho kitakachoonekana. Sasa kwa minajili hiyo, kama CUF haitakuwa na mgombea urais, maana yake kisiasa itakuwa inajiua yenyewe.

“ Kwenye uchumi, kuna hasara yake pia. Ruzuku ya vyama hutolewa kwa kuzingatia wingi wa kura za urais na zile za ubunge. Hata wingi wa wabunge wa viti maalumu pia unategemea wingi wa kura hizo. Ukiacha kuwania urais, maana yake unapunguza kura zako. Utapata ruzuku kidogo na itasumbua kichama.

“Tatizo ninaloliona kwa Chadema ni kwamba, nao wamekuwa kama CCM siku hizi. Wanataka kila jimbo wapewe. Ukiona mgawanyo wa majimbo utaona wao ndiyo wanaongoza. Na bado wanautaka urais. Sasa hapo unataraji nini?” alisema mmoja wa viongozi wa Ukawa aliye karibu na duru za mkutano huo.

Kama Maalim Seif angekubaliana na wazo hilo la Chadema, maana yake ni kwamba angelazimika kujitoa kuwania urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu; ambayo ingekuwa ni mara ya kwanza kwake katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Baada ya CUF kukataa kujadili suala hilo ambalo linadaiwa kutokuwapo kwenye ajenda za kikao hicho na kwamba ‘lilichomekewa tu’, wajumbe waliendelea na kikao hicho ambacho hatimaye kilifikia mwafaka wa namna mgawanyo wa majimbo ya ubunge utakavyokuwa katika uchaguzi wa mwaka huu.

Tayari Ukawa imeeleza mafanikio ya kikao hicho kwa kuweza kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa umoja huo katika majimbo yote nchini isipokuwa 30 tu, sita ya mkoa wa Dar es Salaam, ingawa nayo yanatafutiwa ufumbuzi.

Viongozi wakuu wa Ukawa waliohudhuria mkutano huo wa Zanzibar ni wenyeviti wa vyama hivyo, Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR Mageuzi), Emmanuel Makaidi (NLD) na Mbowe.

Uwezekano wa Ukawa kuingia kwenye Uchaguzi Mkuu wakiwa pamoja unategemea zaidi na namna watakavyoweza kukubaliana katika ngazi ya majimbo na urais kabla ya kuingia kwenye uchaguzi.

2015-03-31

Marafiki wa Lowassa waja na staili mpya



Daniel Mjema na Rehema Matowo, Mwananchi


Moshi. Mbunge wa Moshi Vijijini na Mjumbe wa Nec ya CCM, Dk Cyrill Chami, amewaomba walimu zaidi ya 2,700 wamuombee Waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa, ili ‘ndoto’ yake iweze kutimia.


Wakati Dk. Chami akiwaomba walimu hao, mtandao wa marafiki wa Lowassa Kanda ya Kaskazini, juzi walikuja na staili mpya ya kumshawishi Mbunge huyo wa Monduli agombee nafasi ya Urais.


Staili hiyo mpya imekuja wakati CCM ikiwa imempiga ‘stopu’ kuendelea na utaratibu wake wa kupokea makundi ya watu wanaomshawishi kugombea urais na yeye (Lowassa) kuridhia na kuwaomba wananchi wasubiri maelekezo ya CCM.


Marafiki hao ambao ni wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Kilimanjaro, walikwenda kitengo cha damu salama Kanda ya Kaskazini kuchangia damu kama njia ya kutambua na kuenzi upendo wa Lowassa.


Tukio hilo la wanafunzi hao kwenda katika kitengo hicho, kilitanguliwa na tukio la mkutano mkuu wa Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos) ya Walimu Moshi Vijijini kufanya mkutano wao mkuu. Katika mkutano huo, Dk Chami aliyekuwa mgeni rasmi, aliwaambia amekwenda pale akiwa na salamu kutoka kwa Lowassa kwamba anawapenda sana walimu. “Anasema anawapenda na anawakumbuka sana na anawaomba mmuombee ili ndoto yake na ile safari yake (bila kuitaja) itimie,” alisema Dk Chami na walimu hao kulipuka kwa vigelegele.


Katika tukio la uchangiaji wa damu, wanafunzi zaidi ya 100 wa vyuo vikuu mkoani Kilimanjaro, walitumia tukio hilo kumuunga mkono Lowassa wakimsihi atangaze nia ya kuwania Urais 2015. Mratibu wa marafiki wa Lowassa, Noel Nnko, alisema wanafunzi hao wameamua kuchangia damu kumuunga mkono kada huyo kwa vile wao hawana uwezo wa kutoa fedha za kuchangia fom

Zitto aichokoza Chadema na kuwapa somo wanachama wake

KIONGOZI Mkuu wa Chama cha ACT – Wazalendo, Kabwe Zitto ameahidi chama chake kuendesha shughuli zake kwa uwazi, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku viongozi kufanya biashara na chama hicho, jambo ambalo limekuwa likidaiwa kufanyika ndani ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambako aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu.
Ndani ya Chadema, mara kadhaa imekuwa ikidaiwa kwamba Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, amekuwa akifanya biashara na chama chake.

Akizungumza wakati wa hotuba yake ya uzinduzi wa ACT-Wazalendo uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Zitto, bila kutaja chama wala jina la mwanasiasa yeyote, alisema chama chake kinapozungumzia wananchi kurejesha taifa mikononi mwao ieleweke kwamba wanazungumzia uwajibikaji.

“Chama cha ACT Wazalendo kimeelekeza kikanuni kwamba kila kiongozi wa chama lazima atangaze mali zake na madeni yake. Kila kiongozi lazima aweke wazi maslahi yake ya kibiashara na mengineyo wazi ili kila anapotenda au kusema jambo wananchi wajue maslahi aliyonayo au la katika suala husika.

“Viongozi wote wa kitaifa wa ACT Wazalendo wamefanya hivyo na tutaweka saini zetu mbele yenu kama mashahidi. Naomba Mwanasheria wetu aje hapa tutekeleze matakwa haya ya kikanuni.

“Fomu hizi zitakuwa kwenye tovuti ya chama ndani ya muda mfupi ujao ili kila mtanzaina aone. Kila Kiongozi wa Chama ambaye miiko ya uongozi inamtaja anapaswa kuwa amejaza fomu hizi na kuziwasilisha kwa Katibu wa Kamati ya Uadilifu katika ifikapo tarehe 30 Juni 2015.

“Tunapopinga viongozi wa umma kufanya biashara na serikali na hivyo kuwa na mgongano wa kimaslahi na kushamiri kwa ufisadi, hivyo hivyo tunapinga viongozi wa chama chetu kufanya biashara na chama. Ni marufuku serikali kugeuzwa kuwa genge la watu wachache wanaopora rasilimali za umma. Uadilifu tunaoutaka serikalini ni lazima uanzie kwetu tunaohubiri.

“Tutafanya haya kwa kubadilisha siasa zetu kuelekea kwenye masuala yanayowahusu wananchi; wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara ndogo ndogo, vijana, wanawake na wazee wetu.

“Tunataka kurejesha nchi yetu Tanzania kwa kujenga uchumi wa wote. Tunaporejea kwenye Azimio, hatusemi tunakwenda kutaifisha kila kitu na Serikali kuendesha shughuli zote za kiuchumi. Tunaheshimu na kuthamini sekta binafsi na mchango wake katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo.

“Tunamaanisha kuwa ni lazima Dola isimamie uchumi. Sio kazi ya Serikali kufanya biashara. Lakini tunamaanisha kuwa ni lazima kurekebisha baadhi ya makosa yaliyofanyika kwenye ubinafsishaji na hususan ubinafsishaji holela uliofanyika kwenye sekta ya Kilimo na kupora ardhi ya wananchi wetu na kuwageuza kuwa manamba kwenye ardhi yao wenyewe. Tunataka kutomokeza ukwepaji kodi,” alisema Zitto.

2015-03-30

Hotuba ya Zitto Kabwe Wakati wa Uzinduzi wa Chama Kipya Cha ACT wazalendo


Watanzania wenzangu, wageni waalikwa
Nawashukuru kwa kuwa pamoja nasi siku hii ya kihistoria.

Karibu Miaka 54 iliyopita tulipopata uhuru, Muasisi na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa kijana mwenye umri wa miaka 39, mwenye matumaini makubwa na taifa jipya na alikuwa na ndoto!

Ndoto yake ilikuwa imejikita katika kuhakikisha taifa letu litakuwa taifa lisilo na umaskini, dhiki, ufukara; taifa lisilo na tofauti kubwa kati ya maskini na tajiri; taifa lenye usawa, haki na maendeleo, ambapo watoto wote wanasoma shule bila kujali kipato cha mzazi; taifa ambalo wananchi wake wanamiliki uchumi wao.

Ndoto hii aliiamini kwa dhati na wananchi wote walikubali na kuota nae ndoto hii. Alilisimamia kwa maneno na vitendo kupitia Azimio la Arusha, sera zake na uongozi wake wa kizalendo. Mpaka mauti ilipomkuta aliamini katika misingi hii aliyojitahidi kuturithisha. Lakini miaka 16 baada ya kifo chake, ndoto yake imeyeyuka!

Tulilonalo ni jinamizi alilolihofu Nyerere.

Leo hii:
Watanzania wachache wameondoka katika unyonge na dhiki.
Watanzania wengi bado wapo katika hali ya dhiki.
Watanzania wachache wameshikilia uchumi: Warasimu, Wanasiasa na Matajiri wachache wenye mitaji.
Watanzania wengi bado kama Mwalimu Nyerere alivyosema “wananyonywa kiasi cha kutosha; wanapuuzwa kiasi cha kutosha”.

Ndoto ya Mwalimu Nyerere bado haijawafikia wananchi.
Sasa ndio wakati wa mabadiliko ya kimapinduzi.
Sasa ndio wakati wa kujenga Uchumi shirikishi ambao utaruhusu kila mwananchi kupata fursa ya kuboresha maisha yake;
Sasa ndio wakati dola imara ipate nafasi ya kusimamia uchumi;
Sasa ndio wakati kwa wananchi kuwa na uhuru wa kweli wa mawazo, fikra, kushirikiana, kuabudu;
Sasa ndio wakati wananchi kuwa na nguvu ya kuwawajibisha viongozi wao;
Sasa ndio wakati wetu watanzania kujirithisha upya nchi yetu!

Huu ndio wakati wa kubomoa uchumi wa kinyonyaji na kifisadi na kujenga uchumi wa wananchi. Haya ndio mabadiliko ya kimapinduzi tunayoyataka. Hii ndiyo ilikuwa ndoto ya Mwalimu Nyerere, na muda umefika wananchi turejeshe nchi mikononi mwetu!

Haya yamekuwa mawazo yangu kwa muda mrefu kwa sababu mimi ni zao la ndoto ya Mwalimu Nyerere. Nililelewa na mama yangu mzazi pekee mwenye ulemavu; nimeanza kusoma shule ya msingi nikiwa naenda peku. Lakini kutokana na kufaulu mitihani vizuri, sikuhitaji kuwa tajiri kusoma mpaka chuo kikuu.

Leo hii kutokana na elimu bora niliyoipata bure, nimesafiri na kufika katika nchi zaidi ya 70; nikiwa kama kiongozi nimekutana na kubadilishana mawazo na watu muhimu duniani kama vile wakuu wa nchi. Sio mimi peke yangu bali tupo maelfu tuliofaidika na mfumo huu.


Lakini muhimu kupita yote, nimeweza kutumikia wananchi wa Kigoma na watanzania bungeni kwa miaka 10. Kama hii si ndoto iliyokuja kuwa kweli, ni nini?

Zitto Zuberi Kabwe angezaliwa mwaka 2000, angekuwa kijana ambaye hajakamilisha elimu yake, haelewi lugha za kigeni kama kiingereza, hana ujuzi wowote na kama Mungu angeendelea kuninyima kipaji cha kuimba kama sasa ningeshindwa hata kutoka kama Diamond na Mwana FA!

Mwalimu Nyerere asingepigania ndoto yake miaka ya 60 na 70, ningekuwa kama mamilioni ya vijana leo ambao wanahangaika kutafuta ajira na kipato bila ujuzi na elimu.

Na ndiyo maana siku ya leo ni muhimu kwangu. Nina furaha na heshima kubwa kuwa katika familia yangu mpya ya kisiasa. Familia inayoaamini katika itikadi, misingi na tunu ninazoziamini.

Nimezungumza mara kadhaa kuhusu sababu za kujiunga na chama hiki. Chama cha Wazalendo ACT- Tanzania inaongozwa na misingi ya Uzalendo, Demokarsia, Uhuru wa fikra na matendo, Utu, Usawa, Uadilifu, Uwazi, Uwajibikaji na Umoja katika kila kitu. Chama hiki ni cha wananchi si wenyenchi wa sasa waliojimilikisha taifa. Chama hiki ni cha watanzania wote bila kujali kabila, dini, jinsia, rangi ya ngozi au hali ya ulemavu!

Tunapojadili wananchi kujimilikisha upya nchi yetu ni kupitia usimamizi wa sheria utakaohakikisha kuwa kuna uwazi na uwajibikaji wa viongozi. Uwazi tunaouamini ni ule utakaohakikisha kila mwananchi anapata taarifa za fedha zao, mikataba ambayo Serikali inaingia kwa niaba yao na taarifa za maslahi, mali na madeni ya viongozi wao.

Tunataka uwazi katika uendeshaji wa Serikali na sisi tutaanza na uwazi katika uendeshaji wa chama chetu. Tunataka wananchi sio tu wajione kuwa sehemu ya uendeshaji wa nchi yao, bali pia wawe sehemu ya uendeshaji wa nchi yao.

Tunataka uwazi utakaoruhusu uhuru wa mawazo na uhuru wa wananchi kujieleza bila kuhofu Serikali kuwachukulia hatua kwa kutoa mawazo yao. Ndio maana ACT Wazalendo tunapinga vikali miswada ya sheria ambayo Serikali ya CCM imeiwasilisha bungeni katika mkutano unaoendelea.

Miswada hii kama vile muswada wa Haki ya kupata taarifa, vyombo vya habari na ule wa makosa ya mtandao, inalenga kuminya na kunyima haki za wananchi kuwasiliana kwa uhuru na kutoa mawazo yao kama inavyoainishwa katika katiba ya nchi.

Tunapojadili wananchi kurejesha taifa mikononi mwao tunazungumzia uwajibikaji. Ripoti ya Tume ya Marekebisho ya Katiba ilieleza moja ya sababu kubwa ya kushamiri rushwa, ufisadi na ubadhirifu nchini ni nanukuu ‘kukosekana kwa mfumo madhubuti wa uwajibikaji’ nchini kwetu.

Sababu kubwa ya ACT Wazalendo kupinga Katiba inayopendekezwa ni kwamba Katiba hiyo imechakachua nia hii ya kuweka mfumo wa uwajibikaji. Ndio maana tunawaambia wananchi waikatae Katiba hiyo kwa nguvu zao zote! Katiba inayoepndekezwa inastahili kadi nyekundu, tuikatae na kura ya hapana!

Iwapo wananchi hawawezi kuwawajibisha viongozi kwa matendo yao hatuwezi kujenga jamii ya watu wanaoheshimiana na kutii sheria za nchi.

Kila Mtanzania bila ya kujali cheo chake ni lazima awe chini ya sheria. Uwajibikaji ni lazima uanze na viongozi. Mnajua kuwa katika maisha yangu ya kisiasa hili ndio limekuwa jukwaa langu.

Kwa bahati mbaya tunaishi katika kipindi ambacho wanasiasa wengi wamekuwa wakikumbwa na kashfa mbalimbali za kifisadi na matokeo yake inajengwa picha kuwa kila mwanasiasa ni fisadi.

Mfumo wa Uwajibikaji wenye uwazi utasaidia wananchi kutofautisha wanasiasa wanaosimamia maslahi ya umma na wale wanaosimamia maslahi yao binafsi na vyama vyao vya siasa.

Mwungwana ni vitendo; nimewajibisha watu kwenye Buzwagi na mikataba ya madini, kwenye matumizi mabaya ya fedha za umma na juzi juzi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow. Lakini matukio haya machache hayatoshi kujenga mfumo madhubuti wa Uwajibikaji.

Ni lazima kufanya mapinduzi ya mfumo mzima wa uchumi wa nchi yetu na kujenga mfumo mpya unaohudumia kila Mtanzania na ambao kila Mtanzania anajivunia kuujenga. Hatuwezi kuwa Taifa linaloshikiliwa na vikundi vya wafanyabishara wachache na wanasiasa wanaofadhiliwa na wafanyabishara hao.

ACT Wazalendo inataka kujenga Taifa ambalo viongozi wake wanawajibika kwa wananchi. Hii ndio fikra tunayotaka kurejesha. Hizi ndizo siasa zilizoasisi Taifa letu. Hatuna budi, ni lazima kurudi kwenye misingi na kuanza upya!

Kwa sababu ACT Wazalendo imejikita kwenye misingi hii, tumelihuisha Azimio la Arusha.

Sio tu tumeweka miiko ya uongozi lakini pia tumetunga kanuni za kutekeleza miiko hiyo na kuifanya kuwa sehemu ya Katiba ya chama chetu. Hitaji moja kubwa la Kanuni zetu za Maadili ni kutaka kila Kiongozi wa ACT Wazalendo kuweka hadharani Maslahi yake, Mali na Madeni yake.

Katika chama hiki huo ndio utamaduni wa kisiasa tunaotaka kuujenga. Kutenda tunachohubiri hata kabla ya kuingia kwenye uongozi wa Dola.

Chama cha ACT Wazalendo kimeelekeza kikanuni kwamba kila Kiongozi wa chama lazima atangaze Mali zake na Madeni yake. Kila Kiongozi lazima aweke wazi maslahi yake ya kibiashara na mengineyo wazi ili kila anapotenda au kusema jambo wananchi wajue maslahi aliyonayo au la katika suala husika.

Viongozi wote wa kitaifa wa ACT Wazalendo wamefanya hivyo na tutaweka saini zetu mbele yenu kama mashahidi. Naomba Mwanasheria wetu aje hapa tutekeleze matakwa haya ya kikanuni.

Fomu hizi zitakuwa kwenye tovuti ya chama ndani ya muda mfupi ujao ili kila mtanzaina aone. Kila Kiongozi wa Chama ambaye Miiko ya Uongozi inamtaja anapaswa kuwa amejaza fomu hizi na kuziwasilisha kwa Katibu wa Kamati ya Uadilifu katika ifikapo tarehe 30 Juni 2015.

Tunapopinga Viongozi wa Umma kufanya Biashara na Serikali na hivyo kuwa na mgongano wa kimaslahi na kushamiri kwa ufisadi, hivyo hivyo tunapinga Viongozi wa Chama chetu kufanya Biashara na Chama. Ni Marufuku Serikali kugeuzwa kuwa genge la watu wachache wanaopora rasilimali za Umma. Uadilifu tunaoutaka Serikalini ni lazima uanzie kwetu tunaohubiri.

Tutafanya haya kwa kubadilisha siasa zetu kuelekea kwenye masuala yanayowahusu wananchi; Wakulima, Wafanyakazi, Wafanyabiashara ndogo ndogo, Vijana, Wanawake na Wazee wetu.

Tunataka kurejesha nchi yetu Tanzania kwa kujenga uchumi wa wote. Tunaporejea kwenye Azimio, hatusemi tunakwenda kutaifisha kila kitu na Serikali kuendesha shughuli zote za kiuchumi. Tunaheshimu na kuthamini sekta binafsi na mchango wake katika kukuza uchumi na kuleta maendeleo. Tunamaanisha kuwa ni lazima Dola isimamie uchumi.

Sio kazi ya Serikali kufanya biashara. Lakini tunamaanisha kuwa ni lazima kurekebisha baadhi ya makosa yaliyofanyika kwenye ubinafsishaji na hususan ubinafsishaji holela uliofanyika kwenye sekta ya Kilimo na kupora ardhi ya wananchi wetu na kuwageuza kuwa manamba kwenye ardhi yao wenyewe.

Tunataka kutomokeza ukwepaji kodi.
Tanzania inapoteza 15% ya makusanyo katika forodha kwa sababu ya ukwepaji wa kodi. Hii ni sawa na tshs 490 bilioni kwa mwaka, fedha ambazo zingeweza kuchangia wananchi milioni 4 kwenye hifadhi ya Jamii.

Tanzania inapoteza takribani tshs 2 trilioni kila mwaka kwenye misamaha ya kodi. Hii ni fedha ambayo ingeweza kujenga reli mpya ya kati ya kisasa kutoka Dar mpaka Mwanza na Kigoma ndani ya miaka mitatu. Ili kuondoa upotevu huu ni lazima kupanua wigo wa kodi, kurahisisha kodi, kupunguza baadhi ya kodi kama ( PAYE) na kutumia teknolojia kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi.

Vile vile ni muhimu kuimarisha mfumo wetu wa kodi za kimataifa ili kuzuia utoroshaji mkubwa unaofanywa na makampuni ya kigeni. Ili tujitegemee kama Taifa ni lazima kukusanya mapato ya ndani ya kutosha. Ili kukusanya mapato ya ndani ya kutosha ni lazima kuweka mazingira mazuri ya biashara hasa kwa wafanyabishara ndogo ndogo kwani ndio wazalishaji wakubwa wa ajira.

Kwa Vijana, Taifa hili ni lenu. Asilimia 75 ya Watanzania wapo chini ya miaka 40. Asilimia 65 ya wapiga kura wapo chini ya miaka 40. Nusu ya Watanzania ni watoto chini ya miaka 18. Kurejesha nchi kwenye misingi ni wajibu wa kujenga maisha yenu. Haikubaliki Vijana kuwa mzigo kwa wazazi kwa sababu tu uchumi hauzalishi ajira za kutosha.

ACT Wazalendo ndio jukwaa lenu la kufanya mapinduzi ya mfumo wa uchumi ili kujenga uchumi shirikishi unaozalisha ajira. ACT Wazalendo inataka kuwajengea mfumo wa hifadhi ya jamii ambapo mtakapokuwa Wazee msipate tabu za pensheni na matibabu wanazopata Wazee wetu hivi sasa. Shiriki kujijengea Taifa litakalohakikisha maisha yako ya sasa nay a baadae na ya kizazi kijacho.

Kwa Wanawake, Ninyi ndio mhimili wa Taifa hili, wazalishaji wakuu na walezi wa Taifa letu. Kurejesha nchi kwenye misingi ni wajibu wa kutambua nafasi yenu stahili katika jamii.

Nikiwa nimelelewa na Mwanamke mwenye ulemavu na mpiganaji wa kweli wa haki za wananchi walio pembezoni, sina namna kutoa heshima yangu zaidi ya kuongoza chama chenye misingi thabiti ya kumkomboa mwanamke. Msitarajie watu wengine kuwapigania mnapaswa kuchukua hatua kupitia jukwaa hili la ACT Wazalendo.

Kwa wafanyabishara, ninyi ndio mnachochea shughuli za Uchumi na kuzalisha ajira. Kuanzia kwa wamiliki wa maduka madogo mitaani mpaka kwa mameneja wa maduka makubwa; kutoka kwa wachuuzi na mama lishe mpaka kwa wamiliki wa viwanda na biashara; mnaamka kila siku asubuhi kujenga Taifa hili kwa kuzalisha mali na huduma.

Baadhi yenu ambao mnamiliki viwanda, mashirika makubwa na kutoa ajira kwa maelfu ya wananchi, mmeanza mkiwa mnashona viatu na sare za shule, au mkitengeneza na kuuza mkate.

Mmepata utajiri wenu na mali zenu kwa juhudi na jasho lenu na kutokana na fursa za kiuchumi zilizokuwepo kipindi hicho ambacho hakikuangalia dini, kabila, uwezo wa kifedha au rangi ya ngozi.

ACT Wazalendo inataka kuwawekea mazingira bora ya biashara halali lakini pia kuhakikisha mnalipa kodi zenu na kutonyonya wafanyakazi wenu.

Tunataka kuwawekea mfumo rahisi wa kodi, wenye kueleweka na unaowapa motisha kuzalisha zaidi ili kuongeza ajira zaidi na kupanua Pato la Taifa. Msipotimiza wajibu wenu biashara zenu hazitashamiri. Kurudi kwenye misingi ya Taifa hili ni kurejesha maadili katika biashara zenu.

Kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi, ninyi ndio mnaolilisha Taifa letu na kuleta fedha nyingi za kigeni kupitia mauzo nje.

Kwa miongo mitatu sera za nchi zimewaweka pembeni na hivyo uchumi wenu kusinyaa. Viwanda vyote vya kusindika mazao yenu vimeuzwa kwa bei ya kutupwa licha ya kwamba jasho lenu ndio lilitumika kuvijenga. Miundombinu ya barabara, maji, umeme na mawasiliano haiwafikii ili muweze kupata masoko.

Hamna hifadhi ya jamii wala bima ya mazao yenu. Ardhi yenu wamepewa wawekezaji na mnakodishiwa, mnapanga kwenye ardhi yenu wenyewe. Mmeachwa mkijihangaikia.

Kurejesha nchi kwenye misingi kutawarudishia heshima yenu katika nchi yetu. ACT Wazalendo ndio jukwaa sahihi kwenu kuhakikisha kuwa tunajenga uchumi shirikishi ambao mtafaidika na jasho lenu. Hamna cha kupoteza isipokuwa minyororo ya kinyonyaji.

Kwa Watanzania wote mnaonisikiliza leo, katika ukumbi huu na popote mlipo kupitia vyombo vya habari, mnamo mwaka 1978 Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitangaza vita dhidi ya nduli Idi Amini na kusema;

“Tutampiga. Sababu za kumpiga tunazo, nia tunayo, uwezo wa kumpiga tunao”.

Tanzania ipo katika vita hivi sasa.
Vita dhidi ya Ufisadi,
vita dhidi ya uporaji wa rasilimali zetu,
vita dhidi ya Siasa chafu.
Vita dhidi ya Uchumi wa kinyonyaji.
Vita dhidi ya kuporomoka kwa Utaifa wetu.

Tunapaswa kufanya jambo moja tu, nalo ni kupigana vita hizi. Ni vita kwa ajili ya kurejesha ndoto tuliyoota miaka 54 iliyopita na Muasisi wetu Mwalimu Julius Nyerere. Tunataka kurejesha nchi kwa wananchi, tunataka kujimilikisha nchi yetu. Wananchi wawe WENYE nchi!

Tutimize ndoto yetu ya kuona;
Tanzania yenye Dola madhubuti,
Tanzania yenye Wananchi wenye mwamko,
Tanzania yenye sekta binafsi iliyochangamka,
Tanzania yenye uchumi unaonufaisha watu wote.
Sababu tunazo, nia tunayo na uwezo tunao. Twendeni tukajenge Chama kitakachorejesha misingi ya Taifa letu.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...