Showing posts with label H/KITAIFA. Show all posts
Showing posts with label H/KITAIFA. Show all posts

2015-04-10

Breaking News!!! Mabomu ya Machozi yanarindima muda huu Kituo cha Mabasi Ubungo hali mbaya mgomo wa madereva


Katibu wa Madereva Mboka akiongea na wandishi wa Habari muda huu, kabla ya mabomu hayajarindima

…Mgomo wa Mabasi kuwa endelevu hadi watakapo achiwa viongozi wao wanaoshikiliwa na jeshi la Polisi

Na Andrew Chale wa Modewji blog

Modewji blog ambayo imepiga kambi katika kituo cha Mabasi Ubungo kuanzia majira ya saa 11, alfajiri, ni kuwa tayari baadhi ya viongozi wa madereva wametoa tamko rasmi kuwa mgomo wao huo utaendelea hadi hapo viongozi wao wakuu zaidi ya Sita (6) wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi watakapoachiwa huru ikiwa ni pamoja na kuondoa masharti dhidi ya waliyowekewa katika suala la leseni kwa madereva hao.

Kwa mujibu wa Katibu Mwenezi wa madereva, Mboka Mwalaikwe alibainisha kuwa suluhu pekee kwa kunusuru abiria waendelee na safari ni kwa Jeshi la Polisi kuwaachia huru viongozi hao wanaowashikilia.

“Huu sio mgomo bali ni kueleza kwamba baadhi ya mambo wanayotufanyia Serikali sasa yamefika mwisho, Aprili Mosi mwaka huu tulitaangaza rasmi kuwa ifikapo Aprili 10, endapo madai yetu ya msingi hayajatatuliwa basi tutagoma. 

Baadhi ya madereva wakiwa wamejikusanya muda huu huku magari yaakiendelea kuwashwa moto

Hata hivyo Jana Aprili 9, Jeshi la Polisi asubuhi limewakamata viongozi wetu sita akiwemo Mwenyekiti, msaidizi na wajumbe wake na kuwashikiria, hii bado si haki na sisi tutaendelea na mgomo huu kwanza hadi waachiwe na pia waje hapa watu wa NIT, Waziri na Jeshi la Polisi kwani wao ndio wanasababisha matatizo makubhwa” alieleza Mboka.

Kwa upande wao badhi ya madereva walioongea na Modewji blog, walieleza kuwa, wamechoka na unyanyasi unaofanywa na Serikali ikiwemo kupitia idara na taasisi zake kwani zinaanzisha mambo makubwa ambayo utekelezaji wake ni mgumu pia inawakandamiza wao madereva.

Mabomu mabomu mabomu ya machozi yanapigwa muda huu hapa standi ya mabasi Ubungo hali ni mbaya… 




TAFADHALI TAARIFA HIZI UKINAKILI KWENYE CHOMBO CHAKO UTAJE UMEZIPATA MODEWJI BLOG!!!!

WANDISHI WA HABARI WOTE WANAPIGWA HUKU HAKUNA ANAYEPONA WATU WOTE WAMETAKIWA KUTOKA NJE YA STAND NA NJE MAGARI YANA YANACHOMWA MOTO HASA NOAH ILIYOTAAKA KUBEBA ABIRIA… PICHA NA TAARIFA ZAIDI ZINAWAJIA PUNDE TENA MAANA HAPA NILIPO NIMELEWA MOSHI WA MABOMU…
 MODEWJIBLOG.

Askari wa JKT Auawa Wakati Akisaidiana na Polisi Kuyakabili Majambazi Yaliyokuwa Yamepora Fedha Iringa


Watu wawili akiwemo jambazi mmoja na askari mwanafunzi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), wamekufa na wengine kunusurika kuuawa katika tukio lililotokea juzi, mjini Mafinga mkoani Iringa wakati majambazi wakirushiana risasi na askari wa Jeshi la Polisi.

Risasi hizo zilipigwa wakati Polisi hao wakijaribu kuokoa fedha za mfanyabiashara Salama Semwaiko zilizoporwa na majambazi wawili waliotumia pikipiki wakati wakifanya uporaji huo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi alisema mfanyabiashara huyo aliporwa fedha hizo juzi majira ya saa 2.45 asubuhi alipokuwa akitoka nyumbani kwake kwenda kwenye biashara zake.

Tukio hilo la kusikitisha lililovuta hisia za watu wengi na kufanya baadhi kuzimia wengine kukimbia hovyo na kujifungia ndani kwa ajili ya kuokoa maisha yao lilitokea katika eneo la Kinyanambo B, nje kidogo ya mji wa Mafinga.

Kamanda Mungi alisema; “mfanyabiashara huyo akiwa katika gari lake akielekea kwenye biashara zake mjini Mafinga, mfanyabiashara huyo alisimamishwa na mtu mmoja aliyekuwa amevaa koti jeusi na baada ya kusimama alimtolea silaha na kumtaka atoe fedha na vitu vyote vya thamani alivyokuwa navyo .” 

“Baada ya kuona hana msaada mfanyabiashara huyo alijikuta akilazimika kutoa Sh 700,000 alizokuwa nazo, simu ya mkononi na baadaye ilitokea pikipiki ambayo haikufahamika namba za usajili na kumpakia mtu huyo na kuanza kukimbilia eneo la Kinyanambo,” alisema.

Alisema mara baada ya majambazi hao kutoweka, Jeshi la Polisi lilipewa taarifa na kuwahi eneo la tukio na kwa kushirikiana na wananchi walianza kuwakimbiza majambazi hao na ndipo majibizano ya risasi yalipoanza. 

Katika hekaheka hiyo, Kamanda Mungi alisema Said Ngudi (25) ambaye ni askari wa JKT Makutupora, Dodoma alipigwa risasi na kufa papo hapo wakati akisaidia kupambana na majambazi hao.

Diwani wa CHADEMA Apewa Adhabu ya Kufua Shuka za Wagonjwa Hospitalini na Kuzibua Mitaro ya Barabarani


Diwani wa Kata ya Kasanda wilayani Kakonko, Dickson Barutwa (40) wa Chadema na wenzake watatu, wamehukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Kibondo adhabu ya kufua shuka za wagonjwa katika hospitali ya wilaya ya Kakonko na kuzibua mitaro ya barabarani kwa siku 14 baada ya kukutwa na hatia ya makosa matatu.

Baadhi ya makosa hayo yametajwa kuwa ni kuifunga ofisi ya Mtendaji wa Kijiji isivyo halali na kuweka gundi na unga wa ngano kwenye kufuli kwa lengo la kumzuia Mtendaji wa Kijiji asifanye kazi.

Mbali ya Barutwa wengine ni Daudi Obadia (32), Hatari Kasase (33) na Brighton Jona(29), wote wakazi wa kata ya Kasanda, Kakonko. 

Watu hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibondo, Erick Marley na kusomewa mashitaka na Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Peter Makalla.

Mwendesha Mashtaka alisema mnamo Novemba 8 mwaka jana, majira ya saa kumi jioni katika kijiji cha Kaziramihunda, watuhumiwa wote kwa pamoja walifika katika ofisi ya Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho isivyo halali na kuifunga ofisi hiyo kwa kuweka gundi aina ya Super Glue na unga wa ngano kwenye kufuli ili kumzuia Mtendaji asifanye kazi yake.

Inadaiwa watu hao walifikia uamuzi huo kwa madai kuwa hawakuwa wanamtaka Mtendaji huyo wa Kijiji, Amos Peter na kumtishia kumuua.

Kutokana na makosa hayo, Mahakama ya Wilaya ya Kibondo imewahukumu kulipa faini ya Sh 50,000 au kufungwa jela miezi mitano kwa kosa la kufunga Ofisi ya Mtendaji, na pia kulipa faini ya Sh 50,000 au kwenda jela miezi miwili kwa kosa la kufanya fujo. 

Watuhumiwa wote walilipa faini na kuachiwa huru isipokuwa Kasase anayekabiliwa na kesi nyingine ya mauaji, hivyo alirudishwa gerezani.

Aidha, katika kosa la kutishia kuua diwani huyo na wenzake watatu wamehukumiwa adhabu ya kazi za kijamii ambayo ni kufua shuka za wagonjwa katika hospitali ya wilaya ya Kakonko kwa muda wa wiki moja na kuzibua mitaro ya barabara kwa muda wa wiki moja pia.

Tayari diwani huyo na wenzake wameshakabidhiwa katika Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa ajili ya kuanza adhabu hiyo. Watuhumiwa wengine katika kesi hiyo walioachiwa huru baada ya kukutwa hawana hatia, ni Boniface Obadia (35) Amos Buseni (33), Majaliwa Charles (24) na Samora Barichako (35), wote wakazi wa kijiji cha Kaziramihunda.

Kamanda Wa Polisi Mkoa Wa Arusha Akanusha Kukamatwa Kwa Mwanaume Mwenye Mabomu Na Watu Wanne Wenye Bunduki



Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatusi Sabas amekanusha uvumi ulioenea katika mitandao ya jamii kuhusu kukamatwa mwanaume mmoja aliyevalia vazi la baibui akiwa na bomu mkoani humo na kwamba watu wengine wanne wamekamatwa wakijiandaa kuingia chuo cha uhasibu.

Uvumi huo umeanza kusambaa kwa kasi leo asubuhi ukidai kukamatwa kwa watu wanne waliokuwa ndani ya gari aina ya Toyota Premio huku wakiwa na bunduki 4 aina ya SMG na Risasi 160. 

Ujumbe huo ulidai kuwa watu hao walikamatwa jana usiku wakijiandaa kuingia chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kuonana na ndugu yao mmoja wa kike anayeishi katika hosteli za chuo hicho.

Pia ilielezwa kuwa, baada ya kufika getini,mlinzi aliwashtukia na kupiga simu polisi ambapo walikamatwa. 

Mbali na taarifa hizi kukanushwa na kamanda wa Polisi,Mpekuzi imeongea na Raisi wa wanafunzi wa Chuo hicho ndugu Iman Mkumbo ambaye naye amezikanusha taarifa hizo na kusema si za kweli.

"Hali ni shwari hapa chuoni,tangu juzi usiku kuna doria kali ya polisi maeneo yote ya chuo, hivyo watu wanapata hofu na kuanza kuzusha taarifa zisizo za kweli."Amesema Mkumbo

Sakata la Gwajima: Polisi Wamhoji Kwa Masaa Matano..... Atakiwa Kurudi Polisi Wiki Ijayo na Hati ya Usajili wa Kanisa Lake,Helkopta na Viwanja Anavyomiliki


Askofu wa Kanisa la Ufufua na Uzima Josephat Gwajima amelitikisa tena Jiji la Dar es Salaam jana mara baada kuwasili makao makuu ya Jeshi la polisi kanda maalum ya Dar es Salaam ili kuendela na mahojiano kuhusu tuhuma za kumkashfu Askofu Pengo.

Gwajima aliwasili Makao Makuu ya Jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Majira ya saa mbili kamili asubuhi huku akisindikizwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa la Ufufuo na Uzama pamoja na Mwanasheria wake .

Eneo lote la kituo hicho cha polisi lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa maofisa mbalimbali wa Usalama wa Taifa wakisaidiwa na Jeshi la Polisi.

Baada ya kuwasili kituoni hapo, umati mkubwa wa Waumini wake ulizunguka maeneo yote ya Kituo hicho huku wengine wakiwa maeneo ya stendi ya Treni ya Reli ya kati.

Kama kawaida, Waumini hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali ambazo wanadai zilikuwa mahususi kumpa nguvu Askofu huyo ajibu kesi hiyo kwa ufasaha. 

Baada ya Mahojiano ya takribani masaa Matano, hatimaye Askofu Gwajima alitoka ndani ya kituo hicho,lakini katika hali isiyo ya kawaida,Askofu huyo aligoma kuongea na vyombo vya habari.

Baada ya Gwajima kugoma kuongea,mwandishi wetu alimfuata Mwanasheria wake aliyekuwa ameambatana naye,John Mallya ambaye alisema kuwa mteja wake alikuwa amechoka, hivyo asingeweza kuongea.

Mallya alimweleza mwandishi kuwa mambo aliyohojiwa Gwajima ni kuhusu mali zake na sio matamshi ya kumtukana Askofu Pengo.

“Mahojiano yamekwenda vizuri lakini nasikitika sana kutokana na mambo waliyokuwa wanamhoji. Wamemuuliza mambo ambayo hayahusiani kabisa na kile tulichotarajia na ndicho kilichotuleta hapa, nilidhani mteja wangu ataulizwa kuhusiana na matumizi ya lugha chafu iliyodaiwa kutumika kumkashifu kiongozi mwenzake wa dini,” alihoji wakili wa Gwajima. 


Aliendelea kusema kuwa, mambo aliyoulizwa ni kuhusiana na ukoo wake, wazazi wake hata ndugu zake na watu wengine wa kwao waliokufa.

Alisema walihoji pia juu ya mambo mengine kama umiliki wa helikopta, utajiri wake, nyumba anayoishi, uhusiano wake na watu mbalimbali.

“Nimeshangaa sana kuona mteja wangu ameulizwa vitu kama hivyo ambavyo havihusiani na madai ya hapo awali ya matumizi ya lugha ya matusi. Tumeagizwa tulete nyaraka kumi siku ya mahojiano yetu tena yatakayofanyika tarehe 16 mwezi huu na sisi tutafanya hivyo,” alisema Mallya.

Alizitaja nyaraka na vitu vingine wanavyotakiwa kuvipeleka Aprili 16 ni hati ya usajili wa kanisa, bodi ya udhamini wa kanisa na majina yao, idadi ya makanisa yaliyopo chini yake, na muundo wa uongozi wa kanisa lake.

Vingine ni namba ya usajili wa kanisa, ritani za kanisa lake (mapato na matumizi ya fedha za kanisa lake), mtu anayechukua na kurekodi mkanda wa video kanisani kwake, pamoja na waraka wa Baraza la Maaskofu uliosomwa makanisani.

GWAJIMA AWAACHA WAUMINI WAKE NJIA PANDA


Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

MCHUNGAJI wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amewaacha waumini wake njia panda kufuatia kauli yake ya kuwataka wamsindikize Kituo Kikuu cha Polisi cha Kati jijini Dar, jana alipokwenda kuhojiwa huku Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akiwa ametoa tamko la kuzuia waumini hao kukusanyika kituoni hapo. 

Gwajima aliyetoa kauli hiyo kwa waumini wake katika ibada ya Jumapili iliyopita kanisani kwake, Kawe jijini Dar, alitarajiwa kufika kituoni hapo kujibu tuhuma za kumtusi Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinari Pengo.

Wakizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutoandikwa majina yao, juzi jijini Dar, baadhi ya waumini wa Gwajima walisema wanashindwa kufanya uamuzi wa kumsindikiza kiongozi huyo kwani jeshi la polisi limesema halitaruhusu mtu kumsindikiza.

“Kusema kweli tumebaki njia panda maana mchungaji amesema twende tumsindikize lakini Kova naye kasema jeshi la polisi litatumia nguvu kuwatawanya watu ambao watakaidi amri hiyo ya jeshi la polisi,” alisema muumini mmoja huku waumini wenzake wakiunga mkono. 


Wakati Gwajima alipowataka waumini wake wamsindikize kituoni hapo, Kova alisisitiza kuwa kiongozi huyo wa dini anatakiwa kufika kituoni hapo akiwa na mwanasheria wake pamoja na watu wachache tu wa karibu hivyo kuwafanya waumini wengi wa kanisa la Gwajima kubaki njia panda.

Kupitia video inayomuonesha Gwajima akimtupia maneno makali Pengo, mchungaji huyo wa Ufufuo na Uzima alimtuhumu Pengo kuwa amewasaliti maaskofu wenzake waliotoa tamko la kuipigia kura ya ‘Hapana’ Katiba Inayopendekezwa kwa kile walichodai haikukidhi matakwa ya wananchi.
GPL

Siri mpya Mtanzania Al-Shabaab...........soma hapa









SIRI mpya juu ya Mtanzania Rashid Charles Mberesero, anayehusishwa na tukio la kigaidi kwenye Chuo Kikuu cha Garisa nchini Kenya zimeibuka.

Kwa mujibu wa habari zilizoripotiwa jana na vyombo vya habari vya Kenya, Mtanzania huyo anayedaiwa kuwa miongoni mwa magaidi wa Al-Shabaab walioua watu 148 katika chuo hicho, endapo angesalimika baada ya tukio hilo, angepelekwa Somalia yalipo makao makuu ya kundi hilo la kigaidi.

Hayo yalibainishwa jana na mwendesha mashtaka wa nchi hiyo, Daniel Karuri katika mahakama ya jijini Nairobi.

Mahakama hiyo imeamuru Rashid akae kizuizini kwa siku 30 akisubiri uchunguzi wa tuhuma zake.

Pia watu wengine 14 wanaotuhumiwa kuhusika na kundi la Al Shabaab wameamuriwa wakae rumande kwa muda wa siku 30 wakisubiri kufanyiwa uchunguzi zaidi.

Polisi inaendelea kuchunguza mawasiliano ya simu waliyokuwa wakifanya watuhumiwa hao kwa ajili ya kutafuta ushahidi zaidi wa wahusika wote wa shambulio hilo.

Kwa mujibu wa mamlaka husika, Rashid alikamatwa akiwa amejificha juu ya dari la chuo hicho akiwa ameshikilia silaha na mlipuko.

Mmoja miongoni mwa watuhumiwa hao alikamatwa katika chuo kikuu hicho, akiwa anafanya kazi kama mlinzi na wengine walikamatwa wakati wakijaribu kuvuka mpaka na kuingia Somalia.

Wakati walipovamia chuo hicho, wauaji waliwatenga wanafunzi wa Kiislamu na wale waliobainika kuwa Wakristo waliuawa kwa kupigwa risasi.

Kundi la Al Shabaab limedai kuhusika na mauaji hayo na kwamba tukio hilo lilidhamiria kutuma salamu kwa Serikali ya Kenya ambayo imehusika kutuma majeshi yake Somalia kupambana na kundi hilo.

Mara ya mwisho kwa Kenya kushambuliwa ilikuwa mwaka 1998 ambako ubalozi wa Marekani ulilipuliwa jijini Nairobi.

MIEZI MITANO NJE YA SHULE
Mama mzazi wa Rashid, jana alilieleza gazeti hili kuwa wakati Mkuu wa Shule ya Bihawana, Mbilinyi Joseph akisema tangu Novemba mwaka jana mtoto huyo alitoroka shuleni, yeye anajua mwanawe huyo kwa kipindi cha mwisho wa mwaka alibaki shule ili asome masomo ya ziada.

“Wakati huyo mwalimu wake akisema kuwa Rashid hayupo shuleni kuanzia Novemba, nakumbuka kuwa huo mwezi alinipigia simu akaniambia kwa sababu yeye alichelewa kuanza masomo, anataka abaki shuleni ili asome tuisheni awafikie wenzake.

“Akaniambia nimtumie hela ya twisheni, nikamtumia Sh 110,000 ili Sh 60,000 iwe ya tuisheni na nyingine ya kunua viatu na mahitaji yake mengine.

“Kwa hiyo muda wote huo nilikuwa najua mtoto yuko shuleni na ilivyofika mwezi wa tatu ndiyo akaja nyumbani akaniambia wenzao wa kidato cha sita walikuwa wanafanya mtihani na baada ya hapo kulikuwa na likizo ya wiki.

“Alisema hakuona sababu ya kusubiri hadi shule ifungwe kwa sababu wakati huo wenzao wakifanya mtihani, wao hawakuwa wakisoma, kwa hiyo ameamua kurudi nyumbani,” alisema.

Alisema katika kipindi ambacho mwanawe huyo alikaa nyumbani, hakuhisi mabadiliko yoyote ya tabia yake na kuwa alimsaidia kuvuna mazao yake shambani.

“Kabla ya Pasaka ndiyo akaniambia kwa kuwa umebaki muda mfupi shule ifunguliwe na kwa sababu yeye ni Muislamu hana sababu ya kusubiri sherehe za Pasaka, anarudi shuleni ili akaendelee na masomo.

“Sasa nashangaa kusikia kwamba hakuwepo shuleni tangu mwezi wa 11, kwanini hao walimu hawakunipigia simu kuniambia hadi tunasikia hayo ya Kenya namtuma shangazi yake ndiyo wanamwambia muda mrefu mtoto hakuwa shuleni?” alihoji mama huyo.

Alisema wakati huo wa mwisho wa mwaka jana alipokuwa akijua kuwa mwanawe yupo shuleni, alikuwa akiwasiliana naye ingawa siyo mara kwa mara.

“Alikuwa ananipigia simu, lakini alikuwa anatumia namba tofauti tofauti kwahiyo sikuziweka na nilijua tu anaomba simu za walimu wake kwa sababu pale shuleni hawaruhusiwi kuwa na simu.

“Kwahiyo mimi kabisa nilijua mtoto wangu yupo shule na aliniahidi atasoma kwa bidii hadi awafikie wenzake ambao tayari walikuwa wamemtangulia,” alisema.

MWALIMU MLEZI AFUNGUKA
Mwalimu wa Shule ya Sekondari Bihawana, ambaye pia ni mlezi msaidizi wa Kikundi cha Waislamu cha Tamsiia cha shuleni hapo, Idd Hussein, jana aliliambia gazeti hili kuwa Rashid alihamia mwaka jana kutoka Shule ya Sekondari Kigwe iliyoko Wilaya ya Bahi.

“Huko Kigwe alikuwa anasoma mchepuo wa HGL, alipokuja hapa akabadili akawa anasoma PCB… Alikuwa ni mtu mwenye misimamo na alishikilia sana dini,” alisema.

Alisema Rashid alikuwa anapenda kwenda msikitini, akifika alikuwa anasali na akimaliza anasoma Quran kidogo na kurejea bwenini kuendelea na taratibu zake nyingine.

Mwalimu Hussein alisema kutokana na shule hiyo kuwa ya mchanganyiko wa Wakristo na Waislamu ni marufuku kuvaa rozari wala balaghashia.

“Rashid alikuwa ni mbishi, alivaa balaghashia maeneo ya shule hali iliyosababisha atofautiane na mkuu wa shule ikamlazimu atuite tuzungumze nae.

“Mkuu wa Shule alitaka kuichana balaghashia lakini tukamsihi asifanye hivyo kwa kuwa kitendo hicho kinaweza kuleta chuki kwa Waislamu hivyo tukashauri ampe adhabu ambayo hata hivyo hakuifanya badala yake akapotea shuleni,” alisema.

Alisema baada ya Rashid kupotea shuleni hapo, yeye na viongozi wenzake walimuita kiongozi wa wanafunzi wa Jumuiya ya Kiislamu shuleni hapo ambaye alidai hajui alipokwenda kwa kuwa hakumuaga.

KAULI YA RPC, DC
Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Dodoma, David Misime alipoulizwa kuhusu kijana huyo kutokea Sekondari ya Bihawana, alisema hawezi kuliongelea suala hilo.

“Ugaidi umefanyika Kenya sio Dodoma kwa hiyo siwezi kuliongelea suala hilo,” alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya (DC) ya Dodoma Mjini, Betty Mkwasa alisema hana habari kwamba Rashid alikuwa anasoma Sekondari ya Bihawana.

“Mie sina taarifa ndiyo kwanza nasikia kutoka kwako, basi ngoja nilifuatilie,” alisema Mkwasa.

Gwajima kitanzini


JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemtaka Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kupeleka nyaraka 10 za mali anazomiliki.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwanasheria wa Askofu Gwajima, John Mallya, alisema anatakiwa kuzipeleka nyaraka hizo kituoni hapo Aprili 16 mwaka huu.

Mallya alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya mteja wake kuhojiwa na polisi kuhusu tuhuma zinazomkabili za kumtolea maneno ya kashfa hadharani Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Alisema mahojiano yaliyoanza saa saa 1:14 asubuhi hadi saa 6:45 mchana jana yalitawaliwa na maswali ya kumtaka aeleze mali zake anazozimiliki ikiwamo helkopta pamoja na historia ya familia yake.

“Polisi walitaka kujua ukoo wa baba na mama yake, ndugu zake waliofariki dunia na kujieleza lugha ya matusi anayodaiwa kutoa hadharani dhidi ya Kardinali Pengo,” alisema Mallya.

Alisema baada ya mahojiano hayo polisi walimtaka Askofu Gwajima kupeleka nyaraka 10 zikiwamo hati ya helkopta, hati ya usajili wa kanisa, orodha ya wajumbe wa Bodi ya Baraza wa Wadhamini wa Kanisa, idadi ya makanisa anayomiliki na matawi yake.

Alitaja nyaraka nyingine anayotakiwa kuiwasilisha kuwa ni muundo wa utawala wa kanisa,waraka wa maaskofu, return za kanisa, hati za kanisa, nyumba na mali za kanisa pamoj na mpigapicha za video za kanisa.

“Nyaraka zote hizo ametakiwa kuziwasilisha Aprili 16 katika kituo cha Polisi Kanda maalumu ya Dar es Salaam saa 2:00 asubuhi,”alisema mwanasheria huyo.

Awali Askofu Gwajima alisema polisi walimwita leo (jana) kuendelea na mahojiano baada ya kuyasimamisha kutokana na kutetereka kwa afya yake hivi karibuni.

“Mahojiano yameendelea vizuri na yamemalizika salama, lakini mengine mtaambiwa na wanasheria wangu,” alisema Askofu Gwajima.

Askofu huyo alifika kituoni hapo akiwa ameongozana na msaidizi wake Gwandu Mwangasa na mwanasheria wake, Mallya huku akitembea kwa kuchechemea.

Ilipofika saa 1:30 Naibu Kamishna Msaidizi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Siro, aliwaita waumini zaidi ya 20 wa askofu huyo walikuwapo kituoni hapo na kuwauliza maswali mbalimbali.

Siro: Mmekuja kufanya nini?
Waumini: Tumekuja kwa ajili ya askofu wetu.
Siro:Ninachofahamu ni kwamba Askofu Gwajima ameshapewa hati yake ya kusafiria kwenda kutibiwa nje ya nchi, hivyo hapa amekuja tu kuripoti ataondoka.

Gwajima yupo katika mikono salama nendeni mkafanye kazi za uzalishaji… nyie mtakaa hivyo hivyo bila kuzalisha?…mtazalisha saa ngapi kila siku mpo polisi?
Waumini: Sisi tupo akiondoka tunaondoka naye.
Siro: Makubwa haya…!

Baada ya kutamka maneno hayo aliondoka huku akicheka.
Muda ulivyokuwa unazidi kwenda wafuasi hao walikuwa wakiongezeka katika kituo hicho hadi wakafikia zaidi ya 200 huku baadhi yao wakionekana kuvalia vizibao vilivyoandikwa mgongoni ‘Polisi Jamii’.

Hao walilisogelea lango la kuingilia kituoni hapo na kusimama hapo kama walinzi.

Katika mahojiano ya awali, Machi 27 mwaka huu, Askofu Gwajima alizimia na kukimbizwa katika Hospitali ya Polisi katika Muhimbili kabla ya kulazwa TMJ Dar es Salaam.

Siku tano baadaye askofu huyo aliruhusiwa kutoka hospitalini hapo huku akiwa anasukumwa katika kiti cha kubeba wagonjwa(wheel chair)kabla ya kuombewa siku ya Pasaka na wachungaji kutoka Japan.

Baadaye aliweza kusimama na kutembea.

2015-04-09

Sad Neeeeeeeewzzzzzzzzz:WATU 10 WAFARIKI KWA AJALI HANDENI

Muonekano wa eneo la tukio baada ya ajali hiyo. 

Wananchi wakiwa eneo la tukio.

Watu 10 wamefariki dunia katika ajali iliyohusisha magari matatu katika eneo la Mkata kijiji cha Mbweni wilayani Handeni Mkoani Tanga majira ya saa 5 asubuhi ya leo.

Akizungumza na East Africa Radio Kamanda wa kikosi cha usalama barabara mkoa wa Tanga, Mohammed Mpinga amesema kuwa ajali hiyo imehusisha mabasi mawili ya abiria na gari dogo katika barabara ya Dar es salaa kwenda Tanga na Arusha.

Kwa mujibu wa Kamanda gari dogo ilikuwa likitaka kulipita lori lililokua mbele yake na ndipo ilipogongana uso kwa uso na basi la Ratco lililokuwa likitokea Tanga kwenda Dar es salaam. 

Baada ya Basi la Ratco kugonganana na gari dogo, lilipoteza mwelekeo na kugongana tena uso kwa uso na basi la Ngolika lililokuwa likitokea Dar es salaam kwenda Arusha.

Aidha kamanda huyo amesema kuwa kati ya watu 10 waliofariki dunia wanaume watano wakiwemo dereva wa gari dogo na dereva wa basi la Ngorika pamoja na wanawake watano wakiwemo watoto wawili.

Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. 
GPL

Wazazi wa Mtanzania Al-Shabaab


WAZAZI wa Mtanzania Rashid Charles Mberesero (21), anayetuhumiwa kuwa mmoja wa wanamgambo wa Al-Shabaab ambao walifanya mauaji katika Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya na kuua wanafunzi 148, wamefunguka na kueleza siri ya mtoto wao huyo.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, walisema wakati kijana huyo akihusishwa na tukio hilo lililotokea Kaskazini Mashariki mwa nchi hiyo, walikuwa wakijua mtoto wao yupo shuleni mkoani Dodoma.

Akizungumza na MTANZANIA jijini Dar es Salaam jana, baba mzazi wa mtoto huyo, Charles Mberesero, alisema mwanawe huyo ni mwanafunzi wa kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Bihawana iliyopo mjini Dodoma.

Alisema kwa muda mrefu mtoto wake alikuwa akilelewa na mama yake mzazi huko Gonja, Same mkoani Kilimanjaro, lakini kwa muda mfupi alioishi naye hakuwahi kufikiri kwamba angeweza kujihusisha na tukio kama hilo.

“Rashid alizaliwa mwaka 1994 huko Gonja Same, shule ya msingi aliyosoma siikumbuki, lakini sekondari najua kidato cha kwanza hadi cha nne alisoma katika Shule ya Gonja,” alisema.

Akimwelezea tabia yake, alisema Rashid ni kijana mtaratibu na mvumilivu sana.

“Alipokuwa akisoma O’ level nilikuwa nawasiliana naye sana, lakini kama mwaka mmoja na nusu uliopita tulikuwa hatuna mawasiliano ya karibu.

“Sasa hivi alikuwa anasoma PCB kwenye Sekondari ya Bihawana Dodoma. Kwenye matokeo ya kidato cha nne alipata daraja la pili na michepuo yote ya masomo ya Sayansi ilikubali, lakini akaamua kusoma PCB,” alisema na kuongeza.

“Juzi baada ya kutokea hayo yaliyotokea huko Kenya niliongea na mama yake, akaniambia mtoto alikuwa likizo ya kama wiki mbili na Machi 21, mwaka huu aliaga nyumbani kwamba anarudi shuleni Dodoma.

“Na unajua mambo ya huko kijijini baada ya mtoto kusema anasafiri kwenda Dodoma shuleni hakuna mtu aliyefuatilia hadi baadaye tulipokuja kusikia hayo ya Kenya.” Alisema kutokana na alivyoshtushwa na tukio hilo, tangu alivyopata taarifa zake siku ya Jumapili, alipata presha na jana ndipo aliweza kupata ahuweni na kutoka nyumbani.

UHUSIANO WAKE NA MWANAYE
Baba huyo alisema uhusiano wake na mtoto wake haukuwa mzuri sana kwa sababu alimtaka abadilishe dini yake akakataa.

“Nilikuwa namshawishi afuate dini yangu, mimi ni Mkatoliki kwa hiyo kuna wakati alikuja kwangu akakaa kama mwezi mmoja nikawa naenda naye kanisani, nikawa namshawishi abatizwe.

“Alikataa akasema anafuata dini ya mama yake… baada ya kuzaliwa sikumfuatilia sana kwa sababu mama yake aliolewa na mtu mwingine, sasa pale mimi kuzungumza naye kila saa isingewezekana,” alisema.

Alisema katika kipindi cha mwezi mmoja alioishi naye alikuwa akitembea naye muda mwingi, lakini asipokuwapo alikuwa anakaa ndani na pindi akitoka anakwenda msikitini.

SERIKALI ICHUNGUZE SHULE
Mberesero alisema kwa muda aliomjua mtoto wake huyo, anafahamu kwamba si mtu wa kutoka sana nyumbani kwa hiyo anashindwa kujua ni wapi alipojifunzia mambo ya kigaidi.

“Mimi kwa kweli naiomba tu Serikali ichunguze hizi shule ni nini hasa watoto wanafundishwa huko, kwa sababu leo imekuwa ya huyu anayesoma huko Dodoma, juzi hapa tumeona huyo wa Zanzibar.

“Hawa wote ni watoto wadogo, bila ushawishi mkubwa hawawezi kufanya hivi vitu. Mama yake huyu ni mlezi mzuri tu na ana watoto wengine, ni kwa nini tu huyu ndiyo aende huko? Ni lazima Serikali iangalie hili kwa makini,” alisema.

Akizungumza kwa masikitiko, alisema anaamini kwamba mtoto wake huyo alikuwa na akili sana darasani na endapo angeendelea na masomo yake angefika mbali.

“Sijui ameingiaje huku, angekuja kufika mbali sana,” alisema.

MAMA MZAZI ANENA
Akizungumza kwa njia ya simu na gazeti hili, mama mzazi wa Rashid, Fatma Ally, alisema mwaka jana mtoto wake huyo alifaulu mtihani wa kidato cha nne na kupangiwa kujiunga na kidato cha tano katika Shule ya Sekondari Kingwe iliyopo mkoani Dodoma.

Alisema alivyofika kwenye shule hiyo alibaini haikuwa na mchepuo wa Sayansi aliokuwa akisoma, hivyo akaomba kuhama na ndipo alipopata nafasi Shule ya Sekondari Bihawana.

“Kwenye shule aliyopangiwa alikaa kama miezi miwili akisubiri apate nafasi kwingine, shuleni huko alipelekwa na baba yake mlezi na mwezi wa tatu mwaka huu alirudi nyumbani akakaa kama wiki mbili.

“Hakusubiri likizo iishe, akasema kwa sababu sisi ni Waislamu haisubiri Pasaka, nikamwandalia vitu vyake akasema anaenda shuleni,” alisema.

Alisema siku ya Jumapili iliyopita akiwa sokoni, ndipo alipopata taarifa za mwanaye huyo kukamatwa nchini Kenya akihusishwa na ugaidi.

“Nilipigiwa simu na ndugu yangu mmoja akasema amesikia kwenye redio za Kenya kwamba kuna Mtanzania amekamatwa huko kwa ugaidi na ana jina kama la mtoto wangu.

“Baadaye tena baba yake akanipigia simu akinipa taarifa hizo, kwa kuwa Rashid alikuwa ametuaga anaenda shuleni ilibidi tuzungumze na ndugu zetu walioko Dodoma ili waende shuleni kwake pale wajue kama yupo shuleni.

“Walivyoenda huko wakamkosa na walimu wakawaambia kulikuwa na likizo kwa hiyo labda baada ya likizo ndiyo Rashid anaenda shuleni, nilivyosikia hivyo nikajua moja kwa moja kuwa yeye ndiye huyo aliyekamatwa huko Kenya,” alisema.

Mama huy, alisema hali hiyo ilimshangaza na kumpa wakati mgumu kwani anajua kuwa tangu mwanaye huyo azaliwe, hajawahi kutoka nje ya nchi na hata huko Kenya hapafahamu.

“Hata akiwa nyumbani akitoka sana anaenda msikitini, sijui huo ushawishi kaupata msikitini ama huko shuleni,” alisema.
Alisema siku mwanaye huyo anaenda shule, alimpa Sh 90,000 kwa ajili ya nauli na matumizi mengine.

“Hata akiwa shuleni akiniambia ana shida huwa namtumia fedha yoyote niliyonayo, naweza kumtumia Sh 5,000, 10,000 ama 20,000,” alisema.

Gazeti hili lilipotaka kujua kama mama huyo ana mpango wa kwenda Kenya kumwona mtoto wake huyo, alisema hadi sasa haelewi nini cha kufanya.

“Mimi ni mwanamke sijui huko naendaje kwani ile ni nchi ya watu, sijui utaratibu wa kwenda na hata nikienda sijui kama nitaruhusiwa kumwona,” alisema.

UONGOZI WA SHULE
Wakati hayo yakiendelea, waandishi wetu Debora Sanja na Ramadhan Hassan wa mkoani Dodoma wanaeleza kuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Bihawana, Mbilinyi Joseph, alithibitisha kwamba Rashid Charles Mberesero ni mwanafunzi wa shule hiyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana nyumbani kwake, Mbilinyi alisema tangu mwanafunzi huyo alipoondoka wakati wa likizo Novemba 25, mwaka jana hadi sasa hajarejea shuleni.

“Kwa kweli alikuwa ni mwanafunzi wa kawaida, mimi nilikuwa simjui ila kuna siku mimi alinishangaza sana hali iliyonisababisha kumpa adhabu,” alisema.

Alisema siku hiyo akiwa maeneo ya shule majira ya jioni alimkuta kavaa kofia za Waislamu maarufu kama balaghashia, akamwamuru avue na aichane kwa kuwa hakuwa msikitini na shule hiyo ni ya mchanganyiko wa Waislamu na Wakristo.

“Nilipomwamuru vile akasema hawezi kuivua wala kuichana kwa kuwa amezoea kuivaa, majibu hayo yalinipa hofu kweli nikamwambia kesho yake aje ofisini asubuhi.

“Alipokuja ofisini nikamwamuru tena aivue kofia yake na aichane akaniambia hawezi kufanya hivyo kwa kuwa ni kinyume na sheria za dini ya Kiislamu.

“Nikamwambia namrudisha nyumbani akamlete mzazi wake akasema sawa, bado jibu hilo likanishtua pia kwa kuwa hakuonekana kushtuka na adhabu hiyo, nikamwambia aandike barua ya kujieleza akaandika na kudai yupo tayari kuacha shule kuliko kuivua na kuichana kofia ambayo yeye aliita balaghashia,” alisema.

Alisema kutokana na majibu yake akaamua kuwaita walimu wa dini ya Kiislamu wakazungumza nae akakubali kupewa adhabu, lakini cha kushangaza kuanzia siku hiyo hakuonekana tena shuleni.

“Siku aliyoondoka ilikuwa siku ya mtihani ambapo ulikuwa umebaki mtihani mmoja wamalize ili wafunge shule,” alisema.

Mkuu huyo wa shule alisema hawakuwa na jinsi ya kufanya zaidi ya kusubiri siku ya kufungua shule kuona kama atarejea, lakini hakurejea tena.

Alisema hata hivyo hawakuwa na wasiwasi sana walijua anaweza kurudi shule kwa kuwa baadhi ya wanafunzi huchelewe kuripoti shuleni kutokana na sababu mbalimbali.

“Lakini baada ya kupotea shuleni niliwaita tena viongozi wa dini ya Kiislamu ambao ni wanafunzi wenzake, nikawauliza kuhusu Rashid wakasema hata wao wanamshangaa kwa kitendo chake cha kuvaa kofia shuleni,” alisema.

Mkuu huyo wa shule alisema siku tatu baada ya kufunga shule kuna mwanafunzi wa kidato cha sita, Hassan Kissuda alimwomba ampigie simu ambapo alidai alikutana na Rashid Dodoma Mjini akidai anakwenda Kahama.

Alisema Rashid alichukua namba ya simu ya Kissuda akadai atampigia, lakini hakumpigia hadi leo.

“Shule ilipofunguliwa nikatafuta namba ya mzazi wa Rashid katika vitabu vya usajili vya shule nikapiga simu lakini haikupokewa.

“Baada ya kusikia jina la Rashid kwenye vyombo vya habari akihusishwa na tukio la ugaidi Kenya, Aprili 6 mwaka huu nikaipiga tena namba ile ile ikapokewa na baba yake ambaye kumuuliza akasema tukio hilo ni la kweli.

“Hata hivyo baba yake alisema jina la mtoto ni la kweli, lakini picha zinazoonyeshwa kwenye magazeti sio zake, lakini yeye baba yake alikwenda Polisi Makao Makuu akaonyeshwa picha hizo na kuthibitisha kwamba ni mwanaye,” alisema.

Akizungumzia maendeleo ya kitaaluma ya Rashid, alisema hawezi kuyasemea sana maendeleo yake kwa kuwa mwanafunzi huyo alihamia Agosti mwaka jana akitokea Shule ya Sekondari Kigwe.

Kwa mujibu wa matokeo yake ya muhula uliopita alikuwa na wastani wa C.

Alisema yeye kama mkuu wa shule ameshtushwa na tukio hilo kwa kitendo cha shule kukaa na mtu mwenye uwezo wa kuua wenzake na kwamba tukio hilo limechafua shule yao.

“Hili jambo linatisha sana, limeleta hofu kubwa, shule kuishi na Al Shaabab inatisha, ukimwona kijana mwenyewe alikuwa ‘very polite’, lakini hata hivyo yale majibu ya siku ile mimi yalinitisha sana, alikuwa ananijibu kwa upole, lakini majibu makavu,” alisema.

WANAFUNZI WENZAKE
MTANZANIA lilizungumza na wanafunzi wenzake wa kidato cha tano mchepuo wa PCB, ambapo mmoja wao, Lowassa Mayon alidai Rashid alikuwa mbinafsi na hakupenda kuzungumza na wenzake.

“Darasani alipenda kukaa mbele, alikuwa mpole sana na hakupenda kuzungumza na yeyote na ilikuwa ni vigumu mtu kumfuata na kuzungumza nae,” alisema.

AKIRI KUWA AL SHABAAB
Baadhi ya vyombo vya habari vya Kenya vimeripoti kuwa tayari Rashid amekiri kuwa yeye ni mwanachama wa Al Shabaab.

Juzi watu watano walifikishwa mahakamani jijini Nairobi, lakini Rashid ambaye ni mtuhumiwa wa sita, akuwepo mahakamani.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo viliripoti kuwa Rashid anayetambulika sana kama Rehani Dida, hakuwa mahakamani kwa sababu alisafiri na maofisa wa uchunguzi kutafuta ushahidi zaidi baada ya kukiri kuwa yeye ni mfuasi wa Al-Shabaab.

Mwendesha mashtaka Daniel Karuri, aliiambia mahakama kuwa maofisa wa polisi wanafuatilia taarifa za kijasusi zinazohusisha washukiwa hao watano na shambulio la Alhamisi.

Waliofikishwa mahakamani ni Mohammud Adan Surrow ambaye ni mmiliki wa hoteli ambayo magaidi wanadaiwa kuishi kabla ya kutekeleza mauaji hayo.

Osman Abdi Dakane, mlinzi chuoni hapo aliyekamatwa baada ya kuonekana akijaribu kupiga picha waathiriwa wa shambulio hilo huku akiwa anawasiliana kwa simu na watu wasiojulikana.

Mohammed Abid Abikar, Hassan Adan Hassan na Sahal Diriye Hassan wanaodaiwa kuwaletea silaha magaidi, na walinaswa walipokuwa wakijaribu kutorokea nchini Somalia baada ya mauaji hayo.

Mtanzania Anayetuhumiwa Kwa Ugaidi Kenya Kumbe Alitoroka Shuleni Dodoma Tangu Novemba Mwaka Jana.....Mkuu Wa Shule, Wazazi Wake Wafunguka


Mtanzania aliyekamatwa Kenya akidaiwa kufanya ugaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa uliosababisha vifo vya watu 148, Rashid Charles Mberesero (20) ni mwanafunzi wa kidato cha tano, lakini uongozi wa shule anayosoma umesema alitoweka shuleni hapo Desemba Novemba 2014.

Habari zilizothibitishwa na wazazi wake ni kuwa mwanafunzi huyo anasoma katika Shule ya Sekondari ya Bihawana, Dodoma, baada ya kufaulu katika Shule ya Sekondari Gonja mkoani Kilimanjaro.

Mama mzazi wa kijana huyo, Fatuma Ali alisema jana kuwa: “Baada ya kufaulu alichaguliwa kujiunga na Sekondari ya Bihawana na likizo alirudi nyumbani na baada ya likizo kuisha aliniaga anarudi shuleni.”

Taarifa hizo zimekuja wakati Mberesero maarufu kwa jina la Rehani Dida, akitarajiwa kufikishwa mahakamani leo jijini Nairobi baada ya watuhumiwa wengine kufikishwa mahakamani juzi.


Mwendesha mashtaka, Daniel Karuri alisema, “Rehani Dida” hakufikishwa kortini kwani alikuwa na wapelelezi mjini Garissa kukusanya ushahidi zaidi, baada ya kukiri kuwa ni mfuasi wa kundi la Al-Shabaab.

Mtanzania huyo anadaiwa kukamatwa baada ya kujificha kwa saa nane akiwa amejichanganya na maiti, lakini baadaye alipanda na kujificha darini akiwa na mabomu.

Kauli ya wazazi
Jana, mama huyo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa haelewi ni nani aliyemshawishi mwanaye kujiunga na kundi hilo na kwamba jambo hilo limemshtua.

“Hizi taarifa tumezisikia na kuona kwenye TV na kwa kweli zimetushtua sana, mimi nahisi huko shule ndiko alikokutana na watu wabaya,” alisema Fatuma ambaye ni mkazi wa Gonja wilayani Same.

Baba mzazi wa mtuhumiwa huyo, Charles Mberesero Temba, alikiri kuwa Rashid ni mtoto wake ambaye alizaa na Fatuma mwaka 1994 na miaka yote alikuwa akiishi na mama yake.

“Huyo mtoto sijawahi kuishi naye, muda wote tangu 1994 alikuwa akilelewa na mama yake,” alisema Temba na kuongeza kuwa hakuwahi kuishi na mzazi mwenzake huyo.

“Mwaka jana mama yake ndipo alinikutanisha na mtoto na akanitambulisha na mimi nikamshauri abadili dini kwa sababu mimi ni Mkristo Mkatoliki,” alisema.

Alisema aliendelea kuwasiliana naye na aliwahi kumpeleka kanisani mara tatu akimshauri abadili dini ili arudi kwenye dini ya baba, lakini alikataa.

Alisema inavyoonekana ushauri wake huo haukupokewa vizuri na mwanaye na huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mawasiliano baina yao kukatika.

Kutoka Bihawana
Habari zilizopatikana jana kutoka shuleni Bihawana zilisema kuwa Mberesero alitoroka shuleni Novemba mwaka jana, baada ya kukaidi kuvua kofia katika eneo la shule.

Mkuu wa Shule hiyo, Joseph Mbilinyi alisema alimpokea mwanafunzi huyo Agosti 15, mwaka jana akitokea katika Shule ya Sekondari ya Kigwe wilayani Bahi.

Alisema mwanafunzi huyo alipata uhamisho baada ya kubadilisha masomo kutoka masomo ya sanaa mchepuo wa Historia, Jiografia na Kiswahili (HGK) na kuingia katika masomo ya sayansi ya Fizikia, Kemia na Biolojia (PCB).

Mbilinyi alisema katika shule hiyo wanafunzi walikuwa na mazoea ya kuvaa rozali na kofia, jambo ambalo alilipiga marufuku lakini Novemba 24, mwaka jana alikutana na kijana huyo akiwa amevaa kofia.

“Nilimwambia aivue aichanechane mbele yangu, lakini alikataa na kunijibu kuwa amezoea kuivaa na hawezi kuichana.

"Kwa sababu ilikuwa ni usiku niliondoka na kofia hiyo na kumwambia kesho yake asubuhi aje ofisi kwangu ili tumalize suala hilo, alikuwa ni mtu wa kwanza kufika ofisi kwangu.

"Nilimwambia anieleze kwa nini hataki kuichana, ningeweza kumsaidia kumtafutia shule ambazo zinaruhusu mavazi hayo.”

Alisema hata baada ya mazungumzo hayo, Rashid hakueleza kwa nini alikataa kuichana ndipo alipoambiwa kuwa angerejeshwa nyumbani ili aje na mzazi wake na aichane mbele yake.

“Kwa kawaida wanafunzi wengine ukiwaeleza hivyo, huwa wanaomba msamaha yanaisha lakini kwa Rashid ilikuwa ni tofauti, aliniambia yuko tayari kurudishwa nyumbani lakini siyo kuchana kofia hiyo,” alisema.


Mwalimu huyo aliongeza: “Niliona njia ya kumsaidia ni kuwashirikisha walimu ambao wanasimamia msikiti wetu huu. Walimu walimuita na akakubali kupewa adhabu ili jambo hilo liishe bila kufikishwa kwa wazazi wake.”

Hata hivyo, alisema baada ya mazungumzo hayo, Rashid alichukua begi lake na kuondoka kwenda mjini na kuwaacha wenzake wakimalizia mtihani wa Biolojia.

“Nilipata shida sana sikupenda mwanafunzi huyu aondoke shuleni, nilitaka hili jambo lipate suluhu. Nilipigia simu alizoandikisha shule ikiwamo ya baba yake bila mafanikio kwa sababu hazikupokewa, isipokuwa moja ambayo ilipokelewa na mwanamke ambaye alikana kumfahamu.

“Hadi leo bado ni mwanafunzi wetu kwa sababu kanuni zinasema baada ya siku 90 kama mwanafunzi hajaonekana shuleni, tunapeleka jina kwenye Bodi ya Shule ambayo itatoa uamuzi,” alisema.

Katibu mstaafu wa Jumuiya ya Wanafunzi Waislamu katika shule hiyo, Mungi Ramadhan Mungi alisema Rashid alikuwa ni mtu wa msimamo, akitaka jambo lake hata kama halina usahihi analisimamia.

“Aliwahi kutaka kupigana msikitini mara mbili, mara ya kwanza tulikuwa tukiuliza maswali kuhusu masomo ya darasani yeye akasema hairuhusiwi kufanya hivyo msikitini,” alisema.

Alisema hatua hiyo ilizua mabishano na alifikia uamuzi wa kutaka kuwachapa walioongelea mambo ya masomo ndani ya msikitini.

“Alikuwa ni mtu wa msikitini na bwenini mara nyingi hakupenda kuchanganyika na wenzake, jambo hilo lilimfanya hata kukosa marafiki,” alisema.

Alisema aliwahi kuwahadithia kuwa alibadili dini akiwa anasoma sekondari huko Moshi.

Mwalimu anayewasimamia wanafunzi wa Kiislamu, Mohamed Mwijuma alisema baada ya Rashid kutoroka shuleni hapo waligundua alikuwa ni mwanafunzi aliyekuwa na matumizi yasiyo ya kawaida.

“Pia tuligundua kila mwisho wa wiki alikuwa akitoroka kwenda mjini,” alisema Mwijuma ambaye alishiriki kulipatia ufumbuzi tatizo hilo la kukutwa na kofia shuleni.

Hata hivyo, alisema Februari mwaka huu, Rashid alirejea mwisho wa wiki na kuondoka moja kwa moja na mizigo yake yote.

Habari zilizopatikana shuleni hapo zilisema baada ya Rashid kutajwa kuhusika na tukio hilo, mama yake mzazi alifika shuleni hapo kumtafuta mwanaye.

Baada ya Kunusurika Kifo Sauz TEVEZ wa Isha Mashauzi Afanya Dua la Kumshukuru Mungu

Tevez aliwakusanya ndugu, jamaa na marafiki na kufanya dua hiyo, Ijumaa iliyopita nyumbani kwao Msamvu, Madawa jirani na Shule ya Msingi Msamvu ‘A’ ambapo alifanya kisomo hicho kilichoambatana na dua na chakula.

“Mungu amemnusuru na balaa lile, amemkingia hivyo ameona ni vyema aandae dua ya kumshukuru,” alisikika mmoja wa waalikwa.Baadhi ya mashehe na waumini wengine wa Kiislamu waliohudhuria dua hiyo walimpongeza Tevez kwa kitendo hicho cha kumkumbuka Mungu na kumshukuru kwa kumlinda na majanga yaliyomkuta.

“Hili ni jambo jema sana alilofanya Tevez ambapo tunaelekezwa na mitume wetu kwamba tumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema mmoja wa waumini wa dini ya Kiislamu.Kwa upande wake Tevez alisema amamshukuru Mungu kwani amempigania sana uhai wake.

“Lilikuwa ni tukio kubwa kwangu, sikutegemea kama ningenusurika, Mungu amenipigania sana nimeona bora nijumuike na ndugu, jamaa na marafiki kumshukuru Mungu,” alisikika Tevez.Januari mwaka huu, Tevez alitekwa na watu wasiojulikana katika mji wa Durban nchini Afrika Kusini ambapo mwenyewe alibainisha kuwa mwenyeji wake mjini humo alivujisha habari kuwa ana fedha ndipo akavamiwa, akateswa na kuporwa fedha na simu zake mbili

Tevez aliwafungulia mashtaka vijana waliohusika na tukio hilo ambapo kesi inaendelea kuunguruma nchini humo.

ALA PASAKA KWA KICHAPO TAKATIFU ............ubongo wa nyuma wafumuka

Anton akivuja damu baada ya kupewa kichapo kikali kutoka kwa wananchi wenye hasira kali kwa kosa la wizi.  
Kijana mmoja aliyetambuliwa kwa jina moja la Anton, Jumapili ya Pasaka alikula sikukuu kwa kupewa kichapo na wananchi wenye hasira kwa madai kuwa ni kibaka.Tukio hilo lililotokea saa 12 asubuhi maeneo ya Sinza Afrikasana ambapo walioshuhudia tukio hilo walimwambia mwandishi wetu kuwa, kijana huyo aliyefahamika mtaani hapo kama muokota chupa, ilidaiwa kuwa alikurupushwa kutoka katika nyumba moja ambako alienda kwa gia ya kuokota chupa, akataka kukwapua kitu.

“Baada ya kukurupushwa katika nyumba hiyo, kijana huyo alitoka mkuku mpaka katika nyumba moja ambako alimkuta dada mmoja akifagia na kuingia ndani ya geti kisha kujifungia,” alisema shuhuda mmoja.

Baada ya muda wakatokea watu waliomkurupusha ndipo dada huyo akawaambia kuwa mtuhumiwa wao ameingia ndani baada kulikuta geti hilo wazi wakati akifanya usafi na alikuwa amejifungia kwa ndani.

Habari hiyo iliwafanya baadhi ya vijana kudandia geti ili kuingia ndani, hata hivyo, kijana huyo alipoona watu hao wakiruka getini naye akaruka ukuta upande wa pili na kukimbia.
Akipakizwa kwenye gari safari kuelekea kituoni.

Lakini juhudi zake hizo za kutaka kutoroka hazikuzaa matunda kwani alidakwa hatua chache kutoka kwenye ukuta wa ua wa nyumba hiyo na kuanza kula kichapo kikali ambacho kilisababisha kuchanwa kichwani na damu nyingi ‘kumwagika.’

Kijana huyo aliokolewa na askari polisi waliokuwa doria wakiongozwa na Kamanda Rashidi wa Kituo cha Polisi Mabatini waliokuwa katika gari yao ya doria. 

Moja ya jeraha kubwa alolipata kichwani baada ya kichapo. Kamanda huyo na askari wenzake walifanya kazi kubwa kuzuia raia wasilete madhara zaidi kwa kijana huyo huku wakiwaambia wananchi kuwa siyo busara kujichukulia sheria mkononi, walimkamata wakampeleka kituoni kwa hatua zaidi.
GPL

Wizi noma!!!!!!!!! ANASWA AKIIBA MAHINDI, ALAZIMISHWA KULA MABICHI!



Akilazimishwa kula mahindi hayo.

Jamaa ambaye jina halikuweza kupatikana mara moja, amejikuta akionja joto ya jiwe baada ya kudaiwa kukutwa akiiba kwenye shamba la mahindi hivyo kulazimishwa kula mahindi mabichi.Tukio hilo la aina yake lilijiri hivi karibuni kwenye Kata ya Miembeni, Bukoba mkoani Kagera na kuibua gumzo kubwa.

Kwa mujibu wa shuhuda wetu, baada ya kumnasa kijana huyo akiiba mahindi aliyoyajaza kwenye gunia, wamiliki wa shamba hilo walimuamuru kukaa chini na kuyala yakiwa mabichi hadi yaishe, kitendo ambacho jamaa huyo alikubaliana nacho. 


Akila mahindi hayo ili kuepuka kichapo.

Ilielezwa kwamba, katika hali ya kushangaza, kijana huyo hakukataa wala kuonesha kutetereka kwani alianza kuyala hadi alipoamriwa kuacha na kuambiwa aondoke.Katika habari hiyo iliyoripotiwa na Mtandao wa Harakati, kijana huyo alionekana kuwa na matatizo ya kutosikia vizuri wala kuongea kwa maana ya kuwa ni ‘bubu’. Hata hivyo, kijana huyo hakujulikana alitokea wapi kwani mbali na madai ya wizi na ububu pia hakuonekana mwenye ufahamu mzuri kutokana na mavazi aliyokuwa amevaa.
GPL

Kova: Ole wenu wafuasi wa Gwajima


Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limetoa onyo kwa wafuasi wa Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima ambao leo wamepanga kumsindikiza kiongozi wao kwenda katika mahojiano na jeshi hilo.

Hatua ya wafuasi hao kutaka kumsindikiza kiongozi huyo, imekuja baaada ya kutangaziwa kujitokeza kwa wingi wakiwa katika kanisa hilo lilipo Kawe, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleimani Kova, alisema Askofu Gwajima anaruhusiwa kwenda katika mahojiano na wanasheria pamoja na wasaidizi wake wasiozidi watano tu.

“Ni bora wafuasi hao wakaendelea na shughuli zao za kawaida zikiwamo za uzalishaji mali kuliko kurundikana katika geti la polisi kwa sababu watakaofika kituoni hapa bila kuitwa watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Kova.

Alisema kutokana na hali hiyo, hawategemei kuona mrundikano katika maeneo hayo kwani kufanya hivyo ni kusababisha mkusanyiko usiokuwa na kibali.

Kwa upande wake, mwanasheria wa Gwajima, John Mallya, alisema mpango wa waumini wa kanisa hilo kumsindikiza kiongozi wao upo pale pale.

“Waumini wataenda kama kawaida kumsindikiza kiongozi wao kwa hiyo mpango huo utabaki pale pale kama walivyotangaziwa,” alisema Mallya.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Askofu Gwajima alifikishwa kituoni hapo kwa tuhuma za kutoa maneno ya kashfa dhidi ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Akiwa katika mahojiano, Askofu Gwajima alianguka na kuzimia hali iliyosababisha kukimbizwa katika hospitali ya polisi iliyopo Kurasini na baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Baadaye alipelekwa na kulazwa katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam kabla ya kuruhusiwa kutoka hospitalini hapo huku akiwa anasukumwa katika kiti cha wagonjwa.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...