Showing posts with label SANAA NA MICHEZO. Show all posts
Showing posts with label SANAA NA MICHEZO. Show all posts

2015-04-08

Azam, Yanga SC kuendeleza libeneke



VITA ya ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kati ya Yanga na Azam inatarajiwa kuendelea tena leo, pale timu hizo zitakapoteremka kwenye viwanja tofauti kusaka pointi tatu.

Yanga, ambao ni vinara wakiwa na pointi 40, watakuwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini hapa, wakivaana na Wagosi wa Kaya, Coastal Union, mchezo unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake. 

Mabingwa watetezi wa ligi, Azam FC, wenye pointi 36, wataikaribisha Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex, mchezo unaotarajiwa kukumbushia historia ya msimu uliopita pale timu hizo zilipotoa sare ya mabao 3-3 na kuonyesha burudani safi ndani ya dimba hilo.

Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kutinga raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwa kuichapa mabao 5-2 FC Platinum ya Zimbabwe, vile vile Yanga imeshinda mechi tatu zilizopita za ligi. 

Kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Yanga iliweza kuifunga Coastal kwa bao 1-0, bao lililofungwa na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwa kichwa.

Coastal Union, inayoshika nafasi ya tano kwa pointi 24, haijafanikiwa kushinda mchezo wowote tokea Februari 28, mwaka huu, ilipoifunga Mgambo JKT bao 1-0, hadi inakutana na Yanga leo imeambulia sare mbili dhidi ya Kagera Sugar (2-2) na Ruvu Shooting (1-1) pamoja na vipigo viwili ilipocheza na Azam (1-0) na Tanzania Prisons (1-0).

2015-03-31

Mashabiki kanda ya Ziwa wastaarabu.



Shirikisho la mpira wa miguu nchini Tanzania (TFF) limesema linawashukuru mashabiki wa kanda ya ziwa kwa kuangalia mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Malawi (The Flames) kwa ustaarabu wa hali ya juu bila kufanya vurugu.

Mchezo huo wa kirafiki wa Kimataifa uliofanyika Jumapili jijini Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba na mashabiki wapatao 15,762 walihudhuria.

Afisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto amesema ustaarabu wa mashabiki ulioonyeshwa ni wa hali ya juu katika michezo.

Vurugu zimekuwa zikitokea katika mechi kadhaa za mpira wa miguu viwanjani kwa mashabiki au wachezaji kutokubaliana na maamuzi ya marefa.

Mechi hiyo imeingiza kati ya wenyeji timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya timu ya Taifa ya Malawi (The Flames) umengiza jumla ya shilingi 73 milioni.

2015-03-30

Ngasa Aendelea Kuipasua Kichwa Yanga..Sasa Anataka Mshahara wa Mil 6 kwa Mwezi la Sivyo...






YANGA imetamka kuwa haina lengo la moja kwa moja kuachana na mshambuliaji wao Mrisho Ngassa na katika kuthibitisha hilo kwa vitendo, tayari uongozi wa klabu hiyo umeweka mezani Sh. 80 Milioni wakimtaka asaini dili jipya la kumbakisha timu hiyo. 

Mmoja wa mabosi wa klabu hiyo aliyeko katika kamati ya usajili amesema kuwa uongozi wao chini ya mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji hauna nia ya kutaka kumtosa Ngassa ambapo tayari wameshampatia ofa hiyo kuhakikisha anasaini mkataba mpya. 

Bosi huyo alisema katika ofa hiyo, Ngassa amepewa masharti mawili muhimu ambapo ametakiwa kutumia sehemu ya fedha hizo kumaliza deni lake la benki analodaiwa huku mshahara wake wa Sh. Mil. 4 ukibaki kama ulivyo. 

Hata hivyo sharti hilo la mshahara linaenda tofauti na ofa ambayo Ngassa alitaka kupatiwa na klabu hiyo akitakia alipwe dola 3,500 (Sh. Mil 6.5) kwa mwezi ombi ambalo uongozi wa Yanga umeligomea. 

“Hatuna nia ya kumuondoa Ngassa kuna vitu ambavyo anakosea, anaongea sana, haangalii kwamba juhudi zetu tunazozifanya tumeshampatia ofa hiyo afikirie sasa kama kweli anataka kubaki hapa,” alisema bosi huyo. 

“Tumempa hiyo ofa lakini tatizo lake ni moja anataka mshahara mkubwa sana, kiasi ambacho ametaka tumpatie ni kikubwa sana kama atakuwa muelewa katika hili atakubali kusaini.” 

Ngassa amekuwa akionekana kujuta kwa maamuzi yake ya kukataa ofa ye kwenda El Merreikh ya Sudan iliyomtaka wakati akiwa Simba kwa mkopo akitokea Azam ili tu akipige Yanga na kukumbana na adhabu ya kuwalipa Wekundu wa Msimbazi fedha alizosaini awali kabla ya kukimbilia Jangwani..
~udakuspecially

Twiga Stars imeonyesha wanawake Tanzania wanaweza



Aprili 10, Timu ya Taifa ya Soka ya Wanawake (Twiga Stars) itaikabili Zambia kwenye mchezo wa marudiano wa kusaka tiketi ya kushiriki Michezo ya Afrika iliyopangwa kufanyika Kongo-Brazaville Septemba.


Twiga Stars inaingia katika mchezo huo ikiongoza kwa mabao 4-2, ushindi ilioupata kwenye mchezo wa kwanza uliofanyika Lusaka, Zambia.


Tunaipongeza timu hiyo kwa ushindi huo mnono tena wa ugenini ambao unaipa fursa nzuri ya kukata tiketi ya kushiriki katika michuano hiyo.


Hata hivyo, licha ya ushindi huo, ushiriki wa kina dada hawa katika michuano hiyo mikubwa ya kimataifa bado ni kitendawili.


Kitendawili hili kinatokana na migongano ambayo tumeiripoti kwenye gazeti hili Jumamosi iliyopita ikihusisha wizara inayosimamia michezo pamoja na vyama washirika wake, Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).


Hatupendi kuingia kwenye undani wa suala hilo, lakini tunaingiwa na wasiwasi kutokana na kauli ya Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi kwamba ofisi yake ambayo ndiyo inayoratibu Michezo ya Afrika haina habari za ushiriki wa timu hiyo. Tunaamini msuguano huo ambao gazeti hili liliiuripoti utakuwa umepatiwa suluhisho ifikapo au kabla ya Aprili 10 wakati wa mchezo huo wa marudiano.


Tunashauri suala hilo litafutiwe suluhu mapema ili lisiwaathiri vijana wetu hao.


Tunaamini kwamba kushiriki kwake kungesaidia kujenga msingi wa mchezo huo. Tunasema, timu hiyo haina msingi kwa sababu soka ya wanawake katika nchi yetu licha ya kutambuliwa na TFF kiasi cha kuwa na chama chake, lakini ni kama haina mwenyewe.


Tunasema hivyo, kwani hakuna klabu za kutosha kuwezesha kuwapo kwa ligi za aina yoyote ambazo zingetumika kusaka au kupata wachezaji wanaofaa kuichezea Twiga Stars.


Wachezaji hao wa kuokoteza kila yanapotokea mashindano na ukosefu wa ligi ya soka ya wanawake, ndicho kilio kinachotufanya tufikiri kwamba mafanikio yake katika hatua kama hii ingekuwa chache ya kuuendeleza mchezo huo.


Ni katika muktadha huo, tunakitaka chama hiki kinachosimamia mchezo huo kwa wanawake na TFF kwa jumla, kusimama kidete kuhakikisha timu hii inashiriki katika michuano hiyo.


Baada ya hapo, tunapenda kukikumbusha chombo hicho kinachosimamia soka kwamba, umefika wakati wa kujenga msingi wa kuendelea mchezo huo kwa kina mama hivyo kianze maandalizi tangu ngazi za chini waliko wasichana, shule za msingi, sekondari hadi vyuo.

2015-03-26

Falcao kuondoka Manchester United


MSHAMBULIAJI wa timu ya Manchester United raia wa Colombia, Radamel Falcao, amesema mwisho wa msimu ataondoka katika klabu hiyo na kutafuta sehemu ambayo ataweza kupata nafasi ya kucheza.


Mchezaji huyo ambaye alijiunga na klabu hiyo kwa mkopo akitokea klabu ya Monaco, bado hajaonesha uwezo wake chini ya kocha, Louis van Gaal, ambapo mpaka sasa amefanikiwa kufunga mabao manne msimu huu katika ligi.

Falcao amekuwa akitokea benchi tangu Februari katika mchezo dhidi ya Liverpool na Arsenal, ambapo kutokana na hali hiyo, ameona bora aanze kusuka mipango ya kuondoka na kutafuta timu ambayo atapata nafasi ya kucheza.


“Baada ya ligi kwisha, bila shaka nitakaa chini na kuamua wapi niweze kwenda kwa ajili ya kuendeleza soka langu, naweza kusema sijapata nafasi ya kutosha katika klabu hii ya Manchester United na kwa sasa imesalia michezo nane hivyo chochote kinaweza kutokea.”

Falcao amesema hana ugomvi wowote na kocha wake japokuwa anawekwa nje, ni sawa na makocha wengine katika klabu mbalimbali.

Yanga haikamatiki



Usemi wa Kiswahili kwamba bega haliwezi kushinda kichwa umetimia jana kwa kocha wa JKT Ruvu, Fred Felix Minziro aliposhindwa vishindo vya Yanga na timu yake kufungwa mabao 3-1. 


Kwenye mchezo huo wa kiporo wa Ligi Kuu, mshambuliaji Simon Msuva alifunga mabao mawili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam yaliyomfanyam kumpiku Didier kavumbagu wa Azam mwenye mabao kumi.


Kavumbagu alikuwa akiongoza katika orodha ya ufungaji kwa muda mrefu.


Naye Danny Mrwanda alifunga bao lake la kwanza tangu alipojiunga na Yanga akitokea Polisi Morogoro kwenye dirisha dogo la usajili wakati Samwel Kamuntu aliifunga JKT bao la kufutia machozi.


Ushindi huo umeifanya Yanga ijikite kileleni mwa ligi kwa pointi 40, ikifuatiwa na Azam (36) na Simba ni ya tatu ikiwa nazo 32.


Yanga ilianza mchezo kwa kasi na dakika ya kwanza Msuva alikosa bao baada ya shuti lake kutoka nje baada ya kuwatoka mabeki wa JKT Ruvu.


Naye Mrisho Ngassa alikosa bao, dakika ya 20, akiwa na kipa Benjamin Haule, baada ya kupiga shuti lilitoka nje.


Yanga ilitawala kiungo, kutegeneza nafasi nyingi kwa washambuliaji ambao waliiweka safu ya ulinzi wa JKT Ruvu kwenye wakati ngumu.


Kasi hiyo ilizaa matunda dakika ya 34, wakati kiungo wa JKT Ruvu, Jabir Aziz aliposhika mpira kwenye eneo la penalti na mwamuzi Isihaka Shirikisho kutoa adhabu ya penalti iliyofungwa na Msuva.


Mrwanda alifunga bao lake la kwanza akiwa Yanga dakika ya 42, baada ya kugongeana pasi na Ngassa na kupiga shuti lililomshinda kipa Haule na kujaa wavuni.


Baada ya bao hilo wachezaji wa Yanga walionekana kuridhika na matokeo hayo na kuwaacha JKT Ruvu kujipanga na kufanikiwa kupata bao dakika ya 45, lililofungwa na Kamuntu, akimalizia pasi ya Idd Mbaga na kufanya matokeo kuwa 2-1 hadi mapumziko.


Wakati timu zinakwenda mapumziko mabeki wa Yanga, Juma Abdul na nahodha Nadir Haroub walishikana mashati wakitaka kupigana wakilaumiana kwa uzembe uliosababisha bao la JKT Ruvu.

2015-03-24

Goran: Saa 456 za Simba kutwaa ubingwa


Kocha wa Simba, Goran Kuponovic amesema bado kuna saa456 za timu yake kupigana na kuhakikisha anachukua ubingwa wa LigiKuu Tanzania Bara msimu huu.

Simba iliyoanza ligi kwa kusuasua sasa imefikisha pointi 32 baada yakucheza mechi 20 ikiwa nyuma ya pointi tano kwa vinara Yanga (37), nana Azam yenye pointi 36.

Akizungumza mara baada ya timu yake kupata ushindi wa mabao 3-0dhidi ya Ruvu Shooting juzi, kocha Goran alisema bado ana matumainimakubwa ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bbara katika saa 456 zilizosalia.

“Tuna uwezo wa kukimbiza kijiti cha ubingwa, saa 456 mechi zilizosaliambele yetu tuna mkakati wa kuhakikisha tunashinda kama tulivyofanyavizuri kwenye mchezo na Ruvu, kama tutaendelea kushinda hivi, lolotelinaweza kutokea mwisho wa msimu,” alisema Goran.

Simba imebakiza mechi dhidi ya Kagera itakayofanyika Shinyanga,Mgambo itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa na baadaye itaifuataMbeya City kabla ya kumalizia mechi tatu kwenye Uwanja wa Taifadhidi ya Ndanda, Azam na JKT Ruvu.

Hata hivyo ili Simba iweze kuchukua ubingwa itabidi iziombee Yanga naAzam dua mbaya ili zipoteze katika mechi zao zilizosalia.Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi amewaambia wenzakehakuna kukata tamaa na wala wasiyumbishwe na maneno ya kejeli yawatani zao Yanga kwani mpira una maajabu yake.

Yanga kila mara wamekuwa wakiwambia Simba wao si saizi yao kwakuwatoa katika mbio za ubingwa na kudai kuwa watu pekeewanaopambana nao katika kuwania ubingwa msimu huu ni Azam tu.

Hata hivyo,Okwi anaamini maneno hayo ni kama kelele za chura tu nahamzimzuii Tembo kunywa maji na amewaambia wenzake wakomae,wapambane kwani hiyo ni ligi na lolote linaweza kutokea na kelele zawapinzani wao zisiwasumbue kabisa.

Okwi alisema licha ya kucheza mechi mbili zaidi ya wapinzani wao wamebakiza mechi sita pekee ambazo ni ngumu, lakiniwatapambana mpaka dakika ya mwisho na mbivu na mbichi zitajulikana.


Alisema wanachotakiwa ni kutowaangalia wapinzani wao baliwahakikishe wanashinda michezo yote sita ikiwemo ya ugenini dhidi yaKagera Sugar na Mbeya City na mwisho wa ligi watafanya mahesabukujua wako katika nafasi gani.

“Najua ligi imekuwa ngumu na kuna wengine wameshatutoa katikakuwania ubingwa, lakini hayo ni maneno tu na hatupaswi kuyumbishwa nakejeli zao, tunakomaa na tutaendelea kupambana hadi mwisho.

“Ndio maana ikaitwa ligi, kwamba ubingwa hauna mwenyewe, haowanaongoza tu, lakini bado ligi haijaisha na huwezi kujua ya mbele,unaweza ukapanga hivi na mambo yakageuka, hivyo lolote linaweza kutokea na ndio maana nasema hakuna kukata tamaa hapa"alisema Okwi.

2015-03-23

JOSEPH MAHUNDI WA COSTAL UNION AKABIDHIWA KOMBE NA KITITA CHAKE NA VODACOM TANZANIA

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia (kushoto) akimkabidhi kombe na hundi yenye thamani ya shilingi Milioni 1/- kwa kuwa mchezeji bora wa Mwezi Desemba 2014 wa (VPL) kabla ya mechi kati ya timu yake na Azam FC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa Jumapili. Aliyeshikilia hundi kulia ni Ofisa Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Kaude. 

Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia (kushoto) akiwa ameshikilia hundi yenye thamani ya shilingi Milioni 1/- ya mchezeji bora wa Mwezi Desemba 2014 wa (VPL), kulia Ofisa Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Kaude.

Na Mwandishi Wetu, Tanga
KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania, imemjaza noti kiungo Joseph Mahundi wa Coastal Union baada ya mwishoni mwa wiki kumkabidhi Sh. Milioni 1/-kutokana na kufanya vizuri katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu.

Mahundi, kiungo fundi aliyekulia kwenye kituo cha Azam FC jijini Dar es Salaam, aliibuka Mchezaji Bora wa Mwezi Desemba 2014 wa VPL akiwa ni mchezaji wa nne kutwaa tuzo hiyo tangu ianzishwe msimu huu na kampuni hiyo.


Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia aliyekuwa amefuatana na Ofisa Udhamini na Matukio wa Vodacom Tanzania, Ibrahim Kaude, ndiye aliyekabidhi zawadi hiyo kwa Mahundi dakika chache kabla ya kuanza kwa mechi ya VPL ya Coastal dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini hapa Jumapili.

Baada ya mechi hiyo kumalizika huku Azam FC wakiibuka na ushindi wa bao 1-0, Mahundi aliipongeza Vodacom Tanzania kwa kuanzisha tuzo hiyo.

"Ninawashukuru na kuwapongeza Vodacom kwa kuanzisha tuzo hii kutambua mchango wa wachezaji wanaofanya vizuri VPL. Ninawashukuru pia TFF kwa kuona kutambua uwezo wangu na kunitangaza mshindi wa Desemba. Nitaendelea kujituma zaidi ili nikuze soka langu na kuisaidia Coastal Union," alisema Mahundi.

Matina Nkurlu, Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, alisema kuwa kampuni hiyo itaendelea kutoa zawadi kwa wachezaji wanaofanya vizuri ikiwa ni sehemu ya mikakati na mchango wake katika kuinua kiwango cha michezo, hususan mpira wa miguu nchini.

Tangu tuzo hiyo ianze kutolewa Septemba mwaka jana, ni Coastal Union pekee iliyofanikiwa kutoa wachezaji wawili walioitwaa hadi sasa.

Washindi wa tuzo hiyo tangu ianzishwe ni Antony Matogolo wa Mbeya City (sasa yuko kwa mkopo Panone FC ya Kilimanjaro) aliyeitwaa Septemba, Salum Abubakar 'Sure Boy' wa Azam FC (Oktoba), Rashid Mandawa wa Kagera Sugar (Novemba), Mahundi, Said Bahanunzi wa Polisi Moro (Januari) na Godfrey Wambura wa Coastal Union (Februari). 

GPL

Reina: Asimama golini ligi kubwa nne Ulaya


Ligi hizo ni La Liga (Hispania), Premier League (England), Serie A (Italia) na Bundesliga (Ujerumani).

Kipa wa Bayern Munich ya Ujerumani, Pepe Reina amekuwa wa kwanza katika historia ya soka la Ulaya kucheza katika ligi nne kubwa barani Ulaya.

Ligi hizo ni La Liga (Hispania), Premier League (England), Serie A (Italia) na Bundesliga (Ujerumani). 

Reina (32), ambaye ni raia wa Hispania, wiki iliyopita aliichezea timu yake ya Bayern Munich mechi ya kwanza katika Bundesliga tangu asajiliwe msimu uliopita wakati timu hiyo ilipocheza na Werder Bremen kwenye Uwanja wa Weserstadion.

Katika La Liga, kipa Reina alicheza mechi 100, akiwa na klabu za Barcelona na Villarreal.

Mwaka 2005 alihamia klabu ya Liverpool inayoshiriki Ligi Kuu England na kucheza mechi 284 katika misimu minane. 


Klabu ya Liverpool ilimpeleka Reina katika klabu ya Napoli ya Italia kwa mkopo katika msimu wa 2013/2014 na huko alicheza mechi 29.

Katika msimu uliopita, Reina alichukuliwa na klabu ya Bayern Munich kama mchezaji huru, lakini alikuwa akipata wakati mgumu wa kucheza kwa sababu timu hiyo ina kipa mahiri, Manuel Neuer.

Wiki iliyopita, kocha wa Bayern Munich, Pep Guardiola ambaye ni raia wa Hispania alimpa nafasi ya kucheza Mhispania mwenzake kipa Pepe Reina, hivyo kipa huyo kuweka rekodi ya kucheza ligi nne kubwa barani Ulaya ambazo ni La Liga, Premier League, Serie A na Bundesliga.

Reina ambaye ana watoto watano, ni kipa ambaye akiwa na timu ya taifa ya Hispania alitwaa ubingwa wa Fainali za Kombe la Dunia 2010 na ubingwa wa Ulaya 2008, 2012.

Alipokuwa na Klabu ya Liverpool, alitwaa Kombe la FA msimu wa 2005/06, Kombe la Ligi, 2011/12, Ngao ya Jamii 2006 na UEFA Super Cup, 2005.



Mwananchi

Kiungo Yanga apoteza fahamu uwanjani


Kiungo mkabaji wa Yanga, Said Juma Makapu akitolewa uwanjani baada ya kuanguka na kupoteza fahamu.



FURAHA ya wachezaji wa Yanga juu ya ushindi wao dhidi ya Mgambo JKT ilizimika ghafla baada ya kiungo mkabaji wa timu hiyo, Said Juma Makapu kuanguka na ‘kuzimia’ akiwa uwanjani.Katika mchezo huo ambao Yanga walipata ushindi wa mabao 2-0 yaliyofungwa na Amissi Tambwe na Simon Msuva, kiungo huyo alipata majanga hayo baada ya kugongana na kiungo wa Mgambo wakiwa hewani kuwania mpira.

Baada ya tukio hilo lililotokea dakika ya 90 ya mchezo huo, kiungo huyo alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo kwa gari maalum la wagonjwa ili kufanyiwa ‘check up’ zaidi.

Championi lililoweka kambi mkoani Tanga, lilifika hospitalini hapo na kumkuta kiungo huyo akiwa kimya kitandani, ambapo alikuwa amezinduka dakika chache kisha kupewa maji na daktari wake, Juma Sufiani.
Akizungumza na Championi Jumatatu hospitalini hapo, Sufiani alisema kuwa mchezaji huyo alipata mshtuko kutokana na kugongwa kichwani, lakini afya yake inazidi kuimarika, jana alitarajiwa kusafiri na basi la timu kurejea jijini Dar.

“Alipata mshtuko mkubwa pale uwanjani, unajua aligongwa kichwani sehemu ambayo ni muhimu kwa binadamu yeyote, ndiyo maana hali hiyo ilitokea.“Kama unavyomuona, angalau anaendelea vizuri kwa sababu anazungumza sasa ingawa kwa shida sana, Mungu akipenda kesho tutasafiri naye kurejea Dar kwa uchunguzi zaidi wa kitabibu,” alifafanua Sufiani.

Simba yachinja Ruvu



Wachezaji wa Simba wakishangilia goli.


BAADA ya kupoteza mechi iliyopita dhidi ya Mgambo, vijana wa Msimbazi, Simba, jana waliamka na kutoa kipigo kikali kwa Ruvu Shooting cha mabao 3-0 katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kutokana na ushindi huo, Simba imefikisha pointi 32 na kuendelea kubaki katika nafasi ya tatu ikiwa ni nyuma ya vinara wa ligi, Yanga ambao wana pointi 37 huku Azam FC wakishika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 36 baada ya nao kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jana.

Simba ilipata mabao yake kupitia kwa Ibrahim Ajibu aliyefunga kwa penalti baada ya Awadhi Juma kuchezewa faulo ndani ya eneo la hatari katika dakika ya 60.Awadhi ambaye aliingia uwanjani kuchukua nafasi ya Abdi Banda, alifunga bao la pili kwa shuti kali lililombabatiza beki wa Ruvu, Hamis Kasanga katika dakika ya 61 na kujaa wavuni.

Elias Maguri ambaye naye aliingia kuchukua nafasi ya Emmanuel Okwi, aliipatia Simba bao la tatu katika dakika ya 75 kwa kumalizia mpira ambao ulitemwa na kipa wa Ruvu, Abdallah Abdallah aliyepangua shuti kali la Said Ndemla.

Licha ya kupata mabao hayo, Simba ilishindwa kutumia nafasi nyingi ilizopata katika kipindi cha kwanza kutokana na washambuliaji wake kukosa umakini.Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Simba, Goran Kopunovic alisema:

“Vijana wangu hawakutumia nafasi vizuri kipindi cha kwanza, niliwapa maelekezo ya nini cha kufanya wakati wa mapumziko na wakayafanyia kazi, tumejipanga kushinda mechi zote zilizosalia.”Upande wa Kocha wa Ruvu, To, Olaba alishindwa kuzungumzia mchezo huo akidai kuwa hakuwa katika hali nzuri.

Simba, Azam mdogo mdogo


Kipa wa timu ya Ruvu Shoooting , Abdullah Abdallah akijaribu kuokoa mpira langoni mwake huku mshambuliaji wa Simba ,Emmanuel Okwi (katikati) akifuatilia wakati wa mchezo wa ligi kuu Tanzaia Bara uliofanyika kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana.Simba ilishinda 3-0.


Timu ya Simba imerudi katika kinyang’anyiro cha kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting 3-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Pia, Azam inaipumulia Yanga kileleni baada ya jana kuichapa Coastal Union bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Kwa ushindi iliopata, Simba imefikisha pointi 32 na kuendelea kushika nafasi ya tatu huku Azam ikibaki katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 36 wakati Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 37.

Katika mechi ya jana, Simba ilikubali kulazimishwa na Ruvu kwenda sare mpaka mapumziko lakini katika kipindi cha pili iliamka na kupata bao la kwanza dakika ya 58 ambalo lilifungwa na Ibrahim Ajib kwa mkwaju wa penalti.

Simba ilipata penalti hiyo baada ya Awadhi Juma ambaye aliingia kuchukua nafasi ya Abdi Banda kuchezewa faulo na Pius Michael katika eneo la hatari.

Dakika mbili baadaye, Awadhi aliipatia Simba bao la pili kwa kichwa huku Elius Maguli akihitimisha mabao ya Simba katika dakika ya 76 baada ya kipa wa Ruvu, Abdullah Abdallah kutema shuti kali la Said Ndemla.

Katika kipindi cha kwanza, timu zote zilicheza kwa kushambuliana kwa zamu, lakini kipindi cha pili Simba ilitulia na kumiliki sehemu kubwa ya mchezo iliyowawezesha kuibuka na ushindi huo.

Akizungumza baada ya mechi hiyo kumalizika, kocha wa Simba, Goran Kopunovic alisema, “Tumepata ushindi wa kishindo, bado tuna uwezo wa kukimbia katika mbio za kuwania ubingwa.”

Katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, bao la Azam lilifungwa na John Bocco katika dakika ya 32 baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Coastal na mpira kumrudia Shomary Kapombe wa Azam aliyepiga shuti na kuwagonga mabeki wa Coastal na mpira kumkuta Bocco aliyeuweka kimiani.

Azam ilitwala mchezo kwa muda mwingi, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini kutumia vizuri nafasi walizokuwa wakizipata.

Akizungumza baada ya mechi, kocha msaidizi wa Coastal, Jamhuri Kihwelu alisema, “Nasikitika kufungwa na timu mbovu kama Azam, hawajui kucheza mpira ingawa wana kila kitu, bahati haikuwa yetu.”

Kocha wa Azam, George Nsimbe alisema, “Mimi nautaka ubingwa, haijalishi nimeifunga timu gani, kikubwa ni pointi tatu katika mechi ya Ligi Kuu, hata mechi ijayo nitashinda, ninaamini wachezaji wangu watanipa matokeo mazuri katika mechi zote zilizobaki.”

2015-03-20

Tutawapwelepweta, Barcelona vs Real Madrid



SIRI ni moja ni kuwa kama Real Madrid inahitaji kutwaa ubingwa wa La Liga msimu huu basi inatakiwa kuhakikisha haipotezi mchezo wa keshokutwa Jumapili dhidi ya Barcelona kwenye Uwanja wa Camp Nou.

Takwimu zinaonyesha kuwa mechi za miaka ya hivi karibuni baina ya timu hizo ambayo inajulikana kwa jina la El Clásico, huwa inakuwa na faida kwa Madrid kama inashinda kwenye uwanja huo unaomilikiwa na Barcelona.

Real Madrid imetwaa ubingwa katika misimu minne ya 2011-12, 2007-08, 2006-07 na 2002-03 ambayo haikufungwa uwanjani hapo.

Lionel Messi

Wakati takwimu zikieleza hivyo kikosi cha Madrid kinachoongozwa na Kocha Carlo Ancelotti kinaonekana kutotulia huku vita ya wachezaji mastaa ikidaiwa kuigawa timu hiyo, wakati wenzao, Barcelona wanaonekana kutulia huku makali ya Lionel Messi yakiongezeka.

Christiano Ronaldo

Madrid imekuwa na mwendo wa kusuasua tangu kuanza kwa mwaka huu na inadaiwa kuwa mastaa wake, Cristiano Ronaldo na Gareth Bale hawana uhusiano mzuri.

Upande wa Messi ameongeza kasi ya kufunga mabao ambapo miezi miwili iliyopita alikuwa amezidiwa mabao 12 ya kufunga na Ronaldo, lakini mpaka sasa Messi anaongoza katika ufungaji akiwa na mabao 32 huku Ronaldo akiwa na 30.

Akizungumzia mechi hiyo, Luis Suárez wa Barcelona anasema yupo tayari kwa ajili ya mchezo huo kwa kuwa anajua historia na umuhimu wake ni mkubwa.

“Nakumbuka ule ushindi wa mabao 5-0 (wa Barcelona), nilikuwepo uwanjani siku hiyo, niliona mambo mengi jinsi watu walivyoshangilia lilikuwa jambo zuri na la kipekee,” alisema Suarez.

Aidha, kurejea uwanjani kwa kiungo, Luka Modric kunadaiwa kuamsha morali ya Bale ambaye hakuwa kwenye kiwango kizuri kwa muda. Modric alikuwa nje kwa muda mrefu, katika mechi iliyopita alicheza na Bale akafunga mabao mawili, wawili hao walicheza pamoja Spurs kabla ya kutua Madrid.

Jonas Mkude akinukisha, Mzungu hamtaki tena kikosini



SIRI imefichuka na sasa kila kitu hadharani juu ya kiungo wa Simba, Jonas Mkude kutojumuishwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.

Kuna mambo mawili makubwa yaliyotajwa juu ya Mkude kuwekwa pembeni, moja kubwa ni kuwa utovu wa nidhamu ndiyo kikwazo na Kocha wa Stars, Martin Nooij hana mpango wa kumuita tena labda abadilike baadaye.

Kiungo wa timu ya Simba ya Dar, Jonas Mkude.

Licha ya kuwa kwenye kiwango kizuri ikiwemo kuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha Simba, Mkude hajaitwa katika kikosi cha Stars ambacho kitaingia kambini keshokutwa Jumapili kujiandaa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi, Machi 29, 2015.

Mtu wa karibu na Mkude ameliambia Championi Ijumaa kuwa kuna vitu vingi ambavyo Mkude amekuwa akifanya vinamkera kocha huyo na alichoamua sasa ni kutomjumuisha kikosini kwake na kama akiendelea hivyo, basi ndiyo inawezekana asirejee tena kikosini hapo mpaka atakapoondoka.

“Mkude ni mchezaji mzuri lakini kuna vitu anatakiwa kubadilika, hasa kuzingatia muda. Mara nyingi anachelewa mazoezi akiwa Stars, kitu ambacho Nooij anakitafsri kama utovu wa nidhamu na kuna vitu vingi vya chinichini ambavyo amekuwa akifanya havimfurahishi kocha,” alisema mtoa taarifa huyo.

Sababu ya pili ambayo imetajwa pia kuwa inaweza kuwa imechangia kutoitwa kikosini hapo ni katika masuala ya posho.

“Siyo kwamba kiwango chake kimeshuka ila kuna fitina imefanyika kwa kuwa zile posho za siku wanazopewa wachezaji wakiwa Stars kuna watu wanataka ‘pasu’. Sasa Mkude huwa anagoma kutoa, ndiyo maana imekuwa nongwa, wakaamua wamuundie zengwe,” kilisema chanzo kingine cha uhakika.

Gazeti hili lilipozungumza na Mkude juu ya madai hayo, alisema: “Mwanangu mimi sitaki kuzungumza chochote kuhusiana na Taifa Stars, mwalimu ameshachagua kikosi chake ambacho ni sahihi, acha waendelee.”

Baada ya kusema hivyo, Mkude hakutaka tena kuulizwa swali linalohusu Stars.

Championi Ijumaa likamtafuta Meneja wa Taifa Stars, Clemence Boniface ambaye naye alifunguka: “Ninashukuru kunitafuta kuliongelea hilo lakini hayo mambo hayapo, ni uzushi tu wa kutaka kutuchafua.

“Wachezaji wakiwa kambini kwa siku wanapewa shilingi 50,000 timu ikiwa Tanzania, ikiwa nje ya nchi posho ni dola 50 na hakuna mchezaji anayekatwa.”

Alipotafutwa Nooij na kuulizwa juu ya madai hayo, alisema: “Siwezi nikalizungumzia suala hilo kwa sasa, nitatoa ufafanuzi siku chache kabla ya kucheza na Malawi.” Viungo walioitwa Stars ni; Amri Kiemba, Haruna Chanongo, Frank Domayo, Mcha Khamisi, Salum Abubakari ‘Sure Boy’, Hassani Dilunga na Said Ndemla.

Wakati huohuo, Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, juzi aligeuka mbogo mara baada ya timu yake kupokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Mgambo, ambapo kwanza aligoma kuzungumza na waandishi kisha kupiga teke chupa za maji.

Tukio hilo lilitokea baada ya mechi hiyo kwenye Uwanja wa Mkwakwani, ambapo baada ya hapo alienda kwenye basi la timu yake na kuanza kupiga tairi na mlango kwa hasira kisha kuingia ndani huku wachezaji wake wakiwa kimya.

2015-03-19

Yanga mia mia, Simba ni sheeeeeeeeeeeeda!!!!!!!!!!!!!!!!!

 
Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 34, moja zaidi kwa Azam (33) inayoshika nafasi ya pili, Simba imebaki nafasi ya tatu na pointi zake 29, huku Mbeya City ikijikwamua kutoka nafasi 13, hadi nafasi ya nane baada ya kuichapa Stand United kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Dar/mikoani. Yanga imerejea kileleni mwa Ligi Kuu baada ya kuichapa Kagera Sugar kwa mabao 2-1, huku Mgambo JKT ikiendeleza ubabe wake kwa Simba kwa kuichapa 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Ushindi huo umeifanya Yanga kufikisha pointi 34, moja zaidi kwa Azam (33) inayoshika nafasi ya pili, Simba imebaki nafasi ya tatu na pointi zake 29, huku Mbeya City ikijikwamua kutoka nafasi 13, hadi nafasi ya nane baada ya kuichapa Stand United kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya.

Jijini Dar es Salaam, Safu ya ushambuliaji wa Yanga, ‘MTN’ Msuva, Tambwe na Ngassa imeendelea kuwa moto wa kuotea mbali katika Ligi Kuu Bara.

Yanga ilipata mabao yake kupitia Simon Msuva na Amissi Tambwe wakati Salum Kanoni akifunga bao la kufutia machozi kwa Kagera Sugar.

Mshambuliaji Msuva alifungia Yanga bao la kwanza dakika tisa kwa mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa na beki wa Kagera Sugar Ibrahim Job kwenye eneo la hatari na mwamuzi Andrew Shamba kutoa adhabu hiyo.

Yanga iliendelea kulisakama lango la Kagera katika dakika ya 15, Tambwe alifunga bao akimalizia krosi ya Ngassa, lakini mwamuzi Shamba alikataa kwa madai mfungaji alikuwa ameotea. 

Tambwe alijirekebisha na kuifungia Yanga bao la pili dakika ya 16, akimaliza kazi nzuri iliyofanywa na Ngassa ambaye aliwatoka mabeki wa Kagera kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji.

Yanga ilipata pigo dakika ya 36, baada ya mshambuliaji wake Tambwe kuumia na kulazimika kutolewa nje na nafasi yake kuchuliwana Hussein Javu.

Kagera walimtoa Daud Jumanne na nafasi yake kuchuliwa na Juma Mpola, mabadiliko hayo yalikuwa na faida kwa vijana hao wa Mayanja kwani dakika ya 39, walipata bao la penalti lililofungwa na Salum Kanoni baada ya beki wa Yanga, Rajabu Zahiri kumchezea vibaya Atupele Green kwenye eneo la hatari.
 Mshambuliaji Jerryson Tegete aliyeingia kuchukua nafasi ya Sherman alipoteza nafasi kadhaa za kuifungia Yanga katika dakika za mwisho wa mchezo kutoka na kukosa umakini akiwa yeye kipa. 

Tanga:Mgambo JKT haijawahi kufungwa na Simba wala Yanga kwenye Uwanja wa Mkwakwani tangu ipande Ligi Kuu msimu miwili iliyopita.

Mgambo JKT imeendeleza rekodi yake kwa kuwafunga wachezaji 10 wa Simba kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na Ally Nassoro na Balime Busungu.

Simba ilianza mchezo kwa kasi na kulisakama lango la Mgambo JKT, lakini mashuti ya washambuliaji wake Emmanuel Okwi, Ibrahimu Ajibu yalishindwa kulenga goli. 
GPL

SIMBA SC YAANGUKIA PUA KWA MGAMBO SHOOTING

Kikosi cha timu ya Mgambo Shooting ya Tanga wakionekana katika picha ya pamoja wakati wa mechi yao dhidi ya Simba Sc ya Dar es Salaam. 


Kikosi cha timu ya Simba Sc. 

Mashabiki wa timu ya Simba Sc wakiduwaa baada ya timu yao kupokea kichapo cha bao 2-0 kutoka kwa Mgambo Shooting. 




Kaba nikukabe Emmanuel Okwi wa Simba na walinzi wa Mgambo Shooting.

Simba Sc imekubali kukalishwa na wagambo kwa kukubali kichapo cha bao 2-0 kutoka kwa Mgambo Shooting ya Tanga jioni hii ya leo kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Mabao ya Mgambo Shooting yaliingizwa wavuni na Ally Nassor ''Ufundi' dakika ya 21 aliyemalizia Krosi ya Fully Maganga na baadaye dakika ya 66 Malimi Busungu aliiongezea timu yake ya Mgambo bao la pili kupitia mkwavu wa penati baada ya kipa wa Simba Sc Ivo Mapunda kumchezea 'rafu' Fully Mganga akienda kufunga, Ivo alipewa kadi nyekundu na kutolewa nje ya mchezo huo.

Mpaka mwisho wa mpambano Simba Sc 0-2 Mgambo Shooting. Kwa matokeo hayo Simba inaendelea kuwa nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) ikiwa nyuma ya Azam yenye pointi 33 ikishikika nafasi ya pili nyuma ya Yanga yenye pointi 34 nafasi ya kwanza, wakati huo Mgambo Shooting ikishika nafasi ya 5 ikiwa na pointi 24. 
GPL

Twiga Stars kuelekea Zambia kesho


Twiga Stars wakiwa mazoezi

Timu ya Taifa ya Tanzania ya Wanawake (Twiga Stars), inatarajiwa kuondoka nchini siku ya ijumaa kuelekea nchini Zambia kwa ajili ya mchezo wake wa kwanza dhidi ya timu ya Taifa ya Wanawake ya Zambia siku ya jumapili.

Twiga Stars inaanzia hatua ya pili katika kuwania kufuzu kwa Fainali za Afrika kwa Wanawake baada ya kuwa katika nafasi za juu kwa viwango barani Afrika, na endapo itafanikiwa kuwaondoa Wazambia itafuzu moja kwa moja kwa fainali hizo.

Msafara utaongozwa na Blassy Kiondo (Mjumbe wa Kamati ya Utendaji), Beatrice Mgaya (kiongozi msaidizi), Rogasin Kaijage (kocha mkuu), Nasra Juma (kocha msaidizi), Furaha Francis (Meneja), Christine Luambano (Daktari) na Mwanahamis Abdallah (Mtunza vifaa).

MAN CITY YATUPWA NJE UEFA


Barcelona wakishangilia bao lao lililofungwa na Ivan Rakitic dakika ya 31.

Barcelona imefanikiwa kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Mabingwa Ulaya kwa kuifunga Manchester City bao 1-0 lililofungwa na Ivan Rakitic dakika ya 31 ya mchezo uliopigwa Nou Camp, Barcelona usiku huu na kuitupa nje City kwa jumla ya mabao 3-1.

Manchester City vichwa chini baada ya kuondolewa kwenye michuano hiyo.

Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Etihad nchini England, Manchester City walilala kwa mabao 2-1.

Patashika wakati wa mtanange huo uliopigwa Nou Camp, Barcelona.

Katika mchezo mwingine wa michuano hiyo, straika wa Juventus, Carlos Tevez aliifungia timu yake mabao 2 dakika ya 3 na 79 wakati ikiichapa Borussia Dortmund kwa mabao 3-0 huku bao lingine likiwekwa kimiani na Alvaro Morata dakika ya 70. Kwa matokeo hayo, Juventus nao wamefuzu hatua ya robo fainali huku Dortmund wakifunga virago.

2015-03-18

Ngasa aaga Yanga.


Winga hatari wa Yanga na Taifa Stars, Mrisho Ngasa, amewaaga na kuwashukuru mashabiki wake kwa kumpa sapoti katika kipindi chote alichokaa kwenye klabu hiyo ya Jangwani. 

Ngasa, mfungaji bora wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika mwaka jana na mfungaji bora wa Yanga msimu uliopita, mwishoni mwa wiki alikisaidia kikosi cha wanajangwani kupata ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Platinum FC ya Zimbabwe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo ya hatua ya kwanza ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Ngasa alifunga mabao mawili na kupika mengine mawili, lakini muda mfupi baada ya mechi hiyo aliandika maneno kwenye ukurasa wake wa Instagram yanayoashiria kuondoka Yanga.

“Kwa heri Yanga. Nakupenda, nashukuru kwa kila kitu,” ulisomeka ukurasa wa Ngasa wa Instagram juzi jioni.

NIPASHE ilimpiga simu Ngasa jana mchana, lakini hakupokea huku uongozi wa Yanga ukiweka wazi kwamba atakuwa huru kuondoka Jangwani baada ya msimu huu.

"Kwenye ukurasa ule yale si maneno ya Ngasa, ninadhani kuna mtu ameamua kufanya hivyo. Hata hivyo, Ngasa hajasaini mkataba mpya na Yanga, hivyo yuko huru kujiunga na timu nyingine baada ya kumalizika kwa msimu huu," alisema Jerry Muro, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano na Yanga baada ya kutafutwa na NIPASHE kwa simu jana alasiri.

Katika mechi dhidi ya Platinum FC, Ngasa ambaye miezi miwili iliyopita aliweka wazi kutokuwa na furaha Yanga kutokana na deni la zaidi ya Sh. milioni 40 alizowalipa Simba kufanikisha kuwatumikia mabingwa hao mara 24 wa Tanzania Bara, hakushangilia mabao yote waliyofunga Jumapili dhidi ya Platinum FC.


Nyota huyo alionekana akikutanisha viganja vyake ikiwa ni ishara ya shukrani huku pia akionyesha ishara ya kulia, kilio ambacho hata hivyo, kilihusishwa na kifo cha kocha Sylivester Marsh aliyemuibua.

Katika ukurasa wake huo, Ngasa aliposti picha yake ya mechi ya juzi akilia na aliambatanisha na maneno hayo.

Mbali na Yanga, mkali huyo wa kufumania nyavu, amewahi kuzichezea timu za Kagera Sugar, Azam FC na Simba.
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...