2015-01-23

Amefunguka;Waziri Nkamia Magazeti ya Mwananchi yanaaminiwa


Naibu Waziri Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia akizungumza na waandishi wa habari wa magazeti ya Mwananchi Communications Limited alipotembelea makao makuu ya kampuni hiyo, Dar es Salaam jana.


Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia amesema magazeti ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), yanasomwa na kuaminiwa na wananchi, hivyo yaendelee kufanya kazi kwa weledi.


MCL inachapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti, ambalo ni gazeti la michezo na burudani.


Waziri Nkamia, ambaye katika hali isiyo ya kawaida alihudhuria kikao cha kutathmini gazeti kinachofanyika kila siku asubuhi kwenye ofisi za makao makuu ya MCL, Tabata Relini, aliwataka aliwataka waandishi kufanya kazi kwa weledi ili kudumisha imani ya wananchi kwa gazeti hilo sambamba na amani ya nchi kwa kuwa ndiyo gazeti linalosambaa kwa haraka na kwa wingi katika maeneo mengi nchini.


“Gazeti lenu linafika sehemu kubwa ya nchi hii, ukienda Mwanza saa hizi (saa 2:00 asubuhi) utalikuta. Mkiamua kupotosha mtaivuruga nchi hii. Sitarajii kama mtafanya hivyo. Endeleeni kuwa makini katika kazi yenu,” alisema Nkamia ambaye kitaaluma ni mwandishi wa habari.


Mbunge huyo wa Kondoa Kusini alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, baadhi ya magazeti yameanza kuibuka huku mengine yakitumiwa na baadhi ya watu kuwachafua wengine kwa malengo yao ya kisiasa.


Aliongeza kuwa, siyo nia ya Serikali kukifungia chombo chochote cha habari, lakini kikikiuka utaratibu na sheria, Serikali haitasita kuchukua hatua kama inavyofanya.


Naibu waziri huyo alibainisha changamoto kubwa inayoikabili wizara hiyo kuwa ni kukosekana kwa sheria inayoweka uwiano sawa kati ya Serikali na vyombo vya habari.


“Uhusiano kati ya Serikali na vyombo vya habari siyo mzuri sana kwa muda mrefu. Sasa tumeandaa muswada ambao ukipitishwa utasaidia kuimarisha uhusiano kati ya pande mbili hizi,” alisema Nkamia na kuongeza kuwa katika muswada huo pia wanataka kuwe na bodi itakayokuwa ikisimamia vyombo vyote vya habari nchini.


Nkamia aliwataka waandishi kujiheshimu ili tasnia nzima ya habari nchini iheshimike tofauti na hali ilivyo sasa. Alisema kuna waandishi ‘makanjanja’ wanaotegemea kupewa fedha wakati wa kukusanya habari.


“Katika muswada huu tunalenga kila mwandishi wa habari awe na ajira. Kwa hiyo waandishi wa habari ni wadau wakubwa wa sheria hii tunayotaka kuianzisha, hamna budi kutuunga mkono ili tufanikishe,” alisisitiza.


Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene ambaye aliongozana na Naibu Waziri Nkamia, alisema uendeshaji wa magazeti unahitaji umakini mkubwa katika kuripoti.


Alisema gazeti la Mwananchi limekuwa likizingatia hilo kwa kiasi kikubwa hali inayofanya lijijengee imani kubwa kwa wananchi.
Mwananchi

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...