2015-01-23

MAMA GRACIA MACHEL AKUTANA NA WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO


Mke wa aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini Bi. Gracia Machel yuko nchini katika ziara fupi kusaidia kumaliza tatizo la Ndoa za utotoni kupitia programu na miradi mbalimbali atakayoifadhili ili kuwawezesha watoto wa kike kupata elimu hatimae kujikomboa na umaskini.

Katika ziara yake mama Machel, amekutana na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba ambapo, alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kwa jitihada kubwa inayofanya wizara hiyo kupambana na tatizo hilo la mimba za utotoni.

Vilevile, aliitaka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na wadau mbalimbali hususan viongozi wa mila/jadi na dini kushirikiana nae na kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko chanya kupitia program hizo anazotarajia kuzianzisha, na kuongeza kuwa, “Mkoa wa Mara ndio utakaokuwa wa kwanza kuanzishwa kwa program hiyo kwani bado mkoa huo una mila gandamizi. (mfumo dume)”,alisema Machel.

Naye Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba akiongea katika kikao hicho, alieleza kuwa, ni kweli tatizo hilo lipo nchini lakini Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali yakiwemo Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, Asasi za Kiraia na vyombo vya habari, wanapambana kikamilifu kumaliza tatizo hilo.

Aidha, Waziri Simba alitumia fursa hiyo kumshukuru Mama Machel kwa jitihada anazozifanya kuwawezesha watoto wa kike kuondokana na umaskini. Waziri wa maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba (katikati) akimsikiliza Mke wa aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini Bi.Gracia Machel (wa pili kushoto) aliyefika Wizarani hapo kujadili program maalum ya kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu. Waziri wa maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba (katikati) akisisitiza jambo wakati wa kikao chake na aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini Bi.Gracia Machel (wa pili kushoto) aliyefika Wizarani hapo kujadili program maalum ya kuwasaidia watoto wa kike kupata elimu. Wengine pichani toka kulia ni Naibu Katibu Mkuu , Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto , Nuru Millao na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto, Benedict Missani.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...