JESHI la Polisi nchini na uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), wametofautiana kauli kuhusu aliko Mwenyekiti wa vijana waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), George Mgoba (28), anayedaiwa kutoroshwa na polisi hospitalini hapo alikokuwa amelazwa.
Mgoba anadaiwa kutoroshwa na polisi baada ya Muhimbili kumruhusu ambapo hadi sasa hajulikani alipo.
Wakati Muhimbili wakisema mgonjwa huyo aliruhusiwa jana saa sita mchana, Jeshi la Polisi limedai yuko hospitalini hapo akiendelea kupatiwa matibabu, huku mke wake akidai hajafika nyumbani.
Msemaji wa vijana hao, Omary Bakari, aliliambia MTANZANIA kwamba mwenyekiti wao alionekana akipakiwa kutoka hospitalini hapo katika gari la polisi lenye namba za usajili PT 520 jana saa nne asubuhi.
Bakari alisema wanashindwa kuelewa wapi alikopelekwa kwa sababu ulinzi wa polisi hospitalini hapo ulikuwa mkali ambapo hata wao hawakuruhusiwa kufika wodini alikolazwa.
Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminieli Aligaesha, aliliambia MTANZANIA kuwa Mgoba aliruhusiwa jana saa sita mchana na anaendelea vizuri.
“Mgoba ameruhusiwa jana, kwa sasa anaendelea vizuri na hajakutwa na tatizo lolote. Kuhusu nani amemchukua na wapi ameenda, sisi kama hospitali hatujui,” alisema Aligaesha.
Kaimu Mwenyekiti wa vijana hao, Parali Kiwango, alisema aliwasiliana na mke wa Mgoba kumuuliza kama mumewe amerudi nyumbani na akamjibu hajafika.
“Baada ya kumkosa Mgoba wodini alikolazwa, nilizungumza na mke wake na kumuuliza kama mumewe ameruhusiwa, lakini alikataa na kusema kama ameruhusiwa bado hajafika nyumbani.
“Alisema anashindwa kusema lolote kwani ndugu, jamaa na marafiki walikatazwa kumwona hospitalini na pia hana taarifa yoyote juu ya mumewe ya kuruhusiwa,” alisema Kiwango.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema Mgoba ambaye pia anatuhumiwa kuchochea maandamano na kufanya mikusanyiko isivyo halali, yuko Muhimbili anaendelea na matibabu.
Alisema pamoja na kulazwa hospitalini hapo kwa matibabu, mwenyekiti huyo aligoma kutibiwa kwa siku tatu mfululizo licha ya kudai kuchomwa sindano ya sumu.
“Mgoba anadai amechomwa sindano ya sumu mwilini mwake, lakini cha kushangaza anakataa kutibiwa, hadi sasa ana siku tatu hajapata matibabu na akimwona daktari anapiga kelele, kwa kweli kesi hii ina shaka,” alisema Kamanda Kova.
Katika hatua nyingine, Kamanda Kova alisema Jeshi la Polisi linawashikilia vijana wengine wanne kwa kosa la kuchochea maandamano na kufanya mikutano bila kibali.
Jeshi hilo pia limemtaka Kaimu Mwenyekiti wa vijana hao, Kiwango aliyekimbia wakati wenzake wakikamatwa kujisalimisha haraka katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam au katika kituo chochote cha polisi kilicho karibu naye.
Kamanda Kova, alisema vijana hao walikamatwa juzi katika eneo la Muhimbili walikokuwa wamekwenda kumjulia hali Mgoba.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Linus Emmanuel (28) mkazi wa Tabata, Jacob Joseph (36) mkazi wa Mabibo, Rizione Ngowi (27) mkazi wa Mtoni Mtongani na Emmanuel Richard (28) mkazi wa Kawe.
Kamanda Kova alisema lengo la mkusanyiko wa vijana hao ni kutaka kuandamana kwenda Ikulu kuonana na Rais Jakaya Kikwete ili awapatie majibu ya tatizo la ajira ya kudumu.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa umoja huo wa vijana hauna usajili kisheria, na hakuna ahadi yoyote ambayo kikundi hicho walipewa.
“Watuhumiwa ambao tunaendelea kuwahoji ni Mgoba ambaye ni mwenyekiti pamoja na Emmanuel… Mgoba hivi sasa amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili baada ya kudaiwa kutekwa nyara huko Mabibo mwisho Februari 16, mwaka huu hadi alipopatikana Februari 19 saa nane usiku maeneo ya Tumbi, Kibaha mkoani Pwani kando ya barabara na mtekwaji yupo chini ya ulinzi,” alisema Kamanda Kova.
Kamanda Kova alisema Februari 20 mtekwaji Mgoba akiwa chini ya ulinzi, alijaribu kutoroka kutoka wodini alikolazwa, lakini polisi walibaini na kumkamata kabla hajatokomea na jalada la utoro chini ya ulinzi limefunguliwa na uchunguzi unaendelea.
Alisema tukio la Mgoba kudai kutekwa linaendelea kuchunguzwa kwa ushirikiano kati ya Polisi Mkoa wa Pwani na Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ili kubaini ukweli wa taarifa hiyo na wanaodaiwa kumteka.
0 comments:
Post a Comment