2015-02-04

MADAM MWAKA HUU BSS ISIWE NA LONGOLONGO KUNA BONGE LA ----- KAENE TAYARI


KWAKO Mkurugenzi wa Benchmark Production, Rita Paulsen. Bila shaka u-mzima wa afya na unaendelea na shughuli zako za kila siku za kulijenga taifa.

kitaka kujua hali yangu, mimi sijambo. Mzima wa afya na ninaendelea na majukumu yangu ya kila siku. Nimekukumbuka leo kupitia barua, maana kitambo kidogo hatujakutana ana kwa ana kikazi.

Nimekukumbuka Madam sababu natambua uwepo wa shindano lako kubwa la Bongo Star Search. Msisimko wake ni mkubwa na ndiyo maana Watanzania huwa wanalifuatilia kwa ukaribu pale linaporindima nchi nzima.

Big up kwa mchango wako maana mbali ya mshindi kupatikana na kupata chapaa, huwa kunakuwa na burudani nzuri hususan kutoka kwa washiriki ambao hugeuka kuwa ‘komedi’ kutokana na vituko vyao.

Pamoja na kukupa pongezi hizo lakini pia nina jambo nataka kukukumbusha. Kwa kuwa mwaka jana shindano hilo halikufanyika kwa kile ulichokiita kuwa ni ucheleweshwaji wa taarifa za wadhamini kutoshiriki, umeeleweka lakini swali ni kwamba., mwaka huu je umejipangaje? Jibu najua unalo.

Wakati ukitafakari juu ya ujio wako mpya, ni vyema pia ukatafakari pia juu ya ufanisi kwa kujifunza kupitia mashindano ya miaka iliyopita. Changamoto zote, malalamiko yote uyafanyie kazi. Watu wanataka kuona burudani na mshindi anapatikana kihalali.

Wanataka kuona kweli yule mshindi ambaye ana sifa za kuwa mshindi ndiye anayevishwa taji. Najua pengine kutokana na majukumu yako, yawezekana usiwe unayasikia malalamiko yote yanayoibuliwa na wananchi huku mitaani ila usijali nitakufikishia maana mimi ni balozi wao.

Kelele za watu wengi huwa ni mshindi kuwa tofauti na yule ambaye wengi wanaamini ana uwezo. Jitahidi sana hilo lisitokee mwaka huu. Jitahidi kusimamia majaji wasipendelee. Wampate mshindi ambaye kweli ana vigezo vya kuimba na asije hata kukuangusha, awike kimuziki na si kupotea mara tu shindano linapomalizika.

Kama unaona kuna udhaifu katika majaji ni vyema ukawashirikisha wataalam kutoka Balaza la Sanaa Nchini (Basata) ili waweze kutoa mawazo yao kitaalam.

Kiwango cha zawadi pia huwa ni tatizo. Kumekuwa na uvumi wa muda mrefu kwamba zawadi inayotangazwa si ile anayokabidhiwa mshindi, hivyo ni vyema basi mwaka huu uzushi huo ukatafuta namna ya kuufanya ufikie mwisho.

Ni bora kutangaza zawadi ndogo lakini ikamfikia yote mshindi kuliko kutangaza kubwa halafu kiuhalisia anapewa ndogo. Mfumo wa kupiga kura uwe wazi na kila mtu aamini kabisa kwamba ushiriki wake katika kupiga kura una maana. Kusiwe na chembe ya ujanjaujanja.
Kwa leo naishia hapa.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...