WASIFU Jina: Deogratias Aloyce Ntukamazina Chama: CCM Jimbo: Ngara
Nimefanya juhudi kubwa kama mwenyekiti wa Mfuko wa Bima ya Afya kuhamasisha kaya mbalimbali kujiunga na mfuko huo ambao kaya moja inalipa Sh10,000 kwa matibabu ya kaya nzima kwa mwaka mmoja. Kuna wazee wanaweza kumudu Sh10,000 kwa mwaka.
1.Mwalimu Superi Jeremiah wa Shule ya Msingi Bihororo Ngara.
Uliahidi kuondoa kero ya wazee kulipia gharama za matibabu katika vituo vya kutolea huduma, hadi sasa wananchi bado wanataabika. Je, umefanya jitihada gani kuhakikisha wazee hao wanatibiwa bure katika hospitali ndani ya meneo yao?
Jibu: Naomba wananchi wa Ngara wakumbuke vizuri, mimi nilitoa ahadi moja tu kwamba nitashirikiana na Serikali na halmashauri ya wilaya ya Ngara pamoja na wananchi kupambana na maadui watatu yaani umaskini, ujinga na maradhi. Chini ya adui maradhi nimeshirikiana na wabunge wenzangu kuhimiza Serikali ihakikishe sera yake ya matibabu bure kwa wazee wa miaka 60 akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano inatekelezwa. Nakiri kwamba watoa huduma ni wakaidi lakini Serikali imeahidi kuendelea kuwabana. Nimefanya juhudi kubwa kama mwenyekiti wa Mfuko wa Bima ya Afya kuhamasisha kaya mbalimbali kujiunga na mfuko huo ambao kaya moja inalipa Sh10,000 kwa matibabu ya kaya nzima kwa mwaka mmoja. Kuna wazee wanaweza kumudu Sh10,000 kwa mwaka.
2.Mohamed Namtimba Kata ya Kabanga- Ngara.
Uliahidi kuishauri Serikali kutenga fedha za uhamisho wa watumishi waliokaa kituo cha kazi muda mrefu, lakini ahadi yako haijatekelezeka hadi sasa?
Jibu: Nimeshauri mara nyingi Tamisemi kuhakikisha inakuwa na utaratibu wa kuwahamisha hamisha watumishi wake ili wasikae kwenye kituo kimoja cha kazi kwa zaidi ya miaka 10, tatizo ni fedha. Muuliza swali utakumbuka Rais (Jakaya Kikwete) alipofika Ngara mwaka juzi akiongozana na Waziri wa Tamisemi nilimwomba awahamishe watendaji wa halmashauri ya Ngara ambao walikuwa wamekaa kwenye halmashauri kwa zaidi ya miaka 10. Waziri ameshawahamisha watendaji saba katika kutekeleza ombi langu.
3. Kenedy Staford, Mwenyekiti wa Chadema wilayani Ngara.
Uliahidi kuondoa kero ya maji mbele ya Rais Kikwete hapa mjini Ngara. Je? Baada ya kusikia Meneja wa maji amepora zaidi ya Sh32 milioni, ulichukua hatua gani? Na miradi ya maji ya Benki ya Dunia mboa haijakamilika kikwazo ni nini?
Jibu: Rais alipofika Ngara mwaka 2013 ni mimi kama mbunge nilimuomba mbele ya wananchi atusaidie kutatua tatizo la maji katika mji mdogo wa Ngara. Rais bila kuchelewa alimuagiza Waziri wa Maji kutembelea mitambo ya maji ili kubaini tatizo. Mara tuliporudi bungeni waziri aliniahidi angetoa fedha Sh200 milioni. Wizara ilitoa Sh150 milioni na meneja wa maji akatuibia Sh 32 milioni bahati nzuri nilipohudhuria kikao cha halmashauri nilishiriki katika kuhakikisha meneja huyo anapelekwa mahakamani na sasa kesi inaendelea. Kuhusu kukwama kwa maji chini ya mradi wa Benki ya Dunia tatizo ni Serikali kutokuwa na fedha. Naendelea kufuatilia jambo hilo.
4.David Mapunda wa Idara ya Afya Ngara.
Tangu ahadi za kujenga na kusambaza umeme vijijini kufika kituo cha Forodha Rusumo mpakani mwa nchi ya Rwanda, ujenzi wake unasua sua umefuatilia kwa kiasi gani ili umeme upatikane kabla ya kuondoka kwako madarakani?
Jibu: Namshukuru Mungu kwa ufuatiliaji wangu na kupata ushirikiano wa REA na hivi sasa umeme umeshawaka katika kituo cha Forodha Rusumo na mchakato unaendelea wa kusambaza umeme kwenye vijiji vya jirani na Forodha ya Rusumo. REA imepeleka umeme Mgoma na Mamlaka ya Mji mdogo Rulenge. Nafuatilia mradi wa ORIO-Holland wa kuweka jenereta mbili kubwa kwenye Tanesco ya Ngara ili kusambaza umeme Benaco, Kabaheshi, Nyamahwa hadi kijiji cha Kashinga.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment