2015-02-05

Ni bonge la shangwe:Pinda Wanafunzi wa sherehe za CCM ni wanachama cheki walivyo sheherekea hapa.............................




                          Waziri Mkuu Mizengo Pinda

 
waziri mkuu alisema chama hicho tawala kina mfumo ambao unaazia ngazi ya chipukizi na kwamba wazazi wa watoto hao ni wana-CCM

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mizengo Pinda amedai kuwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari walioshiriki sherehe za miaka 38 ya CCM mjini Songea, wakiwa wamevalia sare, ni watoto wa wanachama wa chama hicho tawala, kauli ambayo imekosolewa na watu wa kada mbalimbali.

Sherehe hizo zilifanyika Jumapili ya Februari 1 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, zikishirikisha makundi mbalimbali, wakiwamo wanafunzi hao wa shule za msingi na sekondari ambao walivalia sare za CCM na kucheza gwaride na halaiki, ambayo kwa kawaida huchukua muda mrefu kujifunza na kuielewa. 


Lakini akijibu swali la mbunge wa viti maalum (Chadema, Susan Lyimo, mtendaji huyo mkuu wa Serikali alitetea ushiriki wa watoto hao wapatao 500 kwenye sherehe hizo akisema kuwa ni sehemu ya mfumo wa wanachama wa CCM.

“Susan, utafikiri tulikuwa pamoja. Nilijua tu swali hili lazima litaulizwa. Ila mtoto wa nyoka ni nyoka. Chama hiki kina mfumo wake ambao umeshuka mpaka kwenye ngazi ya kitu kinaitwa chipukizi,” alisema akijibu swali la mbunge huyo aliyetaka kujua sababu za CCM kutumia watoto kwenye shughuli zake za siasa wakati ina wanachama wapatao milioni 10 kote nchini.

“Chipukizi hawa ni watoto ambao wamezaliwa kutokana na wazazi wana-CCM, ndiyo maana chama kiliwatumia. Sherehe ilikuwa nzuri na ilipendeza sana. Kwa kuwa hawajafikia umri wa kuingia katika masuala ya siasa, halina madhara lile rafiki yangu, pia bado ni wadogo mno na walikuwa wanafurahia gwaride na kuvaa sare tu.”

Lyimo hakuridhishwa na jibu hilo la Waziri Pinda, akisema hakutakiwa kutoa majibu ya aina hiyo na kwamba katika mkusanyiko huo, kulikuwa na watoto wazazi wao si wanachama wa CCM.

“Lengo la watoto hawa ni kusoma na si kufanya siasa. Iweje mfanye mambo kwa double standard (ndumilakuwili)?” alihoji na baadaye Pinda alitaka suala hilo lisiendelee kujadiliwa. 



“Naheshimu maelezo ya Susan, lakini kiacheni chama kiendelee na utaratibu wake. Mfumo wake ndiyo huo, ndiyo ulivyo na sidhani kama kuna haja ya kuendelea kubishana katika suala hili,” alisema Pinda ambaye ofisi yake inasimamia elimu ya msingi na sekondari.

Kitendo hicho cha zaidi ya wanafunzi 500 kushiriki sherehe hizo kwa kuimba nyimbo mbalimbali za CCM, kucheza halaiki na gwaride kimekosolewa na wasomi na wanasiasa nchini, wakisema wanafunzi wanaweza kushirikishwa kwenye shughuli za kitaifa tu, si za vyama vya siasa.

Kabla ya nchi kuruhusu tena siasa za vyama vingi mwanzoni mwa miaka ya tisini, wanafunzi wa shule za msingi na sekondari walikuwa wakitumiwa kwenye shughuli za chama tawala na za Serikali, lakini imekuwa ni nadra sana kuonekana kwenye mikutano ya kisiasa tangu uhuru wa kidemokrasia ulipoanza.

Lakini ili kufanikisha sherehe hizo za CCM ambazo zilifanyika Jumapili kutokana na siku ya kuzaliwa chama hicho (Februari 5) kuwa katikati ya wiki, maofisa wa elimu ya sekondari wa Manispaa ya Songea waliwaandikia barua wakuu wa shule zilizopo karibu na Uwanja wa Majimaji, wakiwataka kuhudhuria pamoja na walimu na wanafunzi ambao waliagizwa kuvaa sare.

Majibu hayo hayakuridhisha wabunge wengine na baada ya kipindi cha maswali ya papo kwa papo ambacho Waziri Pinda alikianzisha ili kujibu hoja mbalimbali za utendaji wa Serikali, mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi), Felix Mkosamali aliomba mwongozo wa Spika juu ya suala hilo. 
Mwananchi.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...