Polisi wakiwa wamewaweka chini ya ulinzi baadhi ya wananchi walioandamana na kufunga Barabara ya Geita kwenda Bukoba jana. Picha na Jackline Masinde
Tafrani hiyo ilikuja baada ya mwanafunzi Mussa Joseph (9), wa darasa la nne, Shule ya Msingi Ludete, kugongwa na kufa wakati akivuka barabara katika eneo la stendi mpya Katoro.
Geita. Mji wa Katoro jana ulizizima kwa mabomu ya machozi wakati polisi walipokuwa wakiwatawanya wanafunzi na wananchi waliofunga barabara kuu ya Geita Bukoba waliokuwa wakiishinikiza Serikali kuwawekea matuta ili kuepukana na ajali.
Tafrani hiyo ilikuja baada ya mwanafunzi Mussa Joseph (9), wa darasa la nne, Shule ya Msingi Ludete, kugongwa na kufa wakati akivuka barabara katika eneo la stendi mpya Katoro.
Sinema nzima ilianza jana saa mbili asubuhi baada ya ajali hiyo ambapo wakazi wa eneo hilo wakishirikiana na wanafunzi wa Shule za Msingi Ludete na Mkapa kufunga barabara kwa mawe huku wakiwa wameshika silaha mbalimbali.
Kwa mujibu wa Diwani wa Kata ya Katoro, Gervas Daudi, akizungumza eneo la tukio alidai kuwa mwanafunzi huyo aligongwa na pikipiki hiyo majira ya saa tano asubuhi wakati akivuka barabara akitoka shuleni hapo.
Alisema mwanafunzi huyo ambaye amezikwa jana nyumbani kwao Katoro alifariki dunia papohapo kutokana na pikipiki hiyo kuwa kwenye mwendo kasi na dereva wake hakuweza kusimama kuhofia kupigwa na wananchi.
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, alifika eneo la tukio na kuamuru uongozi wa halmashauri ya wilaya, walimu waliohamasisha vurugu hizo wachukuliwe hatua za kinidhamu na kwamba walimu wakuu wa shule hizo washushwe vyeo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Joseph Konyo alithibitisha tukio hilo ingawa hakutaka kuzungumzia kwa undani kwa kuwa mkuu wa wilaya alikwishalizungumzia.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kalifonia, Elias Muembeni alisema wanafunzi hao wamechukua hatua ya kufunga barabara baada ya kuwapo kwa ajali za mara kwa mara katika eneo hilo.
“Hadi sasa zaidi ya watu watano wamekwishapoteza maisha kwa kugongwa na magari pamoja na pikipiki katika eneo hili,” alisema Muembeni.
Aliongeza: “Badala ya kutumia busara, waliamua kulala barabarani wakiwa tayari kwa lolote na kudai wasingetoka hadi matuta yawekwe ndiyo maana foleni ya magari imekuwa kubwa kama unavyoiona.’
Mwananchi



0 comments:
Post a Comment