Fally alikuwa bado bwana mdogo, kipindi hicho ndiyo kwanza ametoka katika kwapa za Koffi Olomide na kuamua kuwa mwimbaji wa kujitegemea. Tulipozungumza naye pale katika Ukumbi wa Kampuni ya Sigara, Barabara ya Nyerere, alikiri kwamba alilazimika kuchukua uamuzi mgumu wa kuondoka kwa Koffi, kwa sababu tu, aliamini katika kipaji chake.
Na kweli, katika ile shoo ya World Cinema, ambayo mamia ya mashabiki wa muziki wa Kongo DRC walifurika, Fally Ipupa alifanya kweli kuliko maelezo. Alipata mashabiki wengi, wengi kabisa, wengi wao wakiwa akina dada!
Lakini kama kuna kitu kilinishtua, basi ni pale nilipomuona dogo mmoja Mtanzania akipanda jukwaani na baadaye kupewa nafasi ya kuimba huku akipigiwa vyombo na wanamuziki wa Fally. Huyu dogo alikuwa Barnaba!
Wazungu wanasema ‘he steal the show’ yaani alifunika mbaya kiasi kwamba aliondoka kuelekea ‘home’ akiwa amenona, maana wekundu wekundu aliopewa pale walikuwa siyo haba, hasa kwa kiwango chake wakati ule.
Sina uhakika walionana wapi na Fally hadi akapewa nafasi ile, ingawa kuna uwezekano mkubwa kuwa ilikuwa ni kazi ya THT kwani kumbukumbu zinaonyesha kipindi hicho alikuwa pale. Mwisho wa mchezo, Ipupa alikiri kuvutiwa na kipaji cha Barnaba na kwamba angekuwa naye bega kwa bega.
Leo tunapozungumza ni karibu miaka saba sasa, Fally Ipupa amekuwa mwanamuziki wa kimataifa zaidi huku Barnaba bado akifukuzana na shoo za Kibongo. Kilichonishtua, ni hivi majuzi niliposoma katika mtandao mmoja akisema eti mwanamuziki huyo Mkongo, anakifurahia kipaji chake!
So what Barnaba? Anafurahia kipaji chako, halafu, what’s next? Huenda hajui, lakini uzoefu nilionao kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya, ambao yeye anaufanya, unamtenganisha kwa umbali kabisa kama utazungumza kuhusu uwezo wa kuimba na namna ya kucheza na sauti yake. Yupo juu!
Ninazifahamu na kuzifurahia kazi zake kadhaa, ikiwemo Njia Panda, aliyomshirikisha Pipi waliyekuwa wote THT. Kuna watu wachache wanaoimba ninaoweza kuwalinganisha naye kwa maana ya sauti, lakini inatia uchungu sana unapogundua kuwa hatumii vizuri uwezo wake katika kukwea ngazi moja juu.
Katika kazi hizi tunazotumia vipaji, mara nyingi mtu anasogea kulingana na jinsi anavyotumia fursa anazokutana nazo. Kwa msanii, ni sawa na kosa la jinai kukutana na mwanamuziki mkubwa kidunia, anayefurahia kazi yako, halafu ukamuacha aendelee na shughuli zake bila wewe kumsukuma akusaidie.
Kosa kama hilo liliwahi kufanywa na msanii mwingine ninayezimia uwezo wake, Ali Kiba, ambaye aliishia kuchezacheza kwenye makochi ya Studio za R Kelly kule Marekani wakati walipokutana kwenye project ya One 8, walipotengeneza kazi iliyoitwa Hands Across the World!
Na hii ndiyo siri kubwa ya mafanikio ya Diamond. Kila anapopiga hatua moja, anapenda kwenda mbele zaidi, ndiyo maana wakati wasanii wengi wa Bongo wanaishia kuwakubali tu wenzao wa Nigeria, hivi sasa kijana wa Tandale ni washkaji zake na sitashangaa, siku chache zijazo nikisikia Platinumz akifanya kolabo na Rick Ross!
Niwakumbushe wasanii, vipaji vyao vinawapa fursa ya kukutana, siyo tu na wasanii wakubwa wa nje, bali hata watu wenye ushawishi katika jamii yetu. Hiyo ndiyo fursa, itumie kuhakikisha inakusogeza mbele! JIUNGE NA GLOBAL BREA
0 comments:
Post a Comment