2015-03-13

WANANCHI WACHAMBUA UONGOZI WA JK



Rais Jakaya Mrisho Kikwete.
HAPPY SILVANUS, MUSOMA
Hongera sana mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, hakuna mtu anayeweza kukabidhiwa nchi kubwa kama hii na akatoka bila lawama, jipe moyo Mungu akutie nguvu. Kwangu mimi umefanya kazi nzuri japo si katika maeneo yote. Umejitahidi, nakutakia kustaafu kwema hakunaga kama Chama cha Mapinduzi ‘CCM’.

BORA KAMBI, IRINGA
Kweli Rais Jakaya Kikwete ulisema ukweli ulipokuwa China kwamba kazi ya urais ni ngumu, huna hata hamu ya kuendelea. Siri iliyopo ikulu unaijua, na kipindi chako chote kilitawaliwa na mikasa mingi ya kisiasa na kijamii. Umekuwa mtu wa huruma na fadhila, umekuwa mtu wa dhamira ya kusaidia watu, tutakumbuka upole wako JK.

ABDALLAH AYUBU, KIGOMA
Kiukweli mheshimiwa kwanza nakusifu kwa uimara wako, baadhi ya maendeleo nimeyaona sana tu ila ajira ni janga kwa vijana wa Tanzania hasa huku vijijini ila uongozi wako umekuwa mzuri. Tunaomba ajaye aje kumaliza palipobaki. Nakutakia majukumu mema ya kazi ya kutupa maisha mazuri, hongera sana kwa miaka yako 10.

BATUS DAVID, KIGOMA
Ingawa bado miezi michache uondoke kwenye nafasi yako, nakupongeza kwa kufanya vizuri kwenye sekta za afya, elimu, maji na barabara. Naomba kabla ya kung’atuka uhakikishe unaboresha mishahara ya watumishi wa umma hasa walimu kwani wao ndiyo chimbuko la taaluma zote na maendeleo ya taifa. Pia tukamilishie Barabara ya Kidawe- Nyamakazi kwa kiwango cha lami. Nakupongeza kwa uongozi wako bora ingawa wasaidizi wako uliowaamini walijaribu kutia doa serikali yako lakini ulisikia vilio vya Watanzania ukawaweka kando.

JACKSON VENANT, KAGERA
Katika uongozi wako uliahidi mengi JK ila nashindwa tambua kati ya uliyoahidi umetimiza lipi? Mfano sisi wananchi wa mkoa wa Kagera ulituahidi mengi ikiwemo meli mpya lakini umebakiwa na miezi michache hatujaona meli wala chochote, hata MV Victoria leo haifanyi kazi, madawa hakuna hospitalini, vijana hatuna kazi, leo unamaliza muda wako unasema elimu itakuwa bure, ulishindwa nini wakati wa utawala wako wa miaka 10 kutoa elimu bure? Hata hivyo, wewe ni rais wangu na una mazuri uliyotufanyia Watanzania.

GOODLUCK MADUKWA
Kwa upande wangu JK umefanya makubwa lakini katika suala la elimu tafakari tena maama ubora wake umepotea, lakini pia jitahidi sana katika kipindi hiki kilichobaki kutimiza baadhi ya mambo yanayowezekana ili hata serikali mpya inayokuja iweze kuendelea na yale ambayo utakuwa umebakiza katika kipindi chako, kazi njema mkuu wangu na kazi njema.

LUCANIMA, MWANZA
Pole sana rais wangu JK kwa jukumu ulilonalo kwa sasa kuelekea uchaguzi mkuu, muda ambao ulikuwa madarakani umefanya mambo mengi mazuri, ila katika ahadi zako kuhusu vijana haujafanya chochote kabisa, ulituahidi utatuwezesha vijana kupata ajira, kumbuka mheshimiwa JK chaguzi za mitaa zilivyokuwa, watu wamechoka.

GOODLUCK MWAKALOBE, MBEYA
JK tulikuchagua na tulikuamini lakini mazuri machache uliyoyafanya yamefanikiwa ila mabaya waliyoyafanya wasaidizi wako na watendaji wako yamekutia doa. Mungu atajulie tupate rais mwingine mwenye hekima kama wewe ili mambo mengine yaweze kwenda sawa. Kama kuna kipande hukumaliza kukifanya ajaye amalizie. Tunakupenda ila kuwa makini ili uweze kuacha nchi ikiwa salama.

JACOB MWELEZI, MBEYA
JK nakupenda sana kwa msimamo wako, kuna wakati Watanzania huwa tunapenda kuona ukifanya maamuzi magumu ambayo yataleta maendeleo kwetu sisi walala hoi, nina imani sana na wewe lakini muda uliobaki kumaliza kukalia kiti cha ikulu ni mfupi sana, sijui kama kuna vitu utakuwa umefanya kwa ajili ya kuiweka serikali katika hali nzuri, hasa madeni tunayodaiwa na nchi kubwa.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...