JESHI la Polisi mkoani Pwani linamshikilia raia wa nchi ya China We Sheng (39) mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kumteka nyara Mkurugenzi wa Kiwanda cha Kutengeneza Viatu vya Plastiki (Yeboyebo), Li Cheng Weng (54) baada ya kumtishia kwa silaha
Mtuhumiwa huyo alitoa sharti na kumtaka mlalamikaji atoe fedha kiasi cha dola za Kimarekani 350,000 (sawa na Sh milioni 584.5) ili amwachie huru.
Akizungumza ofisini kwake mjini Kibaha, Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani, Ulrich Matei alisema tukio hilo lilitokea Oktoba 19 mwaka huu majira ya saa 4.00 usiku wilayani Mkuranga
Kamanda Matei alisema kuwa baada ya kupekuliwa kwenye gari lake aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 554 BAJ alikutwa na bunduki aina ya Short gun namba 006085010, risasi 98 na visu viwili.
Kwa mujibu wa Kamanda Matei, Polisi walikwenda kupekua nyumbani kwa kijana huyo wakakuta nyaraka zinazoonesha kuwa, amewahi kumiliki risasi 300, hivyo haijafahamika risasi 202 amezitumia wapi.
Amesema, Ubalozi wa China umewafahamisha polisi kuwa, mtuhumiwa huyo alikuwa akishiriki kufanya uhalifu nchini humo.
Kamanda Matei alisema , polisi wanawasiliana na wenzao wa Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) ili kupata taarifa zaidi kuhusu kijana huyo.
Source: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment