2014-10-24

VIFO VYA WASANII; MSHITUKO

Marehemu Sherry Magali wa Bongo Movies enzi za uhai wake

Misiba kila kona! Achilia mbali watu wasiokuwa na majina hasa vijana wadogo, ndani ya saa 24 wamefariki dunia wasanii wanne wa kutoka kwenye tasnia za Bongo Movies na Bongo Fleva, Amani liliripoti habari yenye kuumiza moyo.  Kama ifuatavyo.

HAWA HAPA
Matukio hayo yalitokea kati ya Jumatatu jioni na Jumanne asubuhi ambapo kutoka kwenye tasnia ya filamu waliotangulia mbele ya haki ni pamoja na Sherry Salum ‘Sheri Magali’, Arafa na Benson Okumu Otieno.

Kwa upande wa Bongo Fleva, Yessaya Ambikile ‘YP’, naye alitangulia mbele ya haki ikiwa ni siku chache tu alionekana kwenye kumbi mbalimbali jijini Dar.

ALIANZA MDOGO TYSON
Jumanne jioni, gazeti hili lilipokea kwa masikitiko kifo cha mdogo wa marehemu George Okumu Otieno ‘Tyson’ aitwaye Benson Okumu Otieno ‘Benii’ ambaye alifariki dunia baada ya kupata homa kali na kuchanganyikiwa.
Marehemu YP kutoka Kundi la TMK Wanaume Family enzi za uhai wake.

Babari za ndani zilieleza kwamba Benii alianza kuumwa mkono kawaida ambapo alitumia dawa lakini baada ya siku chache mkono huo ulianza kuvimba na kupata homa kali iliyosababisha kwenda hospitali.

Ilielezwa kwamba Benii alikwenda Hospitali ya Lugalo, Dar ambapo homa ile ilipanda kichwani na kumfanya achanganyikiwe, mwisho akaaga dunia.  Baada ya msiba huo kutokea, taratibu za kuusafirisha mwili kwenda kijijini kwao Kisumu nchini Kenya zilifanywa nyumbani kwa mdogo wake wa kike maeneo ya Sinza-White Inn jijini Dar.

Habari zilieleza kwamba Benii alikuwa akifanya kazi za uongozaji wa filamu (director) ambapo alifanikiwa kufanya filamu na wasanii mbalimbali. Benii alianza kazi hiyo alipofika jijini Dar akiwa anaishi na kaka yake, George Tyson aliyefariki dunia Mei 30, mwaka huu kwa ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Gairo mkoani Morogoro.

Marehemu Arafa aliyekuwa msanii chipukizi ndani ya Bongo Movies enzi za uhai wake.

“Jamani tatizo ni nini? Hata maumivu ya kifo cha kaka yake hajaisha, jamani na Benii naye? Tumuombe sana Mungu atuepushe na balaa hili la vifo,” alisema mwigizaji mkubwa Bongo, William Mtitu.

ARAFA WA BONGO MUVI AFIA INDIA!
Huku na huku, wakati watu wakitafakari kifo cha Benii na taratibu za kuusafirisha mwili wake, ghafla ziliibuka habari nyingine mbaya kuwa chipukizi wa Bongo Movies aliyetajwa kwa jina moja la Arafa naye aliaga dunia jioni hiyo ya Jumatatu.

Habari zilieleza kwamba Arafa, mtoto mzuri mwenye mvuto huku akiwa na umri chini ya miaka 20, anadaiwa kupelekwa nchini India na mama mmoja kwa shughuli binafsi. Ilielezwa kwamba, akiwa nchini humo aliumwa ghafla (ugonjwa haukutajwa) ndipo akapoteza uhai hivyo taratibu za kuurejesha mwili wake Bongo zinaendelea.

Benson Okumu, enzi za uhai wake akiwa na mtoto wa marehemu George Okumu Otieno ‘Tyson’ , Sonia.

YP NAYE AAGA DUNIA
Msanii YP kutoka Kundi la TMK Wanaume Family, naye aliaga dunia usiku wa kuamkia Jumanne wiki hii. Habari kutoka kwa familia yake zilieleza kwamba YP alianza kusumbuliwa na kifua tangu mwezi Machi, mwaka huu ambapo alitibiwa na kuanza dozi.

Kwa mujibu wa mkewe, Sakina Robert na dada yake Hawa Ambikile, YP alimaliza dozi mwezi Septemba, mwaka huu ambapo hivi karibuni hali ilibadilika na kuwa mbaya zaidi.Mkewe alisema alikimbizwa katika Hospitali ya Temeke, Dar ambako alipatiwa matibabu hadi umauti.

Meneja wa TMK Wanaume Family, Said Fela alisema msiba wa msanii huyo uliwekwa Keko, Dar nyumbani kwa baba yake na alitarajiwa kuzikwa jana saa 10:00 jioni kwenye Makaburi ya Chang’ombe jijini Dar.

Fela alisema kuwa YP alifanya vizuri kimuziki wakati na msanii mwingine Y Dash ambapo alisikika kwenye ngoma kibao kama Ulipenda Pesa na Pumzika.

MASKINI! ALIPANGA KUACHIA NGOMA MPYA
Ngoma nyingine nyingi alifanya na TMK Wanaume Family kama Twende Zetu ya Chegge Chigunda, Dar Mpaka Moro, Kichwa Kinauma na Tufurahi na tayari alikuwa amerekodi wimbo wake mpya akiwashirikisha Tip Top Connection unaokwenda kwa jina la Wazee wa Jiji aliopanga kuuachia mwezi ujao.

YP ameacha mke na mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa miaka saba.

BURIANI SHERRY MAGALI!
Wakati pigo la TMK Wanaume Family likiumiza, majira ya saa 6:00 mchana, siku ya Jumanne iliyopita, ghafla kuliibuka habari nyingine mbaya kwenye Bongo Movies baada ya kuondokewa na mwigizaji ambaye ni mchekeshaji, Sherry Magali.
Sherry Magali aliaga dunia wakati akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kifua na moyo kwa muda mrefu.

Jumamosi iliyopita mwanahabari wetu alimtembelea wodi namba nane ambapo Sherry Magali alisimulia namna alivyokuwa akipata maumivi makali naya muda mrefu tangu mwaka jana huku akionekana kudhoofu mwili na kukosa nguvu.

Baada ya kukutwa na umauti, msiba uliwekwa nyumbani kwao maeneo ya Mji Mpya mjini hapa kwa mzee Msafiri Ngedele.

Mazishi ya Sherry yalitarajiwa kufanyika jana kwenye makaburi ya Kola mjini hapa.
Enzi za uzima wake, Sherry Magali alisifika kwa kuchekesha na lile umbo lake zuri lililokuwa likiwatoa midume udenda. Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi-Mhariri. 


Imeandaliwa na Hamida Hassan, Chande Abdallah, Deogratius Mongela, Shani Ramadhan, Gladness Mallya na Dustan Shekidele, Morogoro.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...