Katika Dodoma/Dar. Pamoja na maneno mengi yaliyosemwa, shutuma lukuki zilizotolewa na mbinu za kila aina kutaka kuzuia mjadala wa ripoti ya uchunguzi wa kashfa ya IPTL, leo ndiyo siku yake ya hukumu.
Hukumu hiyo, ukweli utadhihirika kuhusu nani mkweli na nani mwongo wakati Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), itakapowasilisha bungeni maoni yake kuhusu ripoti ya kuchotwa kwa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Uchunguzi huo ulifanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa maelekezo ya Serikali baada ya kuombwa na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila alipolalamikia ufisadi huo bungeni.
Pamoja na juhudi za kampuni ya IPTL na PAP kufungua kesi kuzua mjadala huo bungeni, hukumu iliyotolewa jana na majaji watatu ilisema kila kitu kiendelee kama kilivyo na kitakachoendelea kisiathiri kesi iliyopo mahakamani.
Uamuzi huo ulipokewa kwa hisia tofauti, upande wa IPTL ukishangilia kwa kupewa ulinzi, huku baadhi ya watu wakieleza kuwa Mahakama imezuia mjadala huo unaosubiriwa kwa hamu.
Muda mfupi baada ya hukumu hiyo kutolewa na kusambaa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe ambaye pia alikuwa mdaiwa, aliandika katika ukurasa wake wa Twitter, “Mahakama imetoa zuio la kujadili taarifa ya CAG kuhusu Escrow.
Hata hivyo, PAC itawasilisha taarifa yake kwa mujibu wa ratiba ya Bunge hapo kesho.”
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel alisema: “Sisi hatuna taarifa hizo kutoka mahakamani, ratiba ya Bunge inaendelea kama kawaida.”
0 comments:
Post a Comment