Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika (kulia) akizungumza kuhusu hali ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika nchi nzima juzi. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu. Picha na Venance Nestory
Hatua hiyo inatokana na malalamiko kutoka kwa wapigakura, wagombea na vyama mbalimbali vya siasa kuhusu kuvurugika na kutofanyika kwa uchaguzi katika baadhi ya maeneo kutokana na kasoro mbalimbali.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika alisema jana kuwa baada ya hujuma na ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi huo, kamati kuu itakuja na mapendekezo ya nini cha kufanya.
“Kikao hicho kitakuja na maazimio juu ya hatua za kuchukua dhidi ya Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) mwenye dhamana ya Tamisemi ambao wamevuruga uchaguzi huu. Hata katika maeneo ambayo uchaguzi umeahirishwa kama Ukawa tutashirikiana kuhakikisha tunaiondoa CCM licha ya vitendo vya kuhujumu uchaguzi unaofanywa na viongozi wa CCM na wakati mwingine kwa kulitumia Jeshi la Polisi,” alidai Mnyika.
Ushindi wa Chadema
Kuhusu ushindi wa chama hicho katika uchaguzi huo, Naibu Katibu Mkuu - Zanzibar, Salum Mwalimu alisema: “Tumefanya vizuri nchi nzima. Kwa mfano, mwaka 2009 Dar es Salaam yote tulikuwa na mitaa saba tu lakini leo hii mpaka sasa jimbo moja tu la Ubungo tumeshinda mitaa 23, unaweza kuona tunavyopiga hatua.
“Mwaka 2009, CCM walishinda kwa asilimia 96 na upinzani tulikuwa tunagawana asilimia nne, sasa leo hii katika maeneo mbalimbali tumefanya vizuri licha ya hujuma na hila zinazofanywa na CCM. Baadhi ya maeneo ambayo wanatoka mawaziri, Chadema tumeshinda hivyo wakitaka kutatuliwa matatizo yao tutawatatulia na tunawaahidi kuwatumikia vizuri bila upendeleo.
“Jimbo la Tundu Lissu la Singida Mashariki ambalo CCM wamekuwa wakisema watalichukua, kati ya vijiji 43, vijiji 41 tumevichukua na CCM wameambulia viwili, Kyela mwaka 2009, tulikuwa na mitaa miwili lakini leo tuna mitaa zaidi ya 28.”
Vyama vingine
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema licha ya uchaguzi huo kutawaliwa na hila na kila aina ya uchakachuaji wa matokeo, bado vyama vya upinzani vimefanya vizuri.
“Ni matokeo mazuri kwa Ukawa licha ya CCM kuwatumia watendaji wa kata na vijiji kuharibu lakini tumepambana hadi hayo matokeo mnayoona ni ushirikiano wetu wa Ukawa. Haiwezekani majina ya wagombea wa Ukawa ndiyo yakosewe halafu ya CCM yawe sawa, kwa nini isiwe wao iwe sisi? Tunafurahi kuona mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) tumeongeza vijiji na mitaa jambo linalotutia moyo,” alisema Profesa Lipumba.
Kuhusu mwingiliano wa wagombea wa Ukawa katika eneo moja alisema: “Hii ni changamoto ambayo ni lazima tuikubali na tuifanyie kazi ili katika uchaguzi ujao mwakani isije kujitokeza lakini kila kitu lazima kiwe na changamoto zake.”
Alisema umefika wakati uchaguzi huo ukawa unasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwani baadhi ya matatizo kama majina ya wahusika kutokuwapo na kuchanganya majina ya wagombea katika karatasi za kupigia kura yasingetokea.
Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo alisema: “Ni uchaguzi ambao umeshindwa kufanikiwa kisera na kivifaa hivyo tufike wakati sasa uchaguzi huu uwe unasimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambao wana mipango ya muda mrefu na si hawa Tamisemi wanaofanya mambo kwa kukurupuka.”
Katibu Mkuu wa muda wa ACT - Tanzania, Samson Mwigamba alisema katika Mkoa wa Katavi chama hicho kimefanikiwa kupata wenyeviti wa vijiji wawili.
Alisema mkoani Kigoma, kimepata wenyeviti wa mitaa tisa, vijiji 10, vitongoji 14 na wajumbe 53.
“Hii ni dalili kwamba upinzani sasa umedhamiria kuiondoa CCM na kama tutajipanga vyema mwakani, CCM inaondoka.”
“Bila kubadili uongozi hususan kuitoa CCM madarakani, basi mabadiliko katika nchi hii tusahau kwani huyo aliyeleta matatizo hayo anataka kuendelea kung’ang’ania kuongoza,” alisema Mwigamba.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Augustine Mrema alisema: “Mpaka sasa nimeshinda vijiji vinane katika jimbo langu la Vunjo, vitongoji ni vingi ambavyo idadi yake kwa sasa sina hapa. Wananchi wa Vunjo bado wana imani na mimi kwa kunipa heshima hiyo... Mrema bado ataendelea kuwa Mbunge wa Vunjo na hao wanaotaka kuniondoa bado hawana nafasi.”
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kukiukwa kwa makubaliano baina ya vyama vya siasa na Serikali ndiyo kumesababisha yote hayo yaliyotokea.
Alisema Septemba 8 mwaka huu, upinzani chini ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) ulikutana Ikulu Ndogo Mjini Dodoma na Rais Jakaya Kikwete na kukubaliana uchaguzi huo usifanyike mwaka huu, jambo ambalo halikufuatwa.
Alisema walikubaliana uchaguzi ufanyike Machi mwakani ili kupisha marekebisho ya sheria ya uchaguzi ili uchaguzi huo usimamiwe na NEC lakini makubaliano hayo yalitupiliwa mbali.
“Licha ya upinzani kufanya vizuri lakini tungefanya zaidi ya hapa kama uchaguzi ungesimamiwa na NEC,” alisema Mbatia.
Chanzo: mwananchi.co.tz
0 comments:
Post a Comment