2014-12-31

Kweli Kabisa;Ufisadi ni mbolea ya kuchochea ugaidi






Huko Nigeria mwanajeshi hunyongwa anapokataa kupigana dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram. Na karibuni huko Kenya ilipitishwa Sheria ya Usalama, ambayo pindi busara haitatumika itaweza ikaipeleka nchi hiyo pabaya na hata kuonekana mbele ya watu wa ndani na nje kwamba ni dola ya kipolisi.


Serikali za nchi hizo mbili za Kiafrika- moja iko Afrika Magharibi na nyingine Afrika Mashariki, zina kila sababu ya kupambana na kuwazuia magaidi wanaohatarisha usalama wa raia na mali zao. Lakini mara kadhaa malengo mazuri humalizikia kwa matokeo mabaya na vurugu, ikiwa uangalifu hauchukuliwi. 



Pia ikiwa watekelezaji wanakuwa wakakamavu na kutokuwa tayari kuzidurusu hatua zao kila wakati kama zinaambatana na tunu muhimu za kuheshimu utu wa mwanadamu. Kuna wasiwasi kwamba hatua zilizochukuliwa na serikali za nchi hizo mbili zinakosa malengo na hazitasaidia kuondoa mzizi wa fitina wa ugaidi.


Mashambulzi ya kigaidi


Katika kisa cha karibuni cha mashambulio ya magaidi huko Nigeria ambayo yametia fora mwaka 2014, magaidi wa Boko Haram waliwateka nyara watu kadhaa. Msemaji wa Serikali ya Nigeria alikuwa hana zaidi la kusema ila kushtushwa, kusikitishwa na kukilaumu kitendo hicho.


Baada ya shambulio hilo lililofanywa karibu na Gumsuri, kijiji kilichoko katika Mkoa wa Kaskazini mwa Borno, mambo yalibadilika na kuwa vurugu tupu. Barabara nyingi zilikuwa hazipitiki na mawasiliano kupitia simu za mikononi yalikuwa hayawezekani. Kwa hakika ilichukua siku kadhaa hadi sura kamili ya tukio hilo kupatikana katika mji mkuu wa Abuja.


Inasemakana wanavijiji walikusanywa na kuhamishwa kama ng’ombe, si chini ya 35 kati yao waliuawa kwa risasi. Habari nyingine zinasema wanawake na wasichana 200 walipakiwa katika malori na haijulikani walikopelekwa.


Japokuwa kikundi cha Boko Haram halijakiri kuhusika, lakini mabingwa wa harakati za magaidi wanasema shambulio hilo jipya lina sura kwamba Boko Haram ndio walioufanya ukatili huo. Idadi ya ukatili unaofanywa na kikundi hicho, ambacho bila ya haki kinajigamba kinausemea Uislamu, imeongezeka hivi karibuni.


Mwaka wa 2014 maelfu ya watu wasiokuwa na hatia wameuawa Nigeria na kundi hilo, ambalo tangu mwaka 2009 limekuwa likidai kuweko dola huru la Ukhalifa ( Mrithi wa Mtume Muhammad). Kwa mujibu wa jumuiya zinazotoa misaada, Wanigeria milioni 1.5 wamekimbilia kwenye mikoa ilio na amani au wameelekea nchi jirani kutokana na kitisho cha Boko Haram.


Jeshi la Nigeria linaonekana kuelemewa, haliwezi kuwalinda raia na zaidi haliungwi mkono na raia. Linakosa silaha za kisasa. Maafisa pamoja na wanajeshi wao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamika kwamba hawana silaha za kutosha kuweza kukabiliana na kuwashinda wapiganaji wa Boko Haram walio na silaha za kutosha.


Nyingi ya silaha waliozonazo Boko Haram ni zile zilizoachwa na wanajeshi wa serikali wanaokimbia kutoka uwanja wa mapigano. Mara kadhaa kumetokea visa vya wanajeshi wa serikali huko Borno kukataa kutii amri za wakuu wao. Wanajeshi hao husimamishwa mbele ya mahakama za kijeshi wakishtakiwa kuwa waoga mbele ya adui au kufanya uasi na 54 kati yao wameshapewa hukumu ya kifo.


Lakini haifikiriwi kwamba hukumu kali za kifo dhidi ya wanajeshi waoga itaibadilisha hali ya mambo inayozidi kuwa mbaya huko Nigeria. Ingekuwa bora kuushughulikia mzizi wa tatizo hilo la ugaidi wa Nigeria.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...