2014-12-31

POLENI;Kenya na ubovu wa upinzani, Katiba na tatizo la usalama

Tangu wiki iliyopita, Bunge la Kenya limeendelea kujadili muswada wa mabadiliko ya Sheria (Security Laws Amendment Bill 2014) ambao ulitarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika mustakabali mzima wa usalama wa nchi. 



Ikumbukwe Kenya imekuwa ikikabiliana na mfululizo wa mashambulizi kutoka kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab kwa zaidi ya miaka miwili sasa. Zaidi ya watu 200 wanakisiwa kuuawa kinyama hadi sasa.


Muswada huu uliishia kwa wabunge kutwangana ngumi bungeni, jambo ambalo ni la aibu mbele ya Wakenya.


Muswada huo ulilenga vyombo vyote vya usalama, jeshi, polisi, uhamiaji na Huduma ya Intelijensia ya Taifa (National Intelligence Services), kuwa na mamlaka ya kukabiliana na ugaidi.


Sheria hii ni kali dhidi ya watumishi wa serikali wanaotoa vitambulisho na nyaraka muhimu, wananchi wanaowahifadhi na kuwasaidia magaidi na taasisi za kidini na kiraia zinazochochea vitendo vya kigaidi.


Kabla ya kupitishwa muswada huo, vitengo hivyo vilikuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na magaidi lakini baada ya kuvurugwa na katiba mpya, mfumo mzima wa usalama unaonekana kuyumba.


Mabadiliko mengine ni kama vile kifungo cha miaka isiyozidi mitatu kwa kosa la kutoa habari inayoweza kukwamisha jitihada za kukabiliana na ugaidi.


Vilevile, kuna kifungo cha miaka isiyozidi 20 kwa matumizi ya bomu katika mashambulizi ya kigaidi.


Mtu yeyote atakayepatikana na silaha ndani ya nyumba za ibada au kuhubiri falsafa za kigaidi au uchochezi wa kidini atatumikia kifungo cha miaka isiyozidi 30. 



Pia, muswada huo ulikusudia kumpa Rais Kenyatta mamlaka ya kuteua mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) baada ya mamlaka kuondolewa na katiba mpya na kuipa tume mamlaka hiyo.


Tatizo la usalama Kenya linatokana na katiba ambayo iliweka sheria ambazo zinaifunga mikono Serikali kuwafuata na kuwahukumu magaidi au watu wenye nia mbaya na kuathiri mtiririko mzima wa usalama. 



Kwa mfano, katiba inasema mtu yeyote asizuiliwe na polisi zaidi ya saa 24, lakini muswada unapendekeza kushikilia mtuhumiwa wa ugaidi zaidi ya muda huo.

0 comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...